Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Uongozi wa Yanga SC umemtaka Rais wa TFF, Jamali Malinzi kuivunja kamati ya mashindano ya shirikisho hilo la soka nchini kutokana na kubadiliko ya mara kwa mara ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Aidha, klabu hiyo ya Jangwani imewataka Kaimu Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB), Fatma Shibo na viongozi wa Simba SC waliohusika katika kumruhusu mshambuliaji Ibrahim Ajibu wa Simba SC kucheza mechi iliyopita dhidi ya Prisons FC ilhali alikuwa na kadi tatu za njano, wajiuzulu katika nyazifa wanazozishikilia.
Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, amesema jijini Dar es Salaam leo mchana kuwa uchunguzi uliofanywa na klabu hiyo ndani ya shirikisho na TPLB, umebaini kuwa taratibu zilizotumika katika kumruhusu Ajibu acheze mechi dhidi ya Prisons FC na inayofuata dhidi ya Yanga SC, hazikufuata misingi, taratibu na kanuni za ligi za shirikisho.
"Mchezaji Ibrahim Ajibu tumebaini ana kadi nne za njano alizoonyeshwa katika mechi dhidi ya Stand United FC Uwanja wa Taifa Oktoba 4, Polisi Moro FC dhidi ya Simba SC Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Februari 15, Stand United FC dhidi ya Simba SC Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga Februari 22 na Simba SC dhidi ya Prisons FC Uwanja wa Taifa Februari 28," Muro amesema.
"Kutokana na tukio lenyewe kuwa la kidhalimu na lenye kutaka kurudisha nyuma maendeleo ya soka la Tanzania, sisi (Yanga SC) tunaitaka TFF kuingilia kati utata huu kwa kuipoka pointi 3 klabu ya Simba SC ilizozipata katika mechi namba 125 dhidi ya Prisons FC kwa sababu ilitumia mchezaji asiye sahihi katika mchezo usio sahihi kwa mchezaji husika.
"Pili, tunalitaka shirikisho litoe adhabu kali kwa viongozi wote wa Simba SC na mchezaji husika kwa kikiuka kanuni na taratibu za uendeshaji wa ligi.
"Tatu, tunamtaka Kaimu Ofisa Mtendaji wa TPLB, Fatma Abdallah Shibo, ajiuzulu kutokana na kupindisha sheria na taratibu na pia kupotosha umma wa Watanzania kuhusu sheria na kutoa kibali hewa cha kuruhusu mchezaji Ibrahim Ajibu kucheza dhidi ya Prisons huku akiwa na kadi nne za njano," amesema zaidi Muro.
Aidha, mtangazaji huyo wa zamani wa ITV na TBC, amelitaka shirikisho kutengua uteuzi wa Makamu wa Rais wa Simba SC, Geofrey Nyange 'Kaburu' ndani ya bodi na Kamati ya Mashindano kwa vile kiongozi huyo ana maslahi binafsi katika vyombo hivyo vya TFF.
"Inakuwaje kiongozi mmoja wa klabu awe na nyazifa tatu ndani ya vyombo vya TFF. Hwaoni kwamba kiongozi huyu ana maslahi na klabu yake ya Simba na ndiye anayeleta hizi vigisu vigisu vya Yanga SC kupangiwa ratiba za ovyo?" Amehoji Muro nakuongeza:
"Kama suala hili halitafanyiwa kazi, basi inabidi kila klabu iwe na mwakilishi kwenye vyombo vya TFF. Kiongozi mmoja wa klabu yumo katika kamati ya mashindano, ni mjumbe wa bodi ya ligi na mjumbe wa kamati ya utendaji pia," amesema zaidi Muro.
0 comments:
Post a Comment