Na Mwandishi Wetu, Tanga
MABINGWA mara ya 24 wa ligi kuu soka Tanzania
bara, Dar Young Africans wamevunja mwiko wa Mgambo JKT kutofungwa na vigogo
Simba, Yanga kwa misimu mitatu katika uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga baada ya
kuifumua mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu iliyomalizika jioni hii.
Mabao ya Yanga yamefungwa kipindi cha pili na winga
mwenye kasi Saimon Msuva na mtaalamu wa
magoli ya kichwa na mfungaji bora msimu uliopita, Amissi Tambwe.
Bao la leo ni la
9 kwa Msuva na la 5 kwa Tambwe.
Msimu uliopita, Yanga walipoteza dira ya kutwaa
ubingwa kufuatia kuchapwa 2-1 na Mgambo katika uwanja huu wa Mkwakwani, lakini
leo wamelipa kisasi.
Mgambo waliwafunga Simba 2-0 jumatano ya wiki hii,
lakini leo mambo yamewageukia kwa kula kichapo kama hicho.
Kwa matokeo waliyopata Yanga wameendelea kujikita
kileleni kwa kufikisha pointi 37, pointi nne mbele ya Azam fc watakaocheza na
Coastal Union kwenye uwanja huo huo wa Mkwakwani.
Hii ilikuwa mechi 18 ya Yanga na Azam fc watacheza
mechi ya 18 kesho. Kama watashinda wataendelea kuwa nyuma kwa pointi moja na
kama watatoa sare watakuwa pointi tatu nyuma ya Yanga.
RIPOTI YA MECHI
Mapema dakika ya 3’ Mliberia Kpah Sherman
alimgeuza beki wa Mgambo Novatus Lufunga eneo la mita sita na kuachia
shuti kali lililopaa juu ya lango.
Dakika ya 8’ Salim Aziz Gila alipiga shuti nzuri
akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini bunduki yake haikulenga lango lililokuwa
chini ya ulinzi wa Ally Mustapha ‘Bartez’.
Dakika 1’ baadaye Gila aliingia tena eneo la
hatari akipomkea mpira mrefu kutoka katikati ya uwanja, lakini shuti lake
halikuwa na macho.
Dakika ya 11’ Mgambo walipata kona ya kwanza iliyochongwa
na Malim Busungu, lakini kipa Mustapha akaudhibiti mpira.
Baada ya kona hiyo mpira ulibadilika na ukawa wa butuabutua
kwa timu zote kutokana na uwanja kuwa na maji na matope kulikosababishwa na
mvua zinazoendelea ukanda wa Pwani.
Mipira ya chini ilikuwa inakataa, lakini Yanga
walijitahidi kutuliza mpira chini na haikuwa rahisi kupenya ngome ya Mgambo
waliokuwa wanapiga bora liende kila mara mpira ukifika katika eneo lao la
hatari.
Dakika ya 30’ Kpah Sherman aliwachachafwa mabeki
wa Mgambo Salim Kipanga na Ramadhan Mlima, na beki akimpigia Saimon Msuva pasi
eneo la 18’ lakini mfungaji huyo bora wa Yanga akapiga shuti la juu kabisa.
Dakika 1’ baadaye Mgambo walifanya shambulizi la
kushitukiza, lakini Gila alishindwa kupiga vizuri kichwa.
Dakika Ya 36’ Mgambo walifanya shambulizi kali,
Gila aliingiza krosi safi, lakini Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliokoa na mpira
ukawa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya 38’ Bashiru Chanacha alimpanda mgongoni
Sherman na mwamuzi Simon Mbelwa akaiona na kuamua uwe mpira wa adhabu uliopigwa
vizuri na Haruna Niyonzima, lakini mlinda mlango Godson Mmasa aliudaka mpira huo
kwa utulivu.
Dakika ya 39’ Said Juma Makapu alioneshwa kadi ya
njano kwa kosa la kumchezea madhambi beki wa kushoto wa Mgambo, Salim Mlima
aliyekuwa anakwenda kujaza krosi kutoka winga ya kushoto.
Almanusura Yanga waandike bao dakika ya 42’,
lakini Msuva alishindwa kutumia pasi nzuri ya Sherman eneo la mita sita kutoka
golini, mlinda mlango Mmasa akaudhibiti mpira.
Dakika ya 44’ Msuva alipata nafasi nyingine,
lakini alipiga shuti mtoto ‘shuti mboga’ kwa kipa Mmasa. Yanga wakarejea tena
kushambulia, lakini mabeki wa Mgambo walisimama imara.
