Kikosi cha Yanga SC kimeshaingia jijini Tanga kusaka rekodi ya kuifunga Mgambo Shooting iliyoshindikana kupoteza mechi kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya klabu kongwe nchini, Simba na Yanga.
Timu hiyo inayonolewa na kocha mkuu, Bakar Shime, juzi iliifundisha soka na kuichapa Simba SC iliyokuwa pungufu kwa mchezaji mmoja tangu dakika ya 68 mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa.
Kipigo hicho cha pili mfululizo kwenye uwanja huo wa CCM kwa Simba SC, kimerudisha nyuma jitihada na matumaini ya mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara kutwaa taji la Ligi Kuu msimu huu.
Mabao ya Azizi Gila dakika ya 45 na Malimi Busungu dakika 68 aliyefunga kwa penalti, yaliifanya timu hiyo ya Kabuku, Handeni jijini hapa kulinda rekodi yake ya kutopoteza mechi dhidi ya Simba SC na Yanga SC tangu ipande daraja misimu miwli iliyopita.
Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Boniface Mkwasa ameuambia mtandao huu muda mfupi uliopita kuwa kikosi kilitua salama jijini hapa kwa basi kikitokea Dar es Salaam ambako juzi kilishinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar FC kwenye Uwanja wa Taifa na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Bara kikiwa na pointi 34, moja mbele ya mabingwa watetezi Azam FC baada ya mechi 17.
"Tumekuja na wachezaji wote isipokuwa (Andrey) Coutinho ambaye bado anaumwa baada ya kuumizwa Mbeya. Mgambo ni wagumu kufungika kwao, lakini kila kitu kina mwanzo," amesema Mkwasa.
Katika msimu wake wa kwanza Ligi Kuu ya Bara 2012/13, Mgambo ilitoka 1-1 na Yanga SC Uwanja wa Mkwakwani kabla ya kuwachapa wanajangwani hao mabao 2-1 msimu uliopita.
Timu hiyo inayotamba na nyota wakali wakiwamo Mohamed Samata, Malimi Busungu, Ally Nassoro, Novatus Lufunga, Fuluzulu Maganga na Salim Azizi Gila, tayari imeshatuma salamu kwa Yanga SC baada ya kuwachapa wababe wao 2-0 jana.
0 comments:
Post a Comment