Rais Malinzi
RAIS wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi aprili 27 mwaka huu amefungua kozi ya
walimu wakufunzi wa mpira wa miguu nchini inayofanyika katika uwanja wa Karume
jijini Dar es salaam ikitarajiwa kumalizika mei 2 mwaka huu.
Malinzi alisema
kozi hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa soka la Tanzania, walimu wakufunzi
watasaidia kuwafundisha walimu wengine wa mpira, ili kuweza kufundisha mpira
kwa watoto wadogo ambao ndio hazina ya baadae.
Malengo ya TFF
ni kuhakikisha timu ya vijana ya U17 inafuzu kwa fainali za Mataifa Afrika 2017
nchini Madagscar, na baadaye kuwa na kikosi bora wakati tunapotarajia kuwa
wenyeji wa fainali za U17 Afrika mwaka 2019.
Ili kufanikisha malengo
hayo, TFF imeeleza program mbili za
kuwaandaa vijana wenye umri chini ya miaka 13, 15 kwa kuwaweka kambini na
kucheza michezo ya kirafiki mikoani na kufanya ziara katika nchi za Malawi,
Zambia, Zimbabwe, Bostwana na Afrika Kusini. Pia ina malengo ya kuanzisha
mashindano ya vijana chini ya miaka 13 yatakayofanyika Alliance Mwanza kwa
lengo la kuibua vipaji.
Ukipima malengo ya TFF
ni mazuri wala hayana shaka, lakini kufanikiwa ni ndoto kwasababu kuna mambo ya
msingi ambayo hayajafanyiwa kazi.
Mtandao huu unatambua
juhudi za Rais Malinzi, lakini unakataa mpango wake wa soka la vijana na
kumshauri mambo saba ambayo anatakiwa kuyafanyia kazi kabla ya kuanzisha
mashindano;
Iwekwe wazi kuwa huwezi kuanzisha
mashindano ya vijana chini ya miaka 13 kwa lengo la kutengeneza timu moja au
mbili ili vijana waandaliwe kucheza mashindnao ya Afrika. Hili sio suluhisho la
maendeleo ya mpira wa nchi.
Mosi;
Malinzi atengeneze falsafa ya mpira wa nchi ya Tanzania, ikishapatikana falsafa
itakuwa ni rahisi kwa kijana aliyetoka Zanzibar, Pemba, Manyara, Lindi
kufundishwa mpira wa aina moja kwasababu tayari kuna falsafa ya nchi ambayo pia itaingia moja
kwa moja kwenye timu za ligi kuu. Kwa mfano ukiangalia ligi ya Ujerumani,
Bundesliga, ukiangailia ligi ya Hispania, La Liga au Uholanzi, inavyocheza timu
ya taifa ukienda kwenye klabu utaona wanacheza vilevile, mathalani,
wanavyocheza Barcelona, Real Madrid, Valencia utaona wanacheza hivyo hivyo
kwenye timu ya Taifa ya Hispania.
Ukienda
Ujerumani ‘Staili’ ya uchezaji wa klabu inaendana na timu ya taifa. Hii ndio
maana ya falsafa, kama taifa mnaamua kwamba hii ndio staili yetu ya uchezaji,
kufundisha wachezaji na hapo ndipo unapata urahisi wa kufundisha mpira. Kabla
ya kukimbilia kwenye mashindano kwanza ni kukaa chini na wataalamu ili
kutengeneza falsafa ya mpira wa Tanzania.
Pili;
Malinzi atengeneza mfumo sahihi wa kutambua na kuendeleza vipaji katika ngazi
zote ikiwemo umri chini ya miaka 13. Yeye anasema yatafanyika mashindano pale
Alliance Mwanza, lakini haiwezekani watu wakaja kucheza tu, lazima uwepo mfumo
thabiti wa kung’amua vipaji kote nchini kupitia vyama vya wilaya na vyama vya
mikoa. Kuwepo mfumo unaofanana wa kutambua vipaji kila kona ya nchi na
kuviendeleza.
Mashindano
ya vijana yatafanyika, lakini kama hakuna mfumo mzuri wa kimashindano wa
kubaini vipaji na mfumo wa kuviendeleza vipaji hivyo, lengo halitafanikiwa. Wachezaji
ambao wamekamilika kiushindani hawatapatikana. Itengenezwe falsafa baada ya hapo
utengenezwe mfumo wa kuviendeleza vipaji na itakuwa rahisi kupata timu bora.
Tatu;
Uandaliwe mfumo mzuri wa kupata viongozi madhubuti, viongozi wenye uwezo. Haiwezekani
Malinzi akawa na malengo yake peke yake kwamba tunataka kucheza fainali za
Afrika chini ya umri wa miaka 17 wakati kwenye vyama vya mikoa au wilaya kuna
watu hawaelewi wala kuona kile unachowaza yeye.
