Kaseke akisaini jana Yanga
MABINGWA wa ligi kuu soka Tanzania bara, Young Africans jana
wamefanikiwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili, aliyekuwa kiungo mshambuliaji
wa Mbeya City fc, Deus Kaseke.
Kaseke ambaye kwa muda mrefu alikuwa anawindwa na Simba aliokuwa
anafanya nao mazungumzo ya mara kwa mara alipata umaarufu mkubwa akiichezea
Mbeya City msimu wa 2013/2014 na msimu wa 2014/2015 uliomalizika mei 9 mwaka
huu.
Baada ya kusajiliwa na Yanga jana, Kaseke alialikwa katika
kipindi cha michezo cha Sports Xtra kinachorushwa na Clouds fm kila siku saa
3:00 usiku.
Nyota huyo alizungumzia mambo mengi kuhusu maisha yake ya
soka ikiwemo vita ya Simba na Yanga katika harakati za kuwania saini yake. Hapa
chini ni baadhi ya mambo aliyoyasema Kaseke:
Swali: Watu wengi wanakujua Deus Kaseke ukicheza Mbeya City
iliyotikisha nchi msimu wake wa kwanza 2013/2014, lakini hawajui historia yako
ya soka, wafahamishe wadau wa michezo wakiwemo wapenzi wa Yanga njia ulizopitia
kisoka.
Deus Kaseke anasimulia: “Nilianza
kucheza mpira shule ya msingi na sikutarajia kama mpira utakuja kulipa. Kuna
shule moja inaitwa Kalobe Sekondari, nikiwa kidato cha pili ndipo nilianza
kucheza mpira shuleni na mtaani mtaani, nikaaminiwa
kwenye timu ya shule na kuchaguliwa kuwa waziri wa michezo 2008.
Baada ya kutoka hapo shule nikawa nacheza timu ya mtaani
kwangu Nzovye inaitwa African Boys, baadaye nikaja kucheza klabu ya Simike FC
na kusajiliwa na Airport Rangers. Nikiwa Airport kuna ‘Braza’ mmoja anaitwa
Venas Mligo akanifanyia mpango, nikaenda
kucheza Mbaspo Academy (Mbeya).
Nikiwa hapo nikaenda mpaka Arusha kucheza Rolling Stone,
nilivyorudi nikaona nitacheza mpaka lini mpira wa kituo?, nikaomba nitafute
timu ligi daraja la kwanza. Nakumbuka
nikaenda kucheza Polisi Iringa, lakini kabla ya kwenda huko nilifanya usaili
Prisons ambao waliniacha.
Nilipofika Polisi Iringa nilisajili bure kabisa, nikaona
mkataba na kusainii tu kwasababu nilikuwa natafuta nafasi ya kutoka. Kuna
kiongozi mmoja wa Polisi anaitwa Willy Chikweo, akaniamba mdogo wangu hapa umekuja kucheza,
unasaini tu, sisi hatuna hela. Kwasababu umekuja kucheza utatoka mwanangu. Nikamwambia
hakuna tatizo, nikafanikiwa kucheza pale
na nilikuwa nacheza namba sita kwa mechi zote saba, lakini hatukufanikiwa
kwenda kwenye kituo cha Morogoro . Nikarudi Mbeya sina hata mia, wazazi wangu
wakaniuliza sasa mpira unakusaidia nini mwanetu?
Unajua mimi nilikuwa nasoma chuo cha ualimu, sisi familia
yetu ni kubwa, mzee wangu alikuwa ananilipia
ada laki 5 au sita, nikamwambia mzee niache, wasomeshe wadogo zangu, mimi nitapambana.
Kitu kilichonifanya niache chuo ni Prisons. Waliniambia Deus
utacheza hapa, njoo ufanya usaili, nikamwambia mzee mimi pale (Prisons)
nitapata kazi, endelea kuwashughulikia wadogo zangu.
Baba akaniacha na
nikaenda Prisons, lakini sikusajiliwa na ndipo nikaenda Polisi
Iringa na kucheza kwa nusu msimu kwasababu nilienda raundi ya pili, lakini
hatukufanikiwa kufika 9 bora ambayo walienda Mbeya City na msimu huo waliopanda
ligi kuu walikuwa Prisons, Polisi Moro na Mgambo katika kituo cha Morogoro.
Baada ya kupanda ligi kuu, Prisons wakasema lazima nikacheze
pale, nikaenda kufanya usaili kwa mara ya pili, nilionekana kama napata nafasi,
lakini wakasema utacheza timu ndogo. Nikawaambia haiwezekani bora waniache, nakumbuka
kipindi kile Prisons waliwaacha wachezaji wengi walioipandisha timu.
Swali: Mchakato wa kujiunga Mbeya City fc ulikuwaje?
