Monday, May 18, 2015


Jonas Mkude

WIKI mbili zilizopita kocha mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij, aliita wachezaji 28 kwa ajili ya kuunda kikosi cha timu hiyo ya taifa inayoshiriki michuano ya COSAFA huku akiwajumuisha kikosini wachezaji majeruhi wa muda mrefu na wasiokuwa na namba katika vikosi vya kwanza vya klabu zao.

Kikosi cha Mdachi huyo pia hakika nyota watatu wanaokipiga DR Congo, Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu. Stars iliyopo Afrika Kusini ina wachezaji wawili wanaocheza nje ya mipaka ya Tanzania, Juma Liuzio, anayeitumikia klabu ya Zescio ya Ligi Kuu ya Zambia na Mwinyi Kazimoto anayekipiga katika klabu ya Al Markhira nchini Qatar.

Kuitwa katika kikosi cha Stars cha COSAFA kwa wachezaji majeruhi wa muda mrefu na wasiokuwa na uhakika wa namba katika vikosi vya kwanza za klabu zao, kulionekana kuwachefua wachambuzi wa soka nchini huku baadhi yao wakienda mbali zaidi kwa kuhoji uwezo wa Nooij.

Wachezaji wa Stars walioko mjini Rustenburg nchini Afrika Kusini ni makipa Deogratius Munishi 'Dida' (Yanga) na Mwadin Ali na mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris (wote Azam), Oscar Joshua (Yanga), Hajji Mwinyi (KMKM), Joram Mgeveke (Mwadui FC) na Salim Mbonde (Mtibwa). Viungo ni Abdi Banda, Said Ndemla (wote Simba), Said Juma, Hassan Dilunga (wote Yanga) na Kazimoto.

Safu ya ushambuliaji inaundwa na Liuzio, Simon Msuva (Yanga), Ibrahim Ajibu (Simba), John Bocco 'Adebayor' (Azam) na Mrisho Ngasa (Yanga/ Free States).

Nyota wengine walioitwa na Mdachi huyo kwenda kwa Mzee Madiba, Afrika Kusini, lakini wakakwama kutokana na matatizo ya kiafaya na kifamilia ni kipa Aishi Manula (Azam), beki Hassan Isihaka (Simba), winga Haroun Chanongo (Stand United), winga Kelvin Friday (Azam), beki Nadir Haroub 'Cannavaro' (Yanga), viungo Salum Telela (Yanga), Amri Kiemba, Salum Abubakar 'Sure Boy' (wote Azam) na beki Kelvin Yondani (Yanga).

Kutoitwa kwa Samata na Ulimwengu katika kikosi cha Nooij pengine kumetokana na ratiba ya michuano hiyo kutokuwa katika kalenda ya matukio ya soka ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na maandalizi ya Stars kuelekea michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Binafsi ninaheshimu mtazamo wa Nooij na benchi la ufundi la Stars lililoita kikosi ambacho leo kinatupa karata ya kwanza ya COSAFA mwaka huu kwa kuivaa Swaziland, lakini ninaamini kuna wachezaji wazuri ambao hawajaitwa licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuiwakilisha nchi katika michuano hiyo ya Ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Kifuatacho ni kikosi cha wachezaji ambao binafsi ninaamini wanastahili kucheza Taifa Stars, lakini wameachwa kimakosa katika safari ya COSAFA mwaka huu na Nooij. Karibu...

1. ALLI MUSTAFA 'BARTHEZI' - YANGA
Unapoyazungumzia mafanikio ya Yanga msimu huu, bila shaka hutaacha kulitaja jina la Barthez, kipa aliyeweka rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, Yanga ilifungwa bao moja huku ikifunga mabao tisa katika mechi nne. Barthez alidaka mechi tatu akifungwa bao lililowang'oa katika hatua ya robo fainali dhidi ya JKU.

Baada ya michuano hiyo Barthez alihamishia makali yake VPL akimpoka namba Dida na akacheza mechi sita mfululizo bila kufungwa bao hadi alipotunguliwa bao moja na Peter Mapunda katika ushindi wa Yanga wa mabao 3-1 dhidi ya City jijini Mbeya.

Barthez pia alifanya vizuri katika michuano ya Kombe la Shirikisho waliyofungwa mabao matano na kufunga tisa. Dida alidaka mechi ya mwisho dhidi ya Etoile Sportive du Sahel (ESS) na kufungwa bao 1-0 mjini Sousse, Tunisia.

