Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Yanga SC hawajapoteza mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi
ya mahasimu wao Simba SC kwa msimu wa tatu sasa, na mchezo ujao wa ‘ Dar es
Salaam derby’ siku ya Jumapili ijayo utakuwa ni mchezo wa sita. Mara ya mwisho
Simba kuishinda Yanga katika ligi kuu ni Mei 7, 2012 walipochomoza na ‘ ushindi
mkubwa zaidi katika karne’ . Simba ilishinda mabao 5-0 msimu ambao walitwaa
ubingwa wao wa mwisho katika ligi kuu.
Yanga imeifunga Simba mara moja tu katika michezo mitano
iliyopita ya ligi kuu na wataingia kwa mara ya sita mfululizo ‘ wakiwa katika
umbo la ushindi’ siku ya Jumapili ili kukamilisha msimu wa tatu pasipo kufungwa
na mahasimu wao hao katika ligi kuu.
Msimu wa 2012/13 timu hizo ‘ watani wa jadi’ zilifungana bao 1-1 katika
mchezo wa mzunguko wa kwanza, kisha Yanga ikaishinda Simba kwa mabao 2-0, Mei,
2013 na kutwaa ubingwa wao wa 24.
Msimu wa 2013/14 timu hizo zilitengeneza ‘ mchezo wa aina
yake’, Oktoba, 2013. Yanga walimaliza dakika 45 za kwanza wakiwa katika kiwango
cha juu huku wakiwa mbele kwa mabao 3-0, kufikia dakika ya mwisho ya mchezo huo
Simba ‘ walikomboa’ magoli yote na kutengeneza sare ya 3-3. Katika mchezo wa
marejeano siku ya mwisho ya msimu, April 24, 2014 Yanga walisawazishia kupitia
kwa Saimon Msuva zikiwa zimesalia dakika chache mchezo kumalizika na
kutengeneza sare ya kufunga bao 1-1.
Oktoba, 2014 timu hizo zilitengeneza sare ya nne mfululizo
katika ligi kuu baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana. Katika mchezo wa
mzunguko wa kwanza msimu huu Yanga waliingia uwanjani wakiwa na matumaini
makubwa ya kushinda lakini wakajikuta wakibanwa mbavu na Simba ambayo ilianza
na wachezaji sita kutoka timu yao ya pili.
Patrick Phiri ndiye mwalimu wa mwisho wa Simba kuikabili
Yanga katika ligi kuu. Phiri alitimuliwa klabuni hapo mara baada ya kupoteza
mchezo dhidi ya Kagera Sugar mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana. Nafasi ya
Mzambia huyo kwa sasa ipo chini ya Mserbia, Goran Kopunovic. Goran hajawahi
kushiriki katika mchezo wa ‘ Dar es Salaa Pacha’, baada ya kufanya kazi Rwanda
na Vietnam, Goran atakutana na presha kubwa katika mchezo wa ‘ tatu kwa ukubwa
barani Afrika’. Mchezo ambao mashabiki huzimia na wengine hupoteza maisha kwa
bahati mbaya kutokana na presha.
Marcio Maximo ndiye mwalimu wa mwisho kuifundisha Yanga
katika ligi kuu, mkufunzi huyo raia wa Brazil alitimuliwa kazi mara baada ya
Yanga kufungwa na Simba mabao 2-0 Disemba, 2014 katika mchezo wa hisani wa ‘
Nani Mtani Jembe-2’. Lakini katika ligi kuu kocha huyo aliendeleza kutunza
rekodi ya Yanga kutofungwa na Simba tangu waliporuhusu kipigo kikubwa cha mabao
5-0 miaka mitatu iliyopita. Maximo ndiye mwalimu aliyeiongoza Yanga katika
suluhu ya 0-0 Oktoba mwaka jana.
Hans tayari anajua presha ya SIMBA NA YANGA kwa kuwa tayari
alishawahi kuiongoza Yanga kusawazisha katika mchezo wa mwisho wa msimu
uliopita. Ni kocha ambaye ameifanya Yanga kuwa na mchezo wa kushambulia na
kufunga mabao. Kumbuka Yanga haifungwa na Simba katika ligi katika michezo
mitano mfululizo huku wakishinda mara moja. KUELEKEA ‘ Dar es Salaam derby ‘
Jumapili hii niteendelea kukuletea rekodi zinazocheza kuhusu mahasimu hao.
Kesho tutatazama ‘ Mbinu na ufundi wa makocha’
0 comments:
Post a Comment