Busungu akisaini Yanga leo
MABINGWA wa soka Tanzania bara, Young Africans wameendelea kuimarisha kikosi chao na leo hii wamekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Mgambo JKT, Malim Francis Busungu.
Busungu amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga kuanzia msimu ujao.
Nyota huyo ambaye kwasasa yupo timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilikuwa kwenye rada za Simba na walifanya mazungumzo mara kadhaa, lakini walishindwa kufikia makubaliano.
Yanga sasa wamesajili wachezaji wanne wa ndani kwani awali waliwasainisha Deus Kaseke kutoka Mbeya City, kipa Benedictor Tinocco kutoka Kagera Sugar na Mlinzi wa kushoto, Mwinyi Hajji kutoka KMKM.
Kwa mara nyingine unaweza kusema Yanga imewapiga bao Simba kama walivyofanya kwa Kaseke.
Simba walianza kuzungumza na Kaseke na walifikia hatua nzuri, lakini Yanga wakaingia katikati na kumnyakua.
Vivyo hivyo kwa Busungu, Simba walikuwa kwenye mazungumzo ya kina, lakini Yanga wamefikia dau na kumsajili leo.
Ingawa taarifa za ndani zinasema Busungu ameshusha dau kidogo ukilinganisha na alilotaja kwa wekundu wa Msimbazi.
Tayari katibu mkuu wa Yanga, Dr. Jonas Tiboroa ametangaza leo kwamba wamekamilisha usajili wa wachezaji wa ndani na sasa wanaanza harakati za usajili wa kimataifa, lakini wanasubiri majibu ya mapendekezo yao waliyowasilisha TFF wakiomba kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano wa sasa mpaka angalau 8.
0 comments:
Post a Comment