Mshambuliaji mahiri wa Mbeya City FC, Peter Mapunda, amesema matokeo mazuri katika mchezo wao unaofuta mwishoni mwa wiki dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ni muhimu.
Mapunda ameyasema hayo mapema leo mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya asubuhi kwenye uwanja wa Sokoine ikiwa ni siku moja baada ya kikosi cha City kurejea kutoka mkoani Morogoro kucheza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar FC uliomazika kwa sare ya bao 1-1.
“Tumetoka Morogoro jana, moja kwa moja tumeingia kufanya mazoezi ya nguvu lengo letu likiwa ni moja tu, kupata matokeo hasa baada ya sare ya mchezo uliopita.
Kupata ushindi Jumapili ndicho kitu pekee tunachokitizama kwa sasa, tumekuwa na matokeo ya sare kwenye michezo mitatu mfululizo ndiyo maana ninasema pointi tatu zinatuhusu Jumapili,” amekaririwa Mapunda katika mtandao rasmi wa klabu ya Mbeya City leo.
Mapunda ambaye mara kadhaa amekuwa akiingia kutoka benchi na kubadilisha mchezo hasa kipindi cha pili, amefunguka zaidi kwa kueleza kuwa wachezaji wanafahamu kuwa wana deni kubwa kwa mashabiki kufuatia sare zilizopita, hivyo wameaahidi kucheza kwa nguvu kubwa kama ambavyo walicheza kwenye mchezo dhidi ya Simba jijini Dar ili kuhakikisha City inanyakua pointi zote 3 Jumapili hii kwenye uwanja wa nyumbani.
0 comments:
Post a Comment