LIGI mbalimbali duniani kote zimefikia tamati na stori kubwa zinazofuatiliwa zaidi kwasasa ni usajili wa wachezaji.
Kama ilivyo kwa Mataifa mengine duniani, ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015 ilifikia tamati mei 9 mwaka huu, Yanga wakitwaa Ubingwa.
Kwasasa 'Headlines' za magazeti mengi ya Tanzania, redio, Televisheni na mitandao ya kijamii ni usajili pamoja na tetesi zake.
Simba, Yanga ni timu kongwe nchini zenye umaarufu mkubwa na msuli wa fedha kutoka mifukoni mwa watu na sio kwenye akaunti za klabu.
Wakati huu wa usajili, klabu hizi mbili zinaongoza kuwania wachezaji wote waliotikisa ligi kuu msimu uliopita wakifuatiwa na klabu tajiri ya Azam fc ambayo mpaka sasa haijaonesha makeke yoyote zaidi ya kuwaongezea mikataba wachezaji wake na kutafuta kocha mpya anayerithi mikoba ya Mcameroon aliyefutwa kazi, Joseph Marius Omog .
Muingereza Stewart John Hall ndiye amerejeshwa kuinoa Azam fc, kilichobaki ni kutangazwa tu.
Tayari Yanga imemnasa kiungo mshambuliaji wa Mbeya City fc, Deus Kaseke na kumsainisha mkataba wa miaka miwili juzi, wakati Simba nao wamemsajili Peter Mwalyanzi wa Mbeya City pia na kumpa mkataba kama huo.
Usajili huu umetikisa vichwa vya habari kutokana na namna Simba, Yanga walivyopigana vita baridi kuwania saini za wanasoka hawa.
Wanaofuatilia mtandao huu wameshapata stori za kusisimua zikieleza namna timu hizi mbili zilivyowania saini za Kaseke na Mwalyanzi.
Jana kwa makusudi kabisa, mtandao huu ulichapisha simulizi maalumu ya Kaseke na Mwalyanzi walivyopiganiwa na klabu za Simba, Yanga. (Rejea habari za jana).
Nimejifunza mambo kadhaa katika usajili wa wachezaji hawa wawili na nadhani nitaendelea kujifunza zaidi kwasababu wengine watasajiliwa kwa staili hiyo hiyo;
Kwanza; Wachezaji wa Kitanzania wameendelea kuutbitishia ulimwengu wa soka kwamba hawajitambui; achana na mambo ya uwanjani ambako uchovu wao tunaujua.
Wanandinga wengi wa Tanzania hawajui namna ya kufanya biashara ya usajili na haki zao za msingi.
Nimesikitishwa sana kuona Kaseke anashindwa kulala kwasababu ya simu za viongozi wa Simba na Yanga.
Inafika wakati analindwa bila kujijua, mara anahamishwa Hoteli 'usiku mkubwa' na viongozi wa Yanga wakiwakwepa watani wao Simba.
Stori ya Kaseke inavutia, lakini kuna jambo kubwa la kujifunza kutoka katika purukushani hiyo.
Ulaya hakuna usajili wa hivyo, watu wanafanya mambo kwa weledi. Hatuwezi kulingana nao, lakini kuna baadhi ya mambo si vibaya kujifunza.
Kaseke alitakiwa asije kabisa Dar es salaam wakati wa kuzungumza na Yanga. Kama kulikuwa na ulazima wa yeye kuja, basi angeambatana na wakala au meneja wake mwenye weledi wa sheria za usajili wa wachezaji na sio mjomba, kaka au Shangazi yake.
Wakala wa Kaseke ndiye anayepaswa kusumbuana na Yanga hadi usiku wa manane . Simu ya wakala ndio inatakiwa kuwa 'busy' akisumbuana na viongozi na si mchezaji.
Lakini kwa kutojua umuhimu wa wakala, Kaseke ameyavaa majukumu yasiyomuhusu, matokeo yake halali, muda wote anasumbuliwa.
