Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Ramadhani Singano 'Messi' wa Simba anahusishwa kutaka kujiunga na matajiri wa Tanzania, klabu ya Azam.'
WAKATI sakata la usajili wa winga Ramadhani Singano 'Messi' na Simba limeendelea kuwa gumzo nchini, uongozi wa Simba umesema kuwa wachezaji wake wenye umri mdogo wameanza kudanganyana kuhusu thamani zao.
Messi (21) ameingia katika msuguano na klabu hiyo ya Msimbazi baada ya meneja wake, Hamis Said, kudai kutoutambua mkataba wa miaka mitatu kati ya nyota huyo na klabu hiyo ya pili kwa ukongwe nchini.
Katika mahojiano na mtandao huu jijini hapa leo, Said amesema mkataba wa miaka miwili kati ya Messi na Simba umefikia tamati baada ya kumalizika kwa msimu wa 2014/15 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
"Ninachotambua mkataba uliokuwapo ni wa miaka miwili. Tunashangaa kuambiwa kwamba mchezaji wangu ana mkataba wa miaka mitatu na Simba ambao utamalizika msimu ujao," amesema Said.
Zacharia Hanspope, mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, amesema jijini hapa leo kuwa Messi aliongeza mkataba wa mwaka mmoja zaidi kuitumikia klabu hiyo katika mkataba wake wa miaka miwili.
"Mkataba uliopo TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ni wa miaka mitatu na Singano ametia saini na dole gumba. Je, sisi tumeghushi dole gumba lake" Hiyo ni kesi ya jinai," amesema Hanspope na kuongeza:
"Vijana wetu wanakaa na kuanza kudanganyana wana thamani kubwa ya Sh. milioni 50, 80 na kadhalika wakati hata Sh. milioni 10 hawafiki. Wakati tunamwongeza mshahara Singano, tuliongeza pia mwaka mmoja katika mkataba wake.
"Tulikuwa na mpango wa kumpeleka Singano Australia, lakini ninaona anaharibu. Watambue kwamba hata Yanga wametuuliza kuhusu wachezaji wetu na tukawaambia ukweli kuhusu (Said) Ndemla na hata Singano."
Matajiri Azam FC wanadaiwa kutaka kumsajili winga huyo kuimrisha safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na Mrundi Didier Kavumbagu na Muivory Coast Kipre Tchetche.
0 comments:
Post a Comment