Dakika 45’ za kipindi cha pili zilikamilika kwa
suluhu (0-0).
Kiujumla mpira haukuwa na ufundi kwa dakika zote
za kipindi cha kwanza kutokana na uwanja kuwa na matope.
Lakini Yanga walitengeneza nafasi nyingi, lakini
Msuva na Sherman walishindwa kuzibadili kuwa magoli.
Mgambo walifika langoni mwa Yanga na kutengeneza
nafasi kadhaa, lakini kulikuwa na ugumu wa kupiga mashuti kutokana na uimara wa
mabeki Kelvin Yondan na Cannavaro.
Nidhamu ya ulinzi na kukaba vizuri kuliwaokoa
Mgambo japokuwa walifanya makosa mengi ya kumuachia nafasi Msuva ambaye unaweza
kusema dakika 45’ za kipindi cha kwanza hazikuwa upande wake.
Kipindi cha pili mpira ulianza kiubabebabe kwa
wachezaji wa timu zote na kila timu ilitengeneza nafasi dakika za mapema,
lakini umakini wa washambuliziaji ulikuwa mdogo.
Dakika ya 45’ Amissi Tambwe alipiga shuti
lililodhibitiwa na Kipa Mmasa. Dakika 1’ baadaye Fuluzuru Maganga alichuana na
Cannavaro na beki huyo wa Yanga akaonekana kumpiga na bega na Maganga
akajiangusha kwa minajiri ya kupigwa, lakini mwamuzi akamuonesha kadi ya njano
akidai anamdanganya.
Dakika ya 50’ beki wa Mgambo Ramadhani Mlima
alichezewa vibaya na Msuva na muamuzi Mbelwa akamuonesha kadi ya njano winga
huyo wa Yanga.
Dakika ya 56’ Mbuyu Twite alikwenda benchi na
nafasi yake ikachukuliwa na Juma Jafar Abdul.
Mabadiliko hayo yalitokana na Twite kuonekana hana
ubora tangu kipindi cha kwanza.
Dakika ya 57’ Mgambo walifanya shambulizi zuri,
lakini mabeki wa Yanga waliokoa shuti la Ally Nassor aliyewafunga Simba goli
safi siku ya jumatano.
Dakika ya 60’ bahati iliendelea kukosekana kwa
Msuva, alimalizia vizuri krosi ya Juma Abdul, mpira ukagonga mwamba wa juu
pembeni upande wa kulia na kutoka nje.
Dakika ya 66’ Yanga walipanga mipango safi,
Niyonzima akapiga krosi kutoka winga ya kushoto, mabeki wa Mgambo wakatoa mpira
nje na kuwa kona iliyozaa kizazaa, lakini haikuzaa goli.
Dakika ya 68’ kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm
alimtoa nje Kelvin Yondan na nafasi yake kuchukuliwa na Rajab Zahir. Mabadiliko
haya yaliwashitua wengi, lakini kiufundi tayari Yondan alikuwa ameanza
kuhamanika, hivyo asingekuwa na msaada zaidi kwa dakika zilizosalia.
Dakika ya 69’ Niyonzima alipiga shuti kali, kipa
Mmasa alikwenda juu na kugusa mpira ukatoka nje na kuwa kona ambayo haikuzaa
matunda.
Yanga walichangamka zaidi na kuendelea kulisakama
lango la Mgambo, lakini walinzi wa timu hiyo ya jeshi la kujenga Taifa
walikomaa kama kawaida yao kuokoa hatari zote.
Dakika ya 75’ Oscar Joshua alipiga krosi nzuri,
Tambwe akapiga kichwa, lakini kipa Mmasa akaudaka vizuri kabisa.
Dakika ya 77’ Saimon Msuva baada ya kosakosa za
hapa na pale aliandika bao la kuongoza kutokana.
Uliingizwa mpira wa kwanza mabeki wa Mgambo
wakatoa, Juma Abdul akajaza tena mpira na ukapigwa kichwa na Rajab Zahir na
ndipo Msuva alipounganisha bila kutuliza na gozi la ng’ombe kutinga nyavuni.
Dakika ya 79’ Sherman alitoka nje na nafasi yake
ikachukuliwa na Hussein Javu.
Dakika ya 83’ Amissi Tambwe alipiga kichwa cha
hatari na kujaza mpira nyavuni akiiandikia Yanga goli la pili akiunganisha
krosi ya Saimon Msuva.
0 comments:
Post a Comment