Ukimsikiliza Kaseke anakwambia ana wakala wake ambaye alikuwa anawasiliana naye anapozungumza na Yanga ,Simba, lakini ukweli ni kwamba mchezaji huyo hana wakala zaidi ya wajanja wajanja ambao yawezekana ni ndugu zake.
Wakala anatakiwa kuwa mtu safi, anayejua sheria, anayejua haki za msingi za wachezaji, kiujumla hana ubabaishaji.
Inaumiza kuona Peter Mwalyanzi anasafirishwa na Simba kutoka Mbeya kwa muda mfupi na kusaini mkataba. Ukisikiliza maelezo yake, hakupata muda wa kutafakari, kusoma mkataba na kupitia vipengele vyote kwa umakini. Anasema alikuwa na ndugu yake anayejua sheria, ni nani huyo?. Mwanasheria au wakala wa mchezaji sio mtu wa siri, ni mtu wa wazi kabisa na ndiye anayehusika na ofa zote za mchezaji.
Simba walimuharakisha Mwalyanzi kusaini, si kwasababu hawajui kama anatakiwa kupewa muda wa kupitia mkataba, anatakiwa kuondoka nao kabisa nyumbani kwake ili akajadiliane na wanasheria wake kama kweli unastahili, halafu anarudisha majibu kama amekubali au kuna vipengele anataka viondolewa au kuongezwa.
Simba wakikamilisha marekebisho, anarudishiwa tena na kuupitia upya, baada ya hapo anasaini.
Lakini mchezaji anakwambia ametoka Mbeya kwa ndege saa 12:00 asubuhi, saa sita baadaye anatangazwa kusajiliwa. Tena anaeleza mwenyewe kuwa tulikuwa kwenye mazungumzo ya haraka na Simba.
Wachezaji wetu wanahitaji kuelimishwa sana, hawajui kitu, wanadanganyika na mamilioni ya Simba au Yanga, ikifika wakati wa kuachwa wanakosa msaada.
Kikubwa waelimishwe umuhimu wa kuwa na mawakala na wanasheria ili kupata haki zao.
kitu cha pili; Uswahili wa viongozi wa Simba na Yanga; lipo kundi kubwa la watu wanaonufaika na usajili wa wachezaji. Kwa bahati mbaya pesa za usajili wa klabu hizi mbili zinatoka mifukoni mwa matajiri na wadau wa timu hizo.
Mtu kama Yusuf Manji (Mwenyekiti wa Yanga) ameshaingizwa sana mkenge na wajanjawajanja inapofika suala la usajili. Kule Simba nako kuna matajari kama Azim Dewji na Zacharia Hans Poppe n.k.
Hawa watu wana hela nyingi na wana wapambe wengi wanatumika kusajili wachezaji. Timu kama Simba, haina kocha kwasasa, lakini watu wanakomaa kusajili kama kawaida.
Inawezekana wachezaji wengine walipendekezwa na Goran Kopunovic aliyemaliza mkataba na klabu hiyo, lakini uzoefu unaonesha viongozi ndio wanaosajili wachezaji, halafu Kocha unakutana nao juu kwa juu, hii ni hatari sana katika soka.
Wapambe wa matajiri wananufaika na posho pamoja na 10% wanazopata katika usajili. Stori nyingi zinazungumzwa, kiongozi anamwambia mchezaji nakufanyia mchongo usajiliwe Simba, utanipigia 10%.
Mchezaji anakubali kwasababu amesikia Simba na Yanga.
Kiukweli kama unacheza soka Tanzania hii ni ngumu kukataa ofa ya Simba na Yanga kwasabababu utapata umaarufu na maslahi ya juu kuliko Mgambo JKT, Mbeya City, Stand United n.k.
Ukiangalia namna wapambe wasiokuwa wataalamu wakisajili wachezaji kwa mbwembwe unagundua haraka kuwa wanawalalia wachezaji.
Hebu jiulize kwanini mikataba ya wachezaji haiko wazi kama wenzetu Ulaya?
Ukitaka kujua mchezaji kasajiliwa kwa shilingi ngapi? amepewa zote au hapana?, mashahara kiasi gani? vipengele vya mkataba ikiwemo posho vimeandikwaje? basi utapigwa chenga mno, kuanzia viongozi mpaka mchezaji wanadai ni siri ya pande mbili.
