MLINZI na kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally
Mayay Tembele ametoa maoni yake kuntu kufuatia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa
Stars kufungashiwa virago katika michuano ya Cosafa inayoendelea Afrika kusini.
Stars ilifungwa goli 1-0 dhidi ya Swaziland katika mechi ya
kwanza ya kundi B na jana ikafungwa 2-0 na Madagascar , sasa inasubiri
kukamilisha ratiba kwa kucheza mechi ya tatu kesho dhidi ya Lesotho majira ya
saa 12:00 kwa saa za Tanzania.
Ukiziangalia timu za Kundi B kwa maana ya Tanzania,
Madagascar, Lesotho na Swaziland, Tanzania ndio nchi yenye kiwango cha juu
katika viwango vya CAF na FIFA, lakini imekula ‘manundu’ katika mechi zake
mbili.
Katika mahojiano maalumu na MPENJA BLOG, Ally Mayay ametoa maoni yake ambayo tunakuletea kama yalivyo:
“Makocha kupingwa kwasababu ya uteuzi wa wachezaji fulani sio
suala geni duniani. Watanzania sio watu wa kwanza kumlalamikia kocha kuwa, kuna wachezaji fulani hawafai, makocha wengi
hukutana na kadhia hiyo.
Kama unakumbuka mwaka 2002, kocha Luiz Felipe Scolari
alipingwa mpaka na rais wa Brazil kwa kumuacha Romario da Souza, lakini
alikwenda na kushinda kombe la dunia kule Korea kusini na Japan. Siku zote
unapopingwa unatakiwa kupata matokeo, kama matokeo hayapatikani, hapo unawajibika
kwa asilimia 100.
Kuanzia uchaguzi wa wachezaji wa Taifa Stars kumekuwa na
maneno mengi, wadau wa soka wanapingana na uteuzi wa mwalimu Mart Nooij. Kilichotakiwa
kwake ni kupata matokeo, sasa kwa bahati mbaya matokeo hajapata, dunia nzima
inaelewa kwamba mwalimu atawajibika.
Mbaya zaidi ni kwamba
Nooij hana ushirikikiano na makocha wenzake kujua nini kinachoendelea, unajua wazi
wachezaji wanalelewa na vilabu, akiwa mwalimu wa timu ya taifa anatakiwa kuwa
na mawasiliano ya kila siku kujua hali za wachezaji, yeye anakaa na wachezaji siku
tano, sita au saba, lakini wachezaji kwa mwaka mzima wanalelewa na makocha wa
vilabu zao.
Ndio maana Ulaya
utakuta kocha Arsene Wenger anamwambia kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy
Hodgson kwamba usimpange Theo Walcott kwasababu jana tu ndio ameanza mazoezi
mepesi kwasababu alikuwa na majeruhi ya miezi miwili.
Kwahiyo kocha wa timu ya taifa anafahamu hali ya Walcott iko vipi. Lakini
ukija kwetu makocha wengi Wazungu hawana ushirikiano wa moja kwa moja na
makocha wa vilabu hasa wazawa ambao wana wajibu mkubwa wa kujua wachezaji.
Kwa bahati mbaya Mart Nooij hana uhusiano mzuri na vyombo
vya habari, lakini kwenye ile semina ya Wakufunzi wa soka iliyofanyika wiki
mbili zilizopita pale TFF, Nooij alikuwa moja kati ya watoa maada.
Aliambiwa na mkurugenzi wa ufundi wa TFF, Mwalimu Salum
Madadi kwamba waliopo mbele yako ni ‘Senior Coaches’. Ni makocha wa Kitanzania
ambao wamefanya kazi katika vilabu mbalimbali na wengine timu ya taifa kwa muda
mrefu, alichojibu hakuonesha kabisa kama anataka hata kubadilishana mawazo na
makocha wazawa, alisema yeye alikuja na begi lake, ataondoka na begi lake, hii
inaashiria kile kinachotokea sasa hivi.
Anaweza kuchagua mchezaji, halafu siku mbili akapanda ndege
kurudi nyumbani kwasababu ya majeruhi (Juma Said Makapu), hii ni kwasababu hana
mahusiano ya moja kwa moja na makocha wa vilabu, unamchagua Haruna Chanongo
kumbe alishaumia siku mbili zilizopita, pia akina Nadir Haroub, Aishi Manula, Hassan
Isihaka wote walikuwa na majeruhi lakini aliwachagua. Hii ni kasoro kubwa,
miongoni mwa vitu ambavyo makocha wanatakiwa kuwa navyo na ni sifa kubwa ya
kuwa kocha bora ni kujifunza kila kitu.
Kama kocha hutaki kujifunza basi unapoteza sifa ya kuwa kocha
bora. Bahati mbaya sana Mart Nooij
anakutana na kadhia hiyo kutokana na kile anachosimamia. Huwezi kusema
tunakwenda Sauzi Afrika kama mazoezi ya kucheza mechi za kufuzu kwa CHAN na
AFCON, hata kama tunakwenda kujifunza ndio tuporomoke?.
Tunatakiwa kujifunza huku tukilinda heshima yetu, tunakwenda
kushiriki kwenye michuano huku tukionekana sisi ndio wenye nafasi kubwa katika
timu za kundi B, yaani kwenye kundi letu sisi ndio wenye kiwango bora zaidi,
Swaziland waliotufunga wako nafasi ya 46, sisi tuko nafasi ya 30 kati ya
mataifa 54 ya CAF, hawa Madagascar wako
nafasi ya 43.
Hata kama tumepoteza, tumepotezaje? Timu inaonekana haina
mpangilio kuanzia inavyocheza, mpango wa mechi ya kwanza ndio huo huo mechi ya
pili, tunafungwa magoli ya aina moja ya kushitukiza.
Hii ni kengele kwa
wanaosimamia mpira, wanatakiwa kuuliza wataalamu wa mpira, wasikae wakajifungia
vyumbani kwamba wao tu ndio wanajua mpira, sio wao tu wanaojua mpira, tuna
makocha wakubwa wazawa waliofundisha mpira kwa zaidi ya miaka 30, wanatakiwa
kuwauliza maoni yao na wayajumuishe katika shughuli za kuendeleza soka”,
Huo ndio mtazamamo wa Ally Mayay….unayo nafasi ya kutoa
maoni yako pia….
0 comments:
Post a Comment