Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa siku ya jumapili kati ya Simba SC na Young African utakaofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 kamili za jioni.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro, akisaidiwa na Soud Lila (DSM) mshika kibendera wa kwanza, Florentina Zabron (Dodoma) mshika kibendera wa pili, Mwamuzi wa akiba Israel Mjuni (DSM), na kamisaa wa mchezo ni Ame Santimeya (DSM).
Viingilio vya mchezo huo, VIP A sh. 40,000, VIP B sh. 30,000, VIP C sh. 20,000, Rangi ya Machungwa (Orange) sh. 10,000, huku Rangi ya Bluu na Kijani ikiwa ni sh. 7,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa keso (jumamosi) saa 2 kamili asubuhi katika vituo vya, Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), BigBon (Kariakoo), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya uwanja siku ya jumapili kwa kupitia barabara ya Mandela na Uwanja wa Uhuru, barabara ya Chang'ombe itafungwa kuanzia saa 12 kamili asubuhi.
TFF inawaomba, wapenzi, washabiki na wadau wa mchezo kununua tiketi katika vituo vilivyotajwa ili kuepuka kuuziwa tiketi bandia, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mchezo, mashabiki wenye mabegi, silaha, vilevi na chupa za maji hawataruhusiwa kuingia navyo uwanjani.
Aidha katika mchezo huo TFF itatoa ujumbe maalum kupitia kwa wachezaji kuhamasisha juhudi za Taifa za kuzuia mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
NKONGO KUCHEZESHA ZESCO Vs AS KALOUM Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania mwenye beji ya FIFA, Israel Mjuni Nkongo amechaguliwa kuchezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) kati ya wenyeji Zesco FC ya Zambia dhidi ya AS Kaloum ya Guinea.
Katika mchezo huo wa kwanza wa mzunguko wa pili, Nkongo atasaidiwa na washika kibendera John Kanyenye na Josephat Bulali na mwamuzi wa akiba Waziri Sheha wote kutoka Tanzania, huku Kamisaa wa mchezo akiwa Mayixole Elvin Shishana kutoka nchini Afrika Kusini
Mchezo huo unatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 13,14,15 Machi mwaka huu nchini Zambia.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
0 comments:
Post a Comment