Lakini ukisikia Cristiano Ronaldo anasajiliwa Real Madrid, basi wakala wake na klabu wanaanika ada ya usajili, mshahara, bonasi zake na vipengele vyote muhimu vya mkataba.
Wakala hawezi kutangaza kumuuza mchezaji bila kutaja dau, lazima aseme ili watu wajitathimini, hili sio suala la chumbani, ni biashara ya wazi kabisa.
Lakini kwa timu zetu za Simba, Yanga na nyinginezo, utasikia Said Ndemla kasajiliwa kwa miaka mitatu, Kaseke, Mwalyanzi miaka miwili.
Je, Dau la usajili ni shilingi ngapi? mashahara je? ukiona mtu anajua basi ana watu wa ndani wanaompa taarifa kutoka klabuni. Mtu wa kawaida hawezi kujua.
Wachezaji wengine ukiwauliza wamekusajili kwa shilingi ngapi hawawezi kusema, labda wanaogopa kukabwa, lakini kama wangekuwa na mawakala wenye uweledi, biashara ingekuwa wazi.Wakala anatangaza bei na mashahara anaotaka mchezaji wake alipwe.
Ukiona watu wanapenda sana usiri, basi ujue kuna magumashi mengi.
Kuna siku nimezungumza na mchezaji mmoja aliyewahi kusajiliwa Yanga (jina ninalo). Nilimuuliza umesajili kwa kiasi gani na mkataba wako unasemaje kuhusu kuondoka ukipata timu pamoja na bonasi?
Akaniamba kaka mimi sijui kitu, nimeona tu kiasi cha mshahara na ada ya usajili nimeanguka sahihi.
"Mkataba wenyewe umeandikwa kiingereza, ujue mimi sielewi kiingereza, nimeona mshahara na ada ya usajili nimesaini". Aliniambia mchezaji huyo.
Niliumia kwasababu hajui anachofanya, baadaye aliachwa hovyo hovyo tu na kwenda timu ya chini.
Kuna lundo kubwa la wachezaji wa aina hii, hawajui kiingereza hata kama wamesoma sekondari mpaka kidato cha sita, kuna maneno ya kisheria ambayo hata mtu wa chuo kikuu anahitaji msaada wa wataalamu wa sheria, sembuse Kaseke, Ndemla, Mwalyanzi?
Wachezaji wa Bongo wanadhulumiwa mno, wanakimbilia Simba na Yanga kwasababu ndio timu kubwa, lakini wakiachwa wanakosa haki zao za msingi.
Jiulize Kaseke au Mwalyanzi alikuwa analipwa shilingi ngapi Mbeya City na alisajiliwa kwa shilingi ngapi? halafu watu wanamuwekea mezani milioni 35, unafiriki atapata muda wa kusoma mkataba? atasaini tu.
Viongozi wanajua udhaifu wa wachezaji wetu, wengi wanatokea kulipwa hela za mboga, wakiweka burungutu la fedha mezani, hakuna kujiuliza zaidi ya kusaini.
Lakini wangekuwa na mawakala wa maana, watu wazima wanaojua sheria, wasingeweza kupaparika.
Mawakala wanajua kuhoji, hiki mbona kiko hivi, sitaki iwe hivi, weka hivi, mwisho wa siku wanatengeneza biashara ya ya maana.
Kuna haja ya wanandinga kusikiliza redio, kutazama TV, kusoma magazeti na mitandao ili kupata uchambuzi wa maana wanaoandika watu kuhusu wao.
Waliowengi hawana taarifa na wengi wametokea katika mazingira ambayo milioni 40 walikuwa wanazisikia kwenye magazeti, wakipewa wanatetemeka. Ndio maana leo nasema wajifunze na kufundishwa namna ya kukabiliana na presha kama hizo.
Nawatakia siku njema! ni halali yako kutoa maoni na kukosoa mtazamo wangu
Na Baraka Adson Mpenja
Mtangazaji wa mpira wa Miguu-Azam TV
Tel: 0712461976
0 comments:
Post a Comment