Uwezo mkubwa ulioonyeshwa na Barthez msimu huu tangu alipompoka namba Dida katika kikosi cha kwanza Januari 2 mwaka huu, ndiyo umechangia Yanga kutwaa ubingwa wa 25 wa Tanzania Bara huku ikiruhusu nyavu zake kutikishwa mara 18. Ninafikiri hastahili kuwa nje ya kikosi cha Stars cha sasa.

2. KESSY RAMADHANI - SIMBA
Mabeki wa pembeni kulia waliofanya vyema msimu huu nchini ni Juma Abdul (Yanga), Salum Kimenya (Tanzania Prisons) na 'kiboko yao' Kessy Ramadhani wa Simba.

Beki mkongwe Said Mkopi ameonekana wazi kushindwa kuziba pengo la Kessy katika kikosi cha Mtibwa tangu nyota huyo aihame timu hiyo na kujiunga na Simba dirisha dogo Desemba mwaka jana.
Kessy ameudhihirishia umma kwamba ana uwezo mkubwa wa kucheza katika kikosi chochote akiwa beki wa pembeni kulia na kutekeleza kikamilifu jukumu la kulinda na kupandisha mashambulizi. Ninafikiri si sahihi Taifa Stars ya sasa kutokuwa na beki wa aina ya Kessy.

3. HASSAN MWASAPILI - MBEYA CITY
City imefungwa mabao 22 msimu huu ikishika nafasi ya nne sawa na Prisons katika orodha ya timu zilizofungwa mabao machache zaidi. Ubora wa beki wa pembeni kushoto, Hassan Mwasapili, katika kulinda na kupandisha mashambulizi, umekisaidia kikosi cha Juma Mwambusi kumaliza nafasi ya nne katika msimamo wa VPL. Ninaamini Mwasapili ni bora kuzidi Joshua. Uwezo wake unaweza kulinganishwa na beki wa pembeni kushoto wa Mtibwa Sugar, David Luhende. Ninafikiri Nooij alipaswa kutambua umuhimu wa mkali huyo (Mwasapili) na kumjumuisha katika kikosi cha Stars ya COSAFA.

4. ANDREW VINCENT - MTIBWA SUGAR
Ubora wa beki wa kati Salim Mbonde katika kikosi cha Mtibwa Sugar unatokana na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwa Vincent. Licha ya kuyumba kwa safu ya ulinzi ya Mtibwa kuanzia Januari, Vincent alishirikiana vyema na Mbonde kupunguza idadi ya mabao ya kufungwa ya timu yao.

Mtibwa imefungwa mabao 26 msimu huu ikiwa ni wastani wa goli moja kwa kila mechi. Safu ya ulinzi iliyumba baada ya kuuzwa kwa Kessy dirisha dogo. Kukosekana kwa mbadala wa beki huyo kuliifanya timu hiyo ifungwe mabao mengi zaidi mzunguko wa pili kikiwamo kipigo cha 5-2 dhidi ya Azam FC.

5. LUGANO MWANGAMA - PRISONS
Ingawa ameweka rekodi ya kusababisha penalti nyingi zaidi msimu huu katika kikosi chake (penalti mbili), Mwangama amekuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Mbwana Makata cha Prisons. Akishirikiana vyema na beki mwingine wa kati, Nurdin Chona, Mwangama ametoa mchango mkubwa kuinusuru timu yake kuporomoka daraja akiimarisha safu ya ulinzi ambayo imeuhusu mabao 22 sasa na safu ya ulinzi ya City, kunakozifanya timu hizo kushika nafasi ya nne kwa kufungwa mabao machache zaidi msimu huu.

6. JONAS MKUDE - SIMBA
Amecheza kwa kiwango cha juu katika kikosi cha Simba kwa muda mrefu, lakini anaonekana kutolivutia benchi la ufundi la Stars. Mkude ana uwezo mkubwa wa kuharibu mipango ya wapinzani. Safu ya ulinzi ya Simba inaonekana kuwa imara msimu huu ikifungwa mabao 19 kutokana na ubora wa kiungo huyo ambaye amekuwa akiwafumba macho watu wengi kutoona makosa ya mabeki wa kati wa Simba. Ninafikiri ulikuwa wakati mwafaka kwa Nooij kumjumuisha Mkude katika kikosi cha Stars iliyopo Afrika Kusini.

