Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga
'Hakuna hata uwanja mmoja wa soka unaomilikiwa na CCM unaokidhi kanuni za FIFA za viwanja vya mashindano ya kimataifa.'
VIWANJA vya soka ni mahali pa hisia (emotion) na mvuto (fascination) kwa watu wengi. Ni sehemu ambayo hutumiwa na maelfu ya watu bila kujali itikadi zao za siasa, kidini, kijamii na kijinsia, kuburudishwa na mechi za soka, mchezo unaopendwa na watu wengi duniani.
Mbali na kutoa fursa hiyo, viwanja vingi vimekuwa alama ya utambulisho (hata kama si rasmi) ya miji mbalimbali. Kwa kutambua umuhimu wa viwanja katika michezo, Sheria Namba Moja katika Sheria 17 za Soka za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ni Uwanja.
Katika miaka ya karibuni tumeshuhudia kukua kwa kiwango cha soka nchini kunakokwenda sanjari na ongezeko la wapenzi wa mchezo huo katika miji mbalimbali. Hata hivyo, ongezeko hilo linaonekana wazi kutokwenda sambamba na ujenzi wa viwanja vipya, upanuzi na uboreshaji wa viwanja vya soka vilivyopo.
Mbali na Uwanja wa Taifa, kwa takribani miaka thelathini hapajakuwa na maendeleo yoyote ya ujenzi wa viwanja vipya au ukarabati wa vilivyopo ili kukidhi matakwa ya ongezeko la wapenzi wa soka na maendeleo ya mchezo huo kwa ujumla.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita FIFA imeisaidia Tanzania kukarabati viwanja kadhaa, lakini jitihada hizo zimekuwa zikikwamishwa na serikali kwa kutoza kodi kubwa vifaa vya ujenzi na ukarabati wa viwanja hivyo. Ukarabati wa Uwanja wa Kaitaba unaoendelea mjini Bukoba umekumbwa na changamoto hiyo ya kodi.
Serikali ya Tanzania pia imekarabati Uwanja wa Uhuru ambao binafsi ninafikiri haukupaswa kupakana na Uwanja wa Taifa. Serikali ilipaswa kuujenga Uwanja wa Taifa kwenye eneo jingine tofuati na ulipo sasa.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha Mapato ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyotolewa Mei 2011, viwanja vingi vinavyotumika katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) vilijengwa miaka ya 1970 na 1980 na havina miundombinu inayokidhi masharti ya ulinzi, usalama na burudani.
Ukurasa wa 10 wa ripoti hiyo yenye jumla ya kurasa 95 na viambatanisho tisa unasema: "Viwanja vyetu vingi havitoi fursa kwa watazamaji kuingia uwanjani bila bughudha, kukaa kwa raha na starehe na urahisi wa kutoka uwanjani baada ya mechi."
"Pia havitoa fursa ya watazamaji kupata viburudisho kama vinywaji na vitafunwa, sehemu ya kuuzia kumbukumbu kama picha na machapisho mbalimbali ya michezo mfano ratiba za ligi na kalenda. Haviwakingi watazamaji dhidi ya jua kali au mvua na havina huduma nzuri ya vyoo kwa ajili ya wachezaji na watazamaji," inaongeza ripoti hiyo.
Uwanja wa CCM Sokoine Mbeya
Ripoti hiyo inaeleza zaidi kuwa viwanja vingi vya soka nchini havina huduma za maji, sehemu za kutupa taka, umeme na taa za kutosha, alama za kuwaelekeza watazamaji sehemu husika na kamera za kufuatilia matukio, vyumba vya huduma ya kwanza na sehemu za kutosha za kuegesha magari kwa watazamaji, wageni mashuhuri, viongozi na vyombo vya habari na ya huduma za dharura kama zimamoto na huduma za wagonjwa 'ambulance'.
Asilimia kubwa ya viwanja hivyo vinamilikiwa na chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM). Ukiuondoa Uwanja wa Taifa, Uwanja wa Azam na Uwanja wa Kaitaba, viwanja vingine vyote vilivyotumika kwa VPL msimu wa 2014/15 vinamilikiwa na CCM.
Uwanja wa Taifa ni mali ya serikali ya Tanzania na umejengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 56 kwa ushirikiano wa Tanzania na China. Tanzania ikichangia Sh. bilioni 25. Uwanja wa Kaitaba unamilikiwa na Halmashauri ya Bukoba wakati Azam Complex unamilikiwa na Azam FC.
