Na Oswald Ngonyani
Najua inasubiriwa na wengi, tena
watu wengi mno. Itakuwa ni mechi ya ndani ya uwanja baada ya majigambo na
mbwembwe nyingi za soka la nje ya Uwanja. Pengine utakuwa ni mchezo wa kumaliza
ubishi katika mwanzo mpya wa mwaka 2015.
Wekundu wa Msimbazi wanaochagizwa
na kauli mbiu ya NGUVU MOJA watakuwa wenyeji wa mahasimu wao wakubwa katika
soka la bongo, Dar Young Africans a.ka. Wazee wa MBELE DAIMA, NYUMA MWIKO katika mchezo namba 117 utakaopigwa kunako
dimba la Taifa Jumapili hii.
Kuelekea mchezo huo kumekuwepo na
sarakasi za kila namna sarakasi ambazo kwa kiasi kikubwa zimekwishatolewa
ufafanuzi