Stand United hali ni tete
WASWAHILI
‘wanasema mbio za sakafuni huishia ukingoni’, hakuna jambo lenye mwanzo
likakosa mwisho wake, hatimaye ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015
inaelekea saa za magharibi.
Timu
chache zimebakiwa na michezo mitatu, lakini nyingi zimesaliwa na karata mbili
tu kujua hatima ya kubaki au kwenda na maji.
Ligi ya
msimu huu inasemekana kuwa na changamoto kubwa ya kiushindani, watu wengi wanaangalia
namna timu zinavyofungana pointi, kama kigezo ni hicho tu, basi kweli ushindani umeongezeka.
Tanzania
Prisons wanashika mkia kwa kujikusanyia pointi 25 kufuatia kucheza mechi 24,
lakini wanatofautiana pointi 6 tu na timu zinazoshika nafasi ya nne (Mbeya
City) na tano (Kagera Sugar) zenye pointi 31 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Kwa mazingira
hayo, Prisons wanaweza kubaki ligi kuu kama watafanya vizuri kwenye mechi mbili
zilizosalia ikiwemo ile ya mahasimu wa jiji la Mbeya dhidi ya Mbeya City fc.
Si jambo
la kawaida kuwa na timu 10 kwenye msimamo zisizokuwa na uhakika wa kubaki ligi
kuu, ni ligi ya aina yake na kila timu roho inadunda. Hakuna tena faida ya kucheza nyumbani, timu
zinapambana kusaka pointi tatu, mfano jana Mtibwa Sugar walikufa kwao goli 1-0
dhidi ya JKT Ruvu.
Licha ya
ushindani huo, Yanga wanaweza kumaliza kazi leo kama wataifunga Polisi Morogoro
uwanja wa Taifa Dar es salaam kwasababu wanahitaji pointi tatu tu kufikisha 55
ambazo haziwezi kufikiwa na mabingwa watetezi Azam fc hata kama watashinda
mechi zao zote tatu zilizobakia.
Yanga
wana pointi 52 baada ya kucheza mechi 23 wakifuatiwa na Azam fc wenye pointi 45
baada ya kucheza mechi 23, kama Azam watashinda mechi tatu zilizosalia watafikisha
pointi 54 ambazo Yanga watakuwa wamevuka kama wataibuka kifua mbele jioni ya leo.
Kwa asilimia
kubwa, Simba wanaoshika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 41 baada ya
kucheza mechi 24 watamaliza ligi katika nafasi hiyo kama watashinda mechi zao
mbili zilizosalia, ni ngumu sana Azam fc kuzidiwa na Mnyama ingawa lolote
linaweza kutokea.
Tuweke
kando hayo na sasa tuangalia kile nilichokusudia kusema leo hii kutokana na utafiti
uliofanywa na mtandao huu kuhusu timu za mikoani kufanya vibaya ukitumia klabu
mbili za Stand United na Ndanda fc.
Hizi ni
timu mbili za wananchi kama ilivyo kwa Simba na Yanga, zinagusa maisha ya watu
wa kawaida mno ukilinganisha na timu za majeshi kama vile JKT Ruvu, Ruvu
Shooting pamoja na timu za makampuni kama vile Azam fc, Mtibwa Sugar na Kagera
Sugar.
Ndanda
na Stand United hazina matokeo mazuri msimu huu ambao ni wakwanza kwao, zipo katika
mstari mwekundu. Mpaka sasa, Stand wamebakiwa na michezo miwili kumaliza msimu
wakiwa na pointi 28 katika nafasi ya 10, wakati Ndanda nao wamebakiwa na
michezo miwili wakiwa tayari wamekusanya pointi 25 katika nafasi ya 12.

Ndanda fc ina kibarua kizito kubaki ligi kuu
Kwa
mfano tuichambue Ndanda fc; klabu hii imeshinda mechi tatu (3) nyumbani na tatu
(3) ugenini, imepoteza mechi 8 ugenini na tatu nyumbani. Imetoa sare sita (6)
nyumbani na moja ugenini.
Ukiyatazama
matokeo haya unaona haijafanya vizuri uwanja wa nyumbani wa Nangwanda Sijaona,
sehemu ambayo wangetengeneza matokeo mazuri.
Swali
linakuja, kwanini timu nyingi za mikoani za wananchi zinafanya vibaya ligi kuu?
Majibu
yanaweza kuwa mengi, lakini utafiti uliofanywa na mtandao huu umebainisha kuwa
sababu iliyobeba uzito wa juu ni
kukosekana kwa uzalendo, kumbuka utafiti huu haujafungwa, mtu yeyote anaweza
kutoa sababu zake.