7. HAMIS MAINGO - PRISONS
Kama ulikuwa hujui, huyu ndiye aliyesababisha Kiemba na Chanongo waungane na kiungo Shaban Kisiga kusimamishwa Simba alipofunga goli la ajabu katika mechi yao ya sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya Oktoba 25 mwaka jana.

Maingo ni winga wa kulia mwenye kasi na hakabiki kirahisi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga chenga na fedheha. Kuwa miongoni mwa wachezaji wa timu inayonusurika kushuka daraja karibu kila msimu, kunamnyima nafasi ya kuonekana na kujulikana kwa watu wengi, lakini ninaamini Maingo angelikuwamo katika kikosi cha Stars cha COSAFA mwaka huu kama ufuatiliaji wa kina wa utendaji wa wachezaji ungelifanywa na benchi la ufundi la timu hiyo ya taifa.

8. JOSEPH MAHUNDI - COASTAL UNION
Mara nyingi Coastal Union wamekuwa wakikmchezesha nafasi ya kiungo mkabaji, lakini anacheza vizuri anapokuwa kiungo mshambuliaji. Licha ya kuwa na umri mdogo, Mahundi ana nguvu, ana uwezo mkubwa wa kukimbia na kupiga chenga. Ninafikiri mchezaji bora huyo wa mwezi Desemba wa VPL alipaswa kuwamo katika kikosi cha Stars kilichopo Afrika Kusini kwa manufaa ya baadaye.

9. AMOUR OMARY JANJA - JKU
Kadri ya uelewa wangu wa soka, Janja ndiye mshambuliaji wa kati hatari zaidi anayecheza ndani ya mipaka ya Tanzania. Janja ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar msimu uliopita na ndiye aliyeharibu mipango ya Yanga katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu baada ya kufunga bao kali lililoipa JKU ushindi wa bao 1-0 na kuing'oa timu hiyo ya Jangwani katika hatua ya robo fainali.

Kutokana na uwezo wake mkubwa katika kupiga mashuti ya nje ya boksi, nguvu na mwili ulioshiba, ninafikiri Nooij na benchi la ufundi la Stars hawajatenda haki kutomjumuisha katika safari ya COSAFA mwaka huu.

10. RASHID MANDAWA - KAGERA SUGAR
Amefunga mabao 10 msimu huu wa VPL licha ya kukosa mechi kadhaa kutokana na malaria na kadi tatu njano. Alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Novemba na ana uwezo mkubwa wa kukimbia kwa kasi na kupiga mashuti. Ninafikiri kutokuwapo kwa Samata, kulitoa fursa kwa mkali huyo kuitwa Stars ya COSAFA.

11. JACOB MASAWE - NDANDA FC
Mawinga wa kushoto Deus Kaseke (Mbeya City), Salum Azizi Gila (Mgambo) na James Ambrose wa Police Moro wamefanya kazi nzuri msimu huu, lakini Masawe amefunika zaidi.
]
Kutoporomoka daraja kwa Ndanda FC kumechagizwa kwa kiasi kikubwa na mchezaji huyo wa zamani wa Toto Africans, African Lyon na Oljoro JKT.

Masawe, mchezaji bora wa VPL 2011/12 akiwa na Toto Africans, amefunga mabao matano msimu huu na yameipa Ndanda pointi 15 (kila alipofunga bao, Ndanda iliibuka na ushindi), hivyo ni wazi ukiondoa mabao hayo, Ndanda inakuwa miongoni mwa timu mbili ambazo zinarudi Ligi Daraja la Kwanza.

Winga huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji wa kati (Na. 8), ana uwezo mkubwa wa kukimbia na kupiga chenga na kufunga mabao. Kumbuka goli alilowafunga Yanga wakati Oljoro JKT ikilala 2-1 jijini Arusha Aprili 12 mwaka jana. Nidhamu ya hali ya juu aliyonayo iliyompa taji la mchezaji bora wa VPL misimu mitatu ni miongoni mwa sababu nyingine kuntu za kuitwa Stars kwa sasa.

*Imeandikwa na Sanula Athanas, mwandishi wa michezo mwandamizi wa NIPASHE. 

CHANZO: NIPASHE la Jumatatu Mei 18, 2015

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video