WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamefanikiwa kumsainisha mkataba
wa miaka miwili kiungo mshambuliaji, Peter Mwalyanzi kutokea Mbeya City fc.
Mwalyanzi alisaini mkataba huo jana na baada ya hapo alifanya
mahojiano maalumu na Sports Xtra ya Clouds fm na hapa chini ni baadhi ya mambo
aliyozungumza:
Swali: Kabla hujawa Peter Mwalyanzi wa leo, ulianza kucheza
mpira wapi?
Mwalyanzi anaeleza: “Nilianza
kucheza mpira nikiwa shule, nilikuwa napenda sana mpira. Nilipomaliza kidato
cha nne nikasajiliwa Kijiweni ya Mbeya, baadaye ikaja kuuzwa na kubadilishwa jina
kuwa TMK. Minziro (Fred) alikuja Mbeya, kuna baadhi ya wachezaji ikabidi
waondoke na ile timu, hawakutakiwa kuondoka watu wote, wakachagua watano na
mimi nikiwemo.
Tulicheza TMK, lakini hatukufanikiwa kupanda ligi kuu, wakapanda
Manyema , Africa Lyon na Majimaji, ambao tulikuwa tunacheza 9 bora pale uwanja
wa Uhuru .
Wale wachezaji watano Mtemvu (Abass), wote alikuwa
anatukalisha Gesti, kwahiyo ikawa gharama, kwake na ikabidi wachujwe, nikabaki
peke yangu TMK. Nilipoona ile timu haiangalii mbele zaidi, nikasajili Pan Africa wakati huo kocha akiwa
Juma Pondamali ‘Meansah’.
Kipindi ambacho tulikuwa
tunacheza tisa bora, tulikuwa na Mgambo JKT kabla ya kupanda ligi kuu. Waliniona
na kuniita Tanga, hatimaye nikasajili pale.
Swali: Baada ya kusajiliwa Mgambo, msimu wako wa kwanza wa
ligi kuu soka Tanzania bara ulikuwaje?
Mwalyanzi anaeleza: “Msimu
wangu wa kwanza haukuwa mzuri pale Mgambo, mechi nne za kwanza zilikuwa ngumu
kwangu, mwalimu alikuwa hanielewi kwasababu mpira wangu ulikuwa laini.
Alikuja kunipa nafasi kwenye mechi na Mtibwa Sugar,
nikamuonesha kwamba alivyokuwa ananifikiria sivyo, baada ya mechi hiyo, Mgambo
wakawa wananihitaji kuwepo uwanjani kila
mechi. Nilicheza misimu miwili Mgambo.
Swali: Baada ya kucheza misimu miwili Mgambo, zilitoka
taarifa za Yanga na Simba kukuwinda, ilikuwaje?
Mwalyanzi: “Nilipomaliza msimu
wa pili pale Mgambo, Yanga wakawa wananihitaji, nikaja mpaka huku Dar es
salaam, nikafanya nao mazungumzo, lakini viongozi wakagawanyika, baadhi walikuwa wananitaka mimi wengine wanamtaka Hassan Dilunga,
wakaonekana wa Dilunga wameshinda, Bin Kleb akaniambia wewe nenda tutakupigia
Simu.
Swali: Baada ya Yanga kuachana na wewe, ulikwenda wapi?
Mwalyanzi: “Nikaenda Mbeya na
kukaa huko. Prisons wakanipigia simu, tukakubaliana kila kitu, nikawaambia mimi
nimemaliza ligi sasa hivi, sio ninyi pekee mlioniona, kuna timu nyingine kama
Mtibwa, Coastal, zote zimenipigia simu.
Fanyeni haraka ili tumalize hii shughuli, wakasema sawa, lakini wao Mbeya sio
makao makuu, inabidi wapate pesa kutoka Dar es salaam.
Nikakaa siku mbili, viongozi wa Mbeya City wakanipigia Simu,
tukaongea nao na wakawa haraka, tukamalizana kila kitu, nikasaini mkataba
kuitumikia msimu uliokwisha mei 9 mwaka
huu.
