Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi limesema linawashikilia zaidi ya watu 20 baada ya kuwanasa wakiwa na tiketi feki katika mechi ya watani wa jadi, Simba SC na Yanga SC Uwanja wa Taifa Jumapili.
"Katika mechi yetu iliyopita dhidi ya Simba, kulikuwa na watu walikuwa wanauza tiketi feki, baadhi yao tuliwakamata na kuwafikisha polisi. Sisi (Yanga) tulikamata watu nane na wenzetu Simba pia walikamata watu wengi. Jeshi la Polisi lina taarifa za kina kuhusu suala hili," Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, amesema leo jijini hapa.
"Mtafuteni afande Jonas (Mahanga), ambaye ni kiongozi wa Jeshi la Polisi kwenye Uwanja wa Taifa. Anajua kinachoendelea."
Mahanga amekiri kukamatwa kwa watu hao, lakini akaeleza kuwa taarifa zaidi anazo Kamanda wa Polisi Mkoa Maalum wa Kipolisi Temeke kwa kuwa watuhumiwa wote walipelekwa huko.
Sebastian Zacharia, Kaimu RPC Temeke, amesema zaidi ya watu 20 walikamatwa wakiwa na tiketi feki na Mwanasheria wa Serikali amekabidhiwa jukumu la kuwafungulia mashtaka.
Licha ya Uwanja wa Taifa kufurika idadi kubwa ya watazamaji Jumapili, mechi hiyo iliingiza Sh. milioni 437 kutokana na watazamaji 49,758 waliokata tiketi halali kuingia kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuketisha watazamaji 57,558.
Simba SC na Yanga SC wamekuwa wakipinga matumizi ya tiketi za kielektoniki katika mechi zao kwa madai kuwa wanachelewa kupata mgawo wao kutoka Benki ya CBRD inayosimamia mfumo huo wa kisasa.
0 comments:
Post a Comment