Deus Kaseke anaeleza: “Kipindi
Maka Mwalwisyi anakwenda kuwa kocha msaidizi pale Mbeya City, nikampigia simu
mwalimu Mwambusi (Juma) nikimuonba nifanye majaribio. Mwalimu (Mwambusi) yeye alijua mimi nacheza namba
sita, akaniambia Deus namba sita imejaa, nikamwambia mimi sichezi namba sita,
nataka kucheza namba za mbele, akaniambia basi poa. Ikabidi nianze kufanya
usaili, ilikuwa unafika uwanjani, unafanya ‘warm-up’ halafu mnaingia kucheza
timu mbili. Bahati nzuri mimi nikacheza vizuri na kuonesha naweza kucheza Mbeya City na kwenye usaili
huo nilikuwa nacheza namba 10, 7 na 11.
Baada ya kumaliza usaili, wakaniambia tutakupigia simu (Mbeya
City), kweli Mwambusi akanipigia simu
akiniambia Deus uje mazoezini kesho asubuhi, lakini sikujua kama nimechaguliwa
kucheza Mbeya City. Nikaenda mazoezini kesho yake, nikaenda tena kesho yake, akaniambia Deus utaingia kambini. Sikuamini
kama kweli nimechaguliwa kucheza Mbeya City ya daraja la kwanza. Sikuchukua
hela yoyote pia katika usajili, nilijua
natafuta nafasi. Sasa kipindi tunapandisha timu ligi kuu, mimi niliibuka mfungaji bora wa Mbeya
City nikifunga magoli manne.
Swali: Msimu wa kwanza wa Mbeya City (2013/2014), timu
ilicheza vizuri na kushika nafasi ya tatu, lakini msimu wa 2014/2015 uliomalizika
mei 9 mwaka huu, timu haikufanya vizuri licha ya kumaliza nafasi nne za juu,
mlikumbwa na nini?
Deus Kaseke anaanika: “Unajua
msimu wa kwanza tulipofanya vizuri, watu wakaanza kutufikiria kivingine. Kila
mtu anawaza kwamba akikutana na Mbeya City anakutana na timu bora, kwakifupi hatukuwa
na mpango B ‘Plan B’, tulicheza kwa staili ile ile ya msimu uliopita .
Upinzani ukawa
mkubwa, watu wakawa wanajiandaa kuliko sisi tulivyo, sisi hatukubadilisha
staili ya uchezaji, ilitupa wakati mgumu mechi saba za kwanza, tulipoteza mechi
nne mfululizo, ligi iliposimama tukashukuru kwasababu tuliona tunaweza kushuka
daraja.
Baada ya ligi kusimama tukajipanga vizuri, lakini wachezaji ambao
walikuwa tegemeo kwenye timu wengi wakaachwa, tukaanza wakati wa mpito tena. Sikuelewa
kwanini wameachwa, sababu walikuwa nazo viongozi. Wachezaji tukaanza kuwaza
kama wanaachwa wale ambao tulikuwa tunafanya nao kazi vizuri kama vile Saady
Kipanga, Antony Matogolo (walitolewa kwa mkopo ), Deogratius Julius (aliachwa),
tutafanyeji? Lakini tukajua viongozi wanatafuta
mchawi.
Tungekuwa pamoja na wale wenzetu tungefanya vizuri kwasababu
tulikuwa tunajuana. Tulituliza akili baada ya kurudi tuliamini kwamba hatuwezi kushuka daraja, hata
watu walikuwa wananiuliza ‘Deus mtashuka daraja?.” nikawa nawaambia sisi tutashika
nafasi nne za juu. Tulipofanikiwa nikawaambia mmeona?
Swali: Kwa muda mrefu ulikuwa unahusishwa kujiunga na Simba
ingawa nao Yanga walikuwemo kwenye mbio hizo. Ulifanya mazungumzo mara nyingi na Simba, lakini ghafla
umesajiliwa na Yanga, vita ya klabu hizi kongwe kuiwania saini yako ilikuwaje?
Deus Kaseke anasimulia:: “ Ujue
toka mwanzo waliokuwa wananifuatilia sana ni Simba. Nilikuwa nafanya nao
mazungumzo toka msimu wa kwanza, lakini hata Yanga walikuwa wananifuatilia, ila
Simba walikuwa ‘serious’ zaidi na nikajua
naenda kucheza Simba.
Baada ya kupoteza mechi nne za kwanza msimu uliokwisha na
ligi kusimama tulipofika raundi ya saba, Simba wakaniita huku Dar, tukafanya
mazungumzo ya awali, wao walikuwa wananihitaji kwa kipindi hiki ambacho
nimesaini Yanga. Wakaniambia nitasaini mkataba mwezi wa 12, halafu inapofika
mwezi wa sita mwaka huu nitamalizia ada yangu ya usajili.
