Mbeya City Fc imefanikiwa kuvuna pointi zingine tatu muhimu baada ya ‘kuidabisha’ Kagera Sugar kutoka Bukoba Mkoani Kagera bao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara uliopigwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Katika mchezo huo ulioanza kwa taratibu huku kila timu ikijaribu kusoma mbinu za mwenzake, City ilikuwa ya kwanza kulifikia lango la Kagera Sugar mnamo dakika ya 5 ambapo mpira ulioanzia katikati ya uwanja kwa Kenny Ally ulimfikia Rafael Alfa aliyetoa pasi nzuri kwa Fredy Cosmas lakini shuti la mshambuliaji huyo lilishindwa kulenga lango na mpira kutoka nje.
Dakika 10 baadae Kagera Sugar walijibu mashambulizi langoni mwa City lakini uimara wa golikipa Hannington Kalyesubula ulimnyima mshambuliaji Mandawa wa Kagera Sugar nafasi nzuri ya kufunga bao kwa timu yake.
Timu ziliendelea kushambuliana kwa zamu na wakati mchezo ukielekea mapumziko Fredy Cosmas alifanikiwa kuiwahi pasi ya Deus Kaseke akiwa ndani ya eneo la penalti lakini wakati akijiandaa kufunga bao alifanyiwa madhambi na mlinda mlango Kagera Sugar na mwamuzi kuamuru kupigwa mkwaju wa penalti.
Kiungo ‘fundi’ Rafael Alfa alifanikiwa kukwamisha wavuni mkwaju huo wa penalti na kuinadikia City bao la kuongoza kabla mwamuzi hajapuliza kipyenga kuashiria kumalizika kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza ambapo City ilikwenda kwenye vyumba vya kupumzikia ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Juma Mwabusi katika kipindi cha pili kwa kumtoa Fredy Cosmas, Mwegane Yeya na John Kabanda na nafasi zao kuchukuliwa na Peter Mapunda,Peter Mwalyanzi na Hamad Kibopile yaliiongeza nguvu City na hatimaye kufanikiwa kupachika bao la pili kupitia Deus Kaseke aliyeunganisha vyema mpira uliopigwa na Peter Mwalyanzi kutoka wingi ya kushoto.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha usingizini Kagera Sugar na kuanza kucheza mpira kwa kasi lakini juhudi zao ziliishia kwenye mikono ya golikipa Hanington Kalyesubula au mipira yao kuokolewa na safu ya ulinzi ya City iliyokuwa chini ya nahodha Juma Nyosso ‘Coulibaly’.
Akiwa kwenye ‘ubora wake’ kiungo mshambuliaji Peter Mwalyanzi alindelea kuinyanyasa ngome ya Kagera Sugar ambapo dakika ya 85 nusura aipatie City bao la 3 baada ya kufanikiwa kuuwahi mpira aliotanguliziwa na Paul Nonga na kufanikiwa kumlamba chenga Salum Kanoni lakini shuti lake lilipaa juu kidogo ya lango la Kagera Sugar hivyo hadi dakika 90 zinakamilika City ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 2-0.
Mara baada ya mchezo kocha Mwambusi aliwashukuru vijana wake kwa ‘kupambana’ na kufanikiwa kupata pointi tatu muhimu huku kuwaomba kujiweka tayari kwa mchezo unaofuata dhidi ya Tanzania Prison utakaochezwa jumamosi ijayo kwenye uwanja wa Sokoine.
“Tumecheza vizuri, nawashukuru kwa kupambana na hatimaye tumepata matokeo, hili ni jambo jema kwa sabbu tayari tumesogea nafasi nyingine kwenye msimamo wa ligi,naomba tujiweke tayari kwa mchezo ujao ambao pia ni muhimu zaidi, tunarudi kufanyia kazi mapungufu tuliyoyaona leo kwa sababu tumetengeneza nafasi nyingi lakini tumetumia chache,naamini kama tungekuwa makini tungeshinda goli nyingi zaidi” alisema Mwambusi.
0 comments:
Post a Comment