Timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni (Beach Soccer)
inatarajiwa kucheza na timu ya Taifa ya Misri siku ya ijumaa majira ya saa 10
kamili jioni, mchezo utakofanyika katika klabu ya Escape 1 Msasani jijini Dar
es salaam.
Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kinaendelea na mazoezi
kujiandaa na mchezo huo, ambapo kwa takribani wiki mbili kipo kambini Bamba
Beach wakijifua kwa mchezo huo.
Tanzania ilifuzu hatua ya pili baada ya kuiondoa timu ya
Taifa ya Kenya kwa jumla ya mabao 12 -9, na endapo itafanikiwa kuwaota Misri,
itafuzu moja kwa moja kucheza Fainali za soka la Ufukweni zitakazofanyika Visiwa
vya Shelisheli mwezi April mwaka huu.
Waamuzi wa mchezo huo ni Eid Haitham Eid Hassan (Sudan),
mwamuzi msaidzi wa kwanza Abaker Mohamed
Bilal (Sudan), mwamuzi msaidizi wa pili Abdalla Hassain Hassaballa, mtunza muda
(time-keeper) Boubaker Bessem (Tunisia) wakati kamisaa wa mchezo huo ni Khiba
Herbert Mohoanyane kutoka Lesotho.
Nayo timu ya Taifa ya Misri inatarajiwa kuwasili Dar es
salaam kesho (jumatano) mchana, ambapo itafikia katika hoteli ya Double Tree by
Hilton iliyopo Masaki, huku waamuzi wa mchezo huo wakitarajiwa pia kuwasili
kesho na kufikia katika hotel ya Protea Oysterbay.
Aidha siku ya alhamis makocha wa timu zote wataongea na vyombo
vya habari katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume kuanzia majira ya saa
5 kamili asubuhi.
Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini
Misri kati ya Machi 20,21 na 22 mwaka huu.
Kwa niaba ya
familia ya mpira wa miguu , Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF),
inaitakia kila la kheri na ushindi timu ya Taifa ya soka la ufukweni (Beach
Soccer) katika huo dhidi ya Misri.
Wakati huo huo
michezo miwili ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyokuwa iichezwe kesho (jumatano) kati ya JKT Ruvu dhidi ya Young Africans
katika uwanja wa Taifa, na Mgambo Shooting dhidi ya Azam FC uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga imeahirishwa na sasa mechi
hizo zitapangiwa tarehe nyingine.
0 comments:
Post a Comment