Siku hiyo Yanga wakanitorosha usiku, nikaenda Hoteli moja,
waling’ang’ania nisaini kipindi kile kile, nikawaambia Yanga niacheni kwanza
nitakuja kusaini mwishoni mwa msimu. Malengo
yangu nilijua kufikia mwishoni mwa msimu mkataba wangu utakuwa umeisha, nilibishana
nao (Yanga) mpaka wakamtuma kiongozi mmoja ambaye nilienda naye Mbeya, lakini nilipofika
Mbeya nikaweka akilini mwangu kuwa kati ya timu hizi mbili (Simba na Yanga)
lazima nitasaini timu moja.
Baada ya kumaliza mkataba Mbeya City, Yanga wakawa Serious
kunitafuta, nikawa naongea na simu za Yanga tu. Simba wakanipigia simu wakiniambia
hebu tutumie namba ya Peter Mwalyanzi, nikawatumia. Wao walitaka mimi na Peter
twende Simba, kila nikipiga hesabu nikaona ngoja nitulie kwanza. Nakawaambia
ngoja nimalize ligi, hata waandishi wa habari nilikuwa nawaambia mwenye kisu
kikali ndiye atayekula nyama
Swali: Inaelezwa kwamba siku mbili kabla ya kusajiliwa Yanga,
kulikuwa na vita ya hali ya juu kati ya Yanga na Simba, hebu simulia
ilivyokuwa?
Deus Kaseke anafunguka: “Wakati natoka Mbeya nilijua naenda
kusaini Yanga kwasababu ndio walikuwa
serious kwa siku mbili, tatu, napanda ndege Airport Mbeya napigiwa simu na
viongozi wa Simba, Deus kumbe unakuja Dar? Unakuja kusaini Yanga? Nikawaambia naenda kufanya nao mazungumzo,
siendi kusaini.
Nafika Airport Dar kumbe kuna viongozi wa Yanga wamekaa
pale, wakati huo huo napigiwa simu na viongozi wa Simba wakiniuliza uko wapi?,
sisi tumeshafika Airport hapa?. Nikawaambia naenda kufanya mazungumzo tu na
Yanga, siendi kusaini.
Jana (juzi) nimepata
taabu sana usiku, kuna watu ambao mimi siwajui walitumwa na Simba waje
kunichukua hotelini na kunipeleka sehemu fulani tumalizane. Yanga wakashitukia,
ikabidi waje Hotelini. Mimi sikutaka
kutoka pale Hotelini kwasababu hawakunileta wao, nikawaambia Simba ninyi ofa
yenu mnasemaje? Mimi sijasaini Yanga.
Ilipofika saa sita usiku wakaja viongozi wa Yanga Hotelini,
wakanipigia simu, nikawaambia mimi nalala, tutaongea kesho asubuhi. Moja ya
viongozi wa Simba naye kanipigia simu akiniambia basi tutaongea kesho, lakini lazima
tukuchukua hapo tukupeleke sehemu fulani.
Kumbe viongozi wa Yanga wanajua hizo taarifa, wakaja
chumbani kuniambia ofa yao, wakaa kikao
na kuniambania Deus hapa inabidi tuhame. Tukakaa pale mpaka saa saba kasoro,
wakasema hawawezi kulala mpaka mimi na wao tuondoke. Nikahamishiwa Hoteli moja
pale Sinza inaitwa Golden Park, tulipofika pale bado simu za Simba zikawa
zinapigwa, nikawaambia tutaongea kesho, nimelala, simu zikaendelea kupigwa, ikabidi nizime simu ili niweze kulala.
Wakati nalala kumbe viongozi wa Yanga nao wamelala hotelini hapo,
wanaogopa kwamba nitatoka. Sasa mimi naamka jamaa mmoja ananiambia, bwana Deus mimi
nipo hapa toka usiku, nimelala chumba hiki kinachotazamana na chako,
nilishindwa kukwambia kwamba nimelala hapa, nilitaka jamaa (Simba) wasifanikiwe
kukutoa.
Lakini nilipokuwa nakuja Dar kusaini , watu wanaonisimamia
waliniambia mwalimu Pluijm (Hans van der wa Yanga) ndiye aliyenipendekeza mimi
kwamba “namhitaji Deus”. Nikawa najiuliza nitaendaje Simba wakati mwalimu ndio
huyo anaondoka? Nikienda Azam si ndio
hao wanahangaika kutafuta kocha?
Azam nao walinipigia simu lakini hawakuwa Serious.
Nilipofika hapa Dar si unajua watanzania tena, wakawa wanapandisha mzigo
washindana wao kwa wao. Ikabidi niwaambie Yanga tukifika hapa (dau) hata aje
nani sitasaini kokote. Wakafika dau nikasaini Young Africans miaka miwili.
Swali: Baada ya kusaini Yanga, nini matarajio yako?
Deus Kaseke: “Namuomba mwenyezi mungu aniepushe na majeraha ya uwanjani kwasababu ili ufanye kazi vizuri lazima uepukane na majeraha na mwenyezi Mungu ndiye anapanga kila kitu, nikiwa vizuri nitafanya kazi”.
0 comments:
Post a Comment