Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Yanga itarudiana na ESS kati ya Mei 1-3 mwaka huu nchini Tunisia baada ya kutoka sare ya 1-1 jijini hapa Jumamosi.'
UONGOZI wa Yanga SC umedai umeanza kuvurugwa kisaikolojia na wapinzani wao katika michuano ya kimataifa, Etoile Sportive du Sahel (ESS) ya Ligi Kuu ya Tunisia.
Yanga SC, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, watarudiana dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Klabu Bingwa Afrika katika mechi ya pili ya hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho nchini Tunisia baada ya kutoka sare ya 1-1 jijini hapa Jumamosi.
Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, ameuambia mtandao huu jijini hapa leo kuwa, wapinzani wao wameanza mchezo mchafu wenye nia ya kuwavuruga kifikra kutokana na kutoiweka wazi tarehe rasmi ya mechi ya pili.
"Walipocheza na sisi (Yanga SC) Jumamosi, walisema mechi itachezwa Mei Mosi, lakini jana wakatuandikia barua wakitutaarifu kwamba mechi ni Mei 3. Leo wametuandikia barua nyingine, tena kwa lugha ya Kifaransa wakitutaarifu kwamba mechi iko Mei Mosi.
"Tunajua hizo ni sehemu ya figisufigisu (fitina) zao. Tutawafuata katika muda tunaoujua wenyewe na kuwapiga huko huko," ametamba Muro.
0 comments:
Post a Comment