Viwanja vyote vya CCM havikidhi matakwa ya kanuni za FIFA za viwanja (FIFA Stadium Technical Recommendations and Requirements) kwa kukosa vigezo vilivyoorodheshwa hapo juu, hivyo haviruhusiwi kutumika kwa michuano ya kimataifa.
Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga
Viwanja hivyo havina vyumba vyenye hadhi ya kuridhisha kubadilisha nguo wachezaji, waamuzi na waokota mipira. Havina vyumba vya wasimamizi wa mchezo, sehemu za wachezaji kupasha misuli (indoor warm-up area), vyumba vya habari, vyumba vya madaktari na sehemu za kuonyesha magoli.
Pia havina sehemu maalum ya kuketi watu wenye walemavu, sehemu maalum za wapigapicha na mahali pa kukaa waandishi wa habari. Hata Uwanja wa Taifa hauna eneo maalum kwa ajili ya kuketisha waandishi wa habari.
Katikati mwa msimu wa 2013/14 wa VPL, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilivifungia viwanja vyote vya soka vinavyomilikiwa na CCM pamoja na Uwanja wa Kaitaba, kutumika kwa mechi za ligi kuu na Ligi Daraja la Kwanza kutokana na dosari mbalimbali.
Mbali na mfumo wa tiketi za elektroniki (ETS) uliosimikwa na CRDB kwenye baadhi ya viwanja kisha kusitishwa kibabe siku nne kabla ya mechi ya mzunguko wa pili wa VPL msimu huu ya Simba dhidi ya Yanga, viwanja vya soka nchini havina vifaa vya ukaguzi, uthibiti wa tiketi na uingiaji viwanjani (ticketing and access control facilities).
Vyanzo vya uhakika vya maji ya kumwagilia nyasi na matumizi mengine ya viwanjani, vifaa vya umwagiliaji maji, mfumo wa kutolea maji yanayotuama (drainage system) na alama za viwanja pia ni tatizo.
Msimu huu Stand United inayotumia Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga kama uwanja wake wa nyumbani, ililazimika kucheza mechi moja ya VPL dhidi ya Kagera Sugar kwa siku mbili kutokana na uwanja huo kujaa maji.
Kwa kifupi, utunzaji na hali ya viwanja vya soka nchini si ya kuridhisha, hivyo ni vyema vyema wamiliki wa viwanja, hususan CCM ambao wana viwanja vingi zaidi, kuweka kipaumbele katika kukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vyao.
Katika hali ya kushangaza wamiliki wengi wa viwanja nchini wanajali zaidi ukusanyaji wa mapato kuliko utunzaji na uboreshaji wa viwanja vyao. Licha ya kupata mgawo mnono utokanao na mapato ya milangoni, CCM kwa kipindi kirefu hakijafanikiwa kuvifanya viwanja vyake kuwa vya kisasa na kukubalika kimataifa.
Lakini, ukurasa wa 12 wa ripoti ya kamati ya TFF unaeleza changamoto zinazowakabili wamiliki wa viwanja vya soka nchini wakiwamo CCM kuwa ni: "Mapato yatokanayo na matumizi ya viwanja vya mpira wa miguu yamekuwa yakitumika kwa shughuli za utawala na si uboreshaji wa miundombinu ya viwanja."
Kutokana na kuwapo kwa changamoto hiyo, ninafikiri ipo haja CCM na wamiliki wa viwanja vya soka nchini kuondokana na dhana ya kumiliki na kuendesha wao wenyewe mbadala yake wakaribishe wabia, wawekezaji katika kuendeleza, kuboresha miundombinu na uendeshaji wa viwanja hivyo kitaaluma na si kisiasa ilivyo sasa.
Pia ninawashuri CCM na wamiliki wengine wa viwanja vya soka nchini wafanye jitihada kuhakikisha wanaondokana na mawazo ya kijima ya kung'ang'ania mfumo wa kizamani wa matumizi ya tiketi za vishina kuingia viwanjani ili kudhibiti hujuma za mapato zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Ikumbukwe kuwa Juni 4, 2014 Bunge kupitia kamati yake ya kudumu ya Viwanda, Uchumi na Biashara lilitoa tamko la kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuilazimisha TFF kuachana mara moja na tikeki za vishina na kutumia tiketi za elektroniki.
Ikumbukwe pia kuwa mimi si mwanasiasa. Tukutane Jumatatu ijayo.
*Imeandikwa na Sanula Athanas ni mwandishi wa michezo mwandamizi wa NIPASHE na mshindi wa tuzo ya Mwandishi Bora wa Habari za Michezo na Utamaduni Tanzania 2014.
CHANZO: NIPASHE la Jumatatu Mei 18, 2015
0 comments:
Post a Comment