Sunday, March 1, 2015

YANGA SC ndio timu pekee ya Tanzania iliyofuzu kucheza raundi ya kwanza ya michuano ya kimataifa barani Afrika baada ya kuitupa BDF XI ya Botswana kwa wastani wa mabao 3-2 katika mechi mbili za kombe la Shirikisho.
Yanga walishinda 2-0 Dar es salaam (februari 14 mwaka huu, uwanja wa Taifa, na juzi wakachapwa 2-1 na BDF mjini Gaborone.
Azam fc wametolewa jana usiku ligi ya mabingwa Afrika na Al Merrikh ya Sudan kwa wastani wa mabao 3-2 kufuatia mabingwa hao wa Tanzania bara kukubali kipigo cha 3-0, mjini Khartoum.
Mechi ya kwanza (februari 15 mwaka huu) walishinda 2-0 uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Huko visiwani Zanzibar, KMKM nao walitupwa nje ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika kwa wastani wa mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Mabingwa mara 27 wa Sudan na timu iliyoshiriki mara 27 michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, Al Hilal, walishinda 2-0 nyumbani kwao Omdurman na jana wakafungwa 1-0 na KMKM uwanja wa Amaan Zanzibar.
Leo katika uwanja Amaan, Polisi FC ya Zanzibar inawakaribisha CF Mounana kutoka Gabon katika mechi ya marudiano ya kombe la shirikisho.
Polisi walifungwa 5-0 ugenini, leo wanahitaji ushindi wa mabao 6-0 ili kusonga mbele. Jambo hili si dogo na nafasi yao ni finyu japo mpira wa miguu huwa una matokeo ya ajabu.
Azam wametupwa nje ligi ya mabingwa

Kwa mazingira haya, Tanzania inaweza kubaki na timu ya Yanga tu katika michuano ya Afrika.
Tayari mpinzani wa Yanga raundi ya kwanza ya kombe la Shirikisho amepatikana jana.
FC Platinum ya Zimbabwe itachuana na Yanga raundi inayofuata baada ya jana kuichapa Sofapaka 2-1 mjini Harare. Platinum walipata ushindi kama huo mjini Nairobi majuma mawili yaliyopita. Wamesonga kwa wastani wa mabao 4-2.
Timu hii inayoshiriki ligi kuu ya Zimbabwe ilianzishwa miaka 20 iliyopita na haijawahi kucheza kombe la Shirikisho, zaidi ilicheza ligi ya mabingwa Afrika 2012 ambapo ilitolewa raundi ya awali.
Mwaka 2010 timu hii ilijulikana kwa jina la Mimosa FC. Mwaka 2011 ilichukua ubingwa wa ligi kuu Zimbabwe na mwaka huo huo mwezi januari walibadilisha jina lao na kuitwa FC Platinum.
Yanga watachuana nao katika mechi mbili zitakazopigwa uwanja wa Taifa na Mandava kule Harare Zimbabwe.
Soka la Afrika lina fitina nyingi, kila timu inapokuwa nyumbani inajaribu kufanya kila linalowezekana kuwaondoka wapinzani mchezoni.
Tumeshuhudia jinsi Azam walivyofanyiwa na Al Merrikh siku ya kwanza tu walipowasili, walipewa basi chakavu kupindukia, hata uwanja wa mazoezi waliotumia ni wa 'kisela' tu.
Lengo la Waarabu lilikuwa ni kuwachanganya Azam wakijikute wanafikiria kupambana na fitina hizo badala ya kuwa makini na maandalizi ya mechi.
Mbali na kuwa na uwezo wa kucheza soka kiufundi, Waarabu wamejaaliwa mbinu nyingi za kutafuta matokeo nchi ya uwanja, mfano klabu za Misri na Sudan na mataifa mengine.
Yanga wanakwenda kuchuana na FC Platinum, mechi hizi mbili zitakuwa ngumu na lazima maandalizi yaanze mapema.
Kuwafunga Sofapaka nyumbani na ugenini si jambo dogo, lazima wawakilishi wa Tanzania, Yanga, wajipange kikamilifu.
Unaweza kubeza uchanga wa Platinum kwenye michuano ya Afrika ukilinganisha na Yanga, lakini mpira umebadilika. Timu zinakua na kuwekeza katika mpira, lolote linaweza kutokea.
Yanga waanze maandalizi mapema, wajipange kutumia vizuri uwanja wa nyumbani.
Azam walishinda 2-0, walipoteza nafasi nyingi mno, wangeshinda mpaka magoli 6.
Nilijua masihara kama yale yatawagharimu, wenzao jana wamewafundisha nini cha kufanya. Mtaji wa magoli mawili sio mkubwa unapoenda kucheza ugenini. Hata Yanga walicheza mpira mzuri, lakini walikuja kukosa nidhamu kipindi cha pili wakaruhusu magoli mawili na kama wangezembea kidogo wangefungwa mengine.
Kikubwa siku Yanga wakienda Zimbabwe wasije pambana na fitina.
Viongozi watatakiwa kuwa na wajibu wa kuiandaa timu kisaikolojia na kuepuka kuwaweka wachezaji katika imani za kuonewa na wenyeji.
Mtu akikufanyia fitina katika mpira, usipambane na fitina hizo, jikikite katika maandalizi ya mechi, atajiona mjini.
Lakini uki-paniki, wewe unashindwa yeye anafanikiwa. Kubali changamoto zozote zile, zione, ziache, angalia mechi tu.
Naamini Yanga watajipanga vizuri na mechi ya nyumbani watashinda magoli mengi ili kujiweka mazingira salama.
Hongereni Yanga kwa kututoa kimasomaso Watanzania!

0 comments:

 
https://www.sexmutant.com/ https://www.sexindrag.com/ porn movies sex videos hd porno video