Swali: Kabla ya kutakiwa na Simba, ulipata ofa ngapi hapa
katikati?
Mwalyanzi: Hapa katikati kabla ya kuja Simba
nimepata ofa mbili kutoka Mwadui na Yanga. Watu wa kwanza kuwasiliana na mimi
walikuwa Yanga. Ile mechi ya mwisho dhidi ya Polisi sikucheza kwasababu
nilikuwa na majeruhi, siku hiyo akanipigia simu kiongozi wa Yanga, Aron Nyanda
wakati timu yao inacheza mechi Mtwara, akaniambia kocha amesema anakutaka wewe
Peter Mwalyanzi ili uchukue nafasi ya Mrisho (Ngassa) kwasababu una kasi
inayofanana na yake.
Nikawa nawasiliana na Aron, lakini akawa hanielezi kwa
ufasaha, anaongea na mimi kama mdogo wake tu. Nikawa namsikiliza tu, kuna
siku nikamtumia meseji nikimuuliza ‘Broo’ mboni kimya? Siku ya pili yake
akanipigia simu, lakini sikuipokea kwasababu nilikuwa nje. Siku ya pili
viongozi wa Simba wakanipigia simu, nikawa naongea nao kwa makini na jamaa
alionekana yuko makini, akaniambia Simba tunakuhitaji si kwababu umetufunga
mechi ya Mbeya, tumekufuatilia kwa muda mrefu.
Swali: Vita ya Simba na Yanga ilikuwaje siku mbili kabla
ya kusaini Msimbazi?
Mwalyanzi: Jana (juzi) niliendea kuangalia
mpira pale Mwenge-Mbeya, kuna watu wakaniambia utapigiwa simu na kutumiwa
tiketi uende Dar. Mimi sikujua kitu na sikutaka kuuliza. Nikiwa pale
Mwenge-Mbeya akanipigia simu kiongozi mmoja akiniambia mpango huo, lakini awali
nilikuwa na mpango wa kuja Dar kwa ndege, kuna binamu yangu anafanya kazi
Fastjet, alikuwa amenikatia tiketi achana na ya Simba waliotaka kukata.
Nikamwambia kiongozi wa Simba nakuja Dar jumapili, lakini
sijui ni saa ngapi kwasababu hiyo tiketi natumiwa kwenye e-mail, akaona kama
namdanganya hivi. Akaniambia kwani hiyo tiketi vipi? Sisi tunakukatia nyingine,
nikawaambia sasa hiyo nyingine itakuwaje? Akaniambia usijali, akanitumia tiketi
nyingine, nikamwambia binamu aachane na kunitumia tiketi.
Yule kiongozi wa Simba akawa ananipigia simu mara kwa mara
akisema bwana nimesikia Yanga wanakutumia tiketi uje, nikamwambia mimi sijui.
Kila muda ananipigia bwana usirubunike, tunakuomba sana. Nikamwambia mimi
nikikwambia kitu nitafanya basi nitafanya, siwezi kurubunika kwasababu ya kitu fulani.
Juzi asubuhi saa 12 kanipigia simu mtu mmoja akiniuliza,
vipi uko wapi? Nikamwambia nipo home, akasema uko home wapi wakati uko Airpot
hapo (Mbeya)? Nikamwambia naenda Dar kuonana na Mtibwa sio huko unakosema wewe.
Kweli nikasafiri na kukutana na wale jamaa wa Simba. Jinsi walivyokaa huwezi
kujua kama wanamsubiria fulani, mmoja kakaa huku, mwingine kakaa kule. Kuna
broo nilikuwa namjua pale, nikaenda alipo, akanichukua tukaenda mpaka kwenye
gari, hatimaye tukaenda ofsini, tukakubaliana mahitaji ya msingi, tukaafikiana kwa
pande zote mbili na nikasaini mkataba wa miaka miwili nikiwa na ndugu yangu
anayejua sheria.
0 comments:
Post a Comment