AMISSI Tambwe ameendelea kuonesha thamani yake na
kuwadhihirishia Simba kuwa yeye ni mfungaji hatari baada ya jana kupiga magoli
matatu ‘hat-trick’ katika ushindi wa magoli 4-1 dhidi ya Polisi Moro.
Yanga walichukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara msimu wa
2014/2015 baada ya ushindi wa jana wakifikisha pointi 55 ambazo haziwezi
kufikiwa na timu yoyote.
Mwaka jana Simba walimuacha Tambwe katika mazingira ya utata
akiwa ndiye mfungaji bora na dakika za mwisho za dirisha dogo la usajili desemba
mwaka jana Yanga wakamsajili kwa kumpa mkataba wa mwaka mmoja.
Katika mechi tatu zilizopita, Tambwe amefunga magoli nane na
kufikisha magoli 14 katika msimu huu mgumu wa ligi kuu.
Alifunga manne katika ushindi wa 8-0 dhidi ya Coastal,
akatia kambani moja kwenye ushindi wa 3-2 dhidi ya Stand United na jana akapiga
tatu dhidi ya Polisi Moro.
Baada ya kufanikiwa kwa muda mfupi ndani ya Yanga, Tambwe
amesema anafurahia maisha ndani ya Yanga na ataendelea kufanya vizuri.
“Nashukuru nimefunga ‘Hat-trick’ yangu ya pili msimu huu,
nikiwa Simba nilifunga ‘hat-trick’ mbili pia, kwangu haya ni mafanikio,
nilipochukua kiatu cha dhahabu mwaka jana nilisikitika kuachwa na Simba, kichwa
changu hakikuwa sawa”, Amesema Tambwe na kusisitiza: “Leo hii (jana) nachukua
ubingwa Yanga nikifunga magoli muhimu, namshukuru Mungu, wachezaji wenzangu,
mashabiki na viongozi, wanaonesha upendo mkubwa kwangu”.
0 comments:
Post a Comment