Tuesday, May 19, 2015



Kopunovic ameachana na Simba

'Tangu mwaka 1998, Simba imepita chini ya makocha wakuu 19 ikiwa ni wastani wa kocha mmoja kila mwaka. Achilia mbali Jamhuri Kihwelo 'Julio' ambaye kwa nyakati tofauti alikuwa akishika jukumu la kocha mkuu kwa muda.'

UONGOZI wa Simba ulikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari jana ukieleza kuachana na kocha mkuu Mserbia Goran Kopunovic.

Kopunovic (48) ameiongoza Simba katika mechi 18 kati ya 26 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu ikimaliza nafasi ya tatu, moja zaidi ya msimu uliopita.

Katika mechi hizo 18 Simba ilipoteza mechi nne dhidi ya Stand United, Mgambo Shooting na mbili dhidi ya Mbeya City, ikashinda 12 na kutoka sare mara mbili.

Mbali na mafanikio hayo VPL, Kopunovic pia aliiongoza Simba katika mechi tano kati ya sita za michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar ambako mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara walitwaa ubingwa.

Kocha huyo alikuwa jukwaani wakati Simba ikifungwa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan visiwani humo siku ya Mwaka Mpya, ikiwa ni saa chache baada ya kusaini mkataba mfupi wa miezi sita kuinoa timu hiyo ya Msimbazi.

Sababu kuntu ya kutomwongeza mkataba mpya Kopunovic ilielezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, kuwa ni kitendo cha kocha huyo kutaka alipwe mshahara mkubwa na donge nono la kusaini mkataba (signing fee).

"Simba tunasaidiwa kulipa mishahara na wadhamini wetu, lakini fungu ambalo Kopunovic anataka ni asimilia 90 ya peza zote za wadhamini. Hatutaki kuwa na madeni mengine zaidi maana mpaka sasa kuna wachezaji wanatudai," alisema Hanspope.

Binafsi ninaupongeza uongozi wa Simba kwa kuchukua uamuzi huo mgumu wa kuachana na mtaalam huyo wa ufundi ili kuiepusha klabu kuingia katika ukata wa fedha, lakini unapaswa kujifunza kutokana na makosa.

Kosa la kwanza la Simba katika usajili wa Kopunovic ni kitendo cha uongozi wa klabu hiyo kumpa kocha huyo mkataba mfupi wa miezi sita. Ninaamini kuwa kabla ya kumpa mkataba, Simba walikuwa wamefuatilia uwezo wake, hivyo hapakuwa na haja ya kumpa muda wa miezi sita ya matazamio.

Pili, Simba imekuwa ikifanya vibaya katika michuano mbalimbali kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya wataalam wa benchi la ufundi. Baadhi ya makocha wapya wamekuwa wakiivuruga timu hiyo kwa kutoa ushauri usiofaa. Msimu huu Simba ilimtema mfungaji bora wa VPL msimu uliopita, Amissi Tambwe, kutokana na ushauri wa aliyekuwa kocha mkuu, Mzambia Patrick Phiri.

Tatu, mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha pia yamekuwa yakisababisha hasara ya mamilioni ya shilingi kwa klabu hiyo. Mfano Mcroatia Zdravko Logarusic alifukuzwa akiwa ametumikia mwezi mmoja tu katika mkataba wake wa mwaka mmoja na klabu ikalazimika kumlipa kwa kukiuka haki za kimkataba.

Hivi karibuni Mserbia Milovan Cirkovic alirejea nchini akiidai Simba dola za Marekani 32,000 (Sh,. milioni 64). Hali hiyo pia iliwahi kumpata Mganda Mosses Basena ambaye alirudi kwa mara ya pili kuinoa Simba huku akiidai Sh. milioni 99 za mshahara wake. Hii ni mifano michache tu.

Nne, kikosi cha Simba kimekuwa kikiathirika kiuchezaji kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha. Ikuknbukwe kuwa kila kocha anakuja na mfumo wake, jambo ambalo katika misingi ya ufundishaji ya michezo (Principles of Sport Training) ni wazi limekuwa likiwachanganya wachezaji.

Kwa kifupi, tangu mwaka 1998 timuatimua ya makocha ilipoanza, Simba imenolewa na makocha wakuu 19 ikiwa ni wastani wa kocha mmoja kila mwaka (miaka 17 makocha 19.

Makocha walioinoa timu hiyo tangu 1998 ni Mohamed Kajole (1998), David Mwamaja (1999), Mrundi Nzoyisaba Tauzany (1999-2000), Abdallah 'King' Kibadeni (2000), Syllersaid Mziray (2000), Mkenya James Siang'a (2001-2004), Phiri (2005), Mbrazil Neider dos Santos (2006), Talib Hilal raia wa Oman (2007), Cirkovic (2009), Phiri (2010), Mbulgaria Krasmir Benziski (2011), Basena (2012), Cirkovic (2012), Mfaransa Patrick Liewig (2013), Kibadeni (2013), Logarusic (2013-2014), Phiri (2014) na Kopunovic (2015).

Ninafikiri ipo haja uongozi wa Simba kuajiri kocha atakayedumu kwa muda mrefu ili kuepuka gharama za usajili wa makocha kila mwaka na changamoto nyingine zitokanazo na mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha.

*Imeandikwa na Sanula Athanas, Mwandishi wa michezo mwandamizi wa gazeti la NIPASHE.

CHANZO: NIPASHE la Jumatatu Mei 18, 2015

0 comments:

 
https://www.sexmutant.com/ https://www.sexindrag.com/ porn movies sex videos hd porno video