Ni
lazima kutengeneza mfumo mzuri wa kitaifa wa kuwa na watu sahihi kuanzia ngazi
zote, viongozi ambao wana uwezo wa kutekeleza mawazo yake kama kiongozi wa juu.
Sawasawa na wewe ni mmiliki wa kampuni, una malengo ya kufikia malengo fulani
kumbe wafanyakazi wako wote ni ‘vimeo’. Unafikiaje malengo wakati huna
wafanyakazi wenye mawazo na matazamo kama wakwako?. Tuna tatizo la kiuongozi
katika ngazi ya vyama na kwenye klabu pia. Lakini kama nilivyosema mwanzo ukiwa
na falsafa itakuongoza kujua ni aina gani ya viongozi na wachezaji uwe nao.
Kitu cha
nne; kabla ya mashindano kufanyika,
Malinzi atengeneze mfumo wa kimashindano wa kitaifa kwa ngazi zote za kitaifa.
Mfumo ule ule wa mashindano ya watoto ufanane kote nchini, ukienda Mbeya,
Mwanza, Lindi, Pemba uone mfumo mmoja wa mashindano ili ukipata wachezaji
wafanane kiuchezaji.
Tano, Malinzi
afundishe na kuzalisha makocha wa
kutosha, angalau kuwepo uwiano wa kocha mmoja kufundisha vijana 30, hapa
inategemeana na bajeti yake, mfano kama anataka awe na vijana elfu 10
wanaocheza mpira, inatakiwa awe na makocha wengi, huwezi kuwa na idadi hiyo ya
vijana halafu ukawa na makocha watatu, lazima ujiulize kuna makocha wangapi
nchi hii waliojikita kwenye ufundishaji wa soka la vijana? Itakuwa ni ndoto za
mchana kutaka kutengeneza mashindano wakati miondombinu ya kupata makocha hakuna.
Ukizalisha
makocha wengi watakuwa na nafasi ya
kufundisha vijana wengi unaotaka kuwaandaa. Uanzishwe mpango madhubuti wa
kuzalisha makocha wengi. Uwiano wa sasa unakuta kuna vijana elfu tatu halafu
kocha mmoja, inawezekana kocha mmoja kufundisha vijana elfu tatu? Haiwezekani!.
Kama nilivyogusia hapo juu , kama unataka kuwa na idadi kubwa ya vijana pia
unatakiwa kuwa na wataalamu wengi wa kung’amua vipaji na kuviendeleza,
usipokuwa na wataalamu utaishia kutengeneza kundi la wachezaji wa zamani na
kuwagawa kwa maeneo wakati utaalamu wenyewe wa kubaini wachezaji hawana.
Sita;
Malinzi aboreshe miondombinu ya mpira na utawala kwenye ngazi zote.
Nilizingumzia kidogo mwanzoni kuhusu viongozi, nasisitiza tena, uboreshe
miondombinu ya kiuongozi kwenye ngazi ya taifa, mikoa na wilaya. Lazima kuwepo na
mabadiliko chanya ya kuendana na usasa ili uwepo uhalisia wa kufikia malengo
tuliyojiwekea ya kucheza michuano ya Afrika. Hata kama tutakuwa wenyeji lazima
tushindane, lazima tutafute wataalamu na kuacha kukwepa njia sahihi.
Jambo la
saba ni kufanya utafiti na kubaini mbinu sahihi za kufundishia, kuna mabadiliko
makubwa sana ya kiufundishaji, kabla ya kuanzisha mashindano ya kupata vijana,
lazima tukae chini kufanya utafiti mzuri kupata njia sahihi za kufundishia
mpira. Lazima utengenezwe mfumo mzuri wa kisayansi wa kuweza kufundisha soka.
Pia miundombinu bora ya kitabibu kwa ajili ya kuwapatia wachezaji tiba nzuri,
waweze kupewa ushauri mzuri vya vyakula, sio kukimbia tu na kucheza mpira.
Hitimisho
ni kwamba; kabla ya mashindano hayo kuanza, Jamal Malinzi anatakiwa kuyapa
kipaumbele mambo haya saba ili kutimiza malengo ya kuona Tanzania inacheza
fainali za vijana za Afrika na kombe la Mataifa ya Afrika kwa timu ya wakubwa (Taifa
Stars), bila kufanya hivyo ni kutwanga maji kwenye kinu.
Nawakakia
jumatano njema, tukutena tena ijumaa panapo majaaliwa!! Ni halali yako kutoa
maoni au mtazamo wako!
0 comments:
Post a Comment