Ndanda fc
ina wachezaji watatu tu wanaotoka Mikoa ya kusini ambao ni Omari Nyenye kutoka
Mtwara, Salum Mineli kutoka Newala na Majidi Lubanda kutoka Lindi. Kwa maana
hiyo wanaotoka Mtwara ni wawili tu na hiyo ni timu ya wananchi wa Mtwara.
Lakini
ukiangalia wakati ule timu ya Bandari Mtwara iliundwa na wachezaji wengi wazawa
wa mkoa huo wakiwemo Mohamed Hussein ‘Chinga’, Hassan Ahmed, Shomari Seleman,
Andrew Nyambi, David Anawake, Amlima, Said Mnunduma, Liziga, Yusuf Jeta, Jerome
Gabriel, Jacob Peter, Ziada Ambunda.
Hii
ilikuwa na faida kubwa moja, walicheza kwa uzalendo, waliitetea timu yao,
walijitolea kwa nguvu zote, walikuwa na utashi wa kujua wananchi wanataka nini,
waliweka maslahi pembeni, walitetea nembo ya timu yao tofauti na ilivyo kwa
Ndanda iliyojaza wachezaji wengi kutoka nje ya mkoa.
Ukiitazama
timu ya Stand United, ‘Chama la Wana’, ina wachezaji wachache wazawa kama vile David
Mwita, Pastory Athanas, , Richard Elisha, Ganga John, Jisend Mathias. Walio
wengi wanatoka nje ya Shinyanga, hebu angalia walichofanya Shabani Kondo, Hamis
Thabeet na Patrick Mrope, wachezaji hawa
waliikimbia timu kwa kukosa uzalendo na hii ni kwasababu ya kutokuwa wazawa.
Ukirudisha
kumbukumbu nyuma, timu ya wakati ule, RTC Shinyanga ilikuwa na wachezaji wengi
wazawa , mfano, Abadallah Magubika, Paul John Masanja, Deus Pamba, Willy John,
Charles Masule, Mwinyimvua Komba, Musa Salum, Nchambi Juma, Joseph Lubisha.
Siku
hizi hakuna tena ‘programu’ ya kuzalisha wachezaji wazawa kwa timu za mikoani
na hili ndio chimbuko la timu hizi kufanya vibaya, wachezaji wanaosajiliwa
kutoka nje ya mikoa hiyo wanakosa uzalendo.
Kwa
utaratibu ulivyo duniani, asilimia kubwa
ya wachezaji wanaounda timu za miji wanatakiwa kuwa wazawa ili wapambane na
kupata matokeo, lakini kwa timu za Ndanda na Stand hazina wazawa, wachezaji
wengi ni wageni, wanakuja kutafuta
maslahi.
Inapotokea
timu hazijawalipa mishahara mwezi mmoja au miwili, wachezaji wanakosa uzalendo,
hawachezi vizuri kwasababu hakuna wanachopoteza kama timu itashuka wataondoka
zao na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.
Wakati
utafiti huu unafanyika, ilielezwa kuwa timu ya Kariakoo ya Lindi, wakati
inacheza ligi kuu, kocha wake Salum Madadi alikuwa na uwezo wa kupanga
wachezaji wote wa Lindi.
Na mara
zote kwenye mechi za nyumbani, Madadi
alikuwa anapanga wachezaji wengi wazawa, mashabiki wakienda uwanjani wanawaona
wana wao, washikaji zao na hii
iliwafanya wachezaji wajitolee, maslahi hayakupewa kipaumbele, walipambana kwa ajili ya timu yao ya nyumbani tofauti na
siku hizi, hakuna morali ya hivyo.
Unapokuwa
na wachezaji wengi waliokuja kuvuna pesa kupitia mpira lazima uwalipe ili
wacheze vizuri, lakini ukikwama kidogo kifedha watacheza vibaya. Timu nyingi za
wananchi hazina uwezo wa kifedha, kuna wakati zinakwama kulipa posho, mishahara
kwasababu wakati fulani zinategemea misaada ya wananchi wenyewe ingawa siku
hizi kuna wadhamini tofauti tofauti.
Kinachotakiwa
kufanyika ili kurudisha hadhi ya timu za mikoani ni kuwa na mpango maalumu wa
kuzalisha wachezaji wazawa, sio vibaya kusajili kutoka nje ya mkoa, lakini
angalau asilimia 60-70 wawe wazawa ambao watamwaga mpaka tone la mwisho
kupigania timu zao.
Nawatakia
jumatatu njema! Tukutane tena jumatano panapo majaaliwa!
0 comments:
Post a Comment