WAKATI Azam fc wakidai idadi ya wachezaji wa kigeni ligi kuu soka Tanzania bara iongezwe kutoka idadi ya sasa ya watano, kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi amepinga mtazamo huo.
Hoja ya Azam kutaka idadi iongezeke ni kupata wachezaji
wengi wa kigeni watakaowasaidia katika michuano ya kimataifa pamoja na kuwapa
changamoto wachezaji wazawa ndani ya timu hiyo.
Makamu bingwa hao wa ligi kuu msimu wa 2014/2015 wanadai
wamejifunza kwa TP Mazembe na El Merreikh ambao wamesheheni wanasoka wengi
kutoka nje ya nchi zao.
Azam wakitoa hoja hizo, Mwambusi amesema haoni haja ya
kuongeza wachezaji wa kigeni bali vipaji vya ndani viangaliwe zaidi.
“Siungi mkono kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni katika
soka letu la Tanzania kwasababu sisi tuna wachezaji wengi wenye vipaji. Muhimu
ni wachezaji wetu kujitambua kwanza, halafu viongozi wa klabu zetu wanawachukuliaje
wachezaji wetu?” Amesema Mwambusi na koungeza: “Saa nyingine watu wanataka
kusajili kwa fasheni, vilabu vikubwa vinashindana kusajili wachezaji wa nje,
tusichukue wachezaji kwasababu tu tunataka kushindana na fulani, tuwachukue
wachezaji wa nje kwasababu wana kiwango cha juu ili waje kuleta changamoto hapa
kwetu”.
“Kwa idadi iliyopo inatosha kwasababu tumeshaona hata hao
watano kuna wengine wanakaa nje kwa kushindwa na wazawa. Mimi nasema wachezaji
wetu wanatakiwa kujitambua tu ili wajue kuwa mpira ni kazi, wajitoe na kucheza
kwa juhudi zote uwanjani ili kuweza kuendeleza soka letu”.
“Wanaweza kuja hata wachezaji 11 wa kigeni, sijui kama itatusaidia,
kikubwa tuangalie tulipojikwaa, tusiangalie tulipoangukia. Viongozi wanaweza
kusema vijana wetu hawajitambui, sawa!, watajitambuaje? Kila mtu kwa nafasi
yake katika mpira afanye kazi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na kwa umakini
mkubwa, viongozi wanaotawala soka katika nchi yetu wana nia kweli ya kuendeleza
soka letu?. Tunaweza tukakubali kuleta wachezaji wengi, lakini tusipopita
kwenye mfumo sahihi hatuwezi kufika kokote”.
0 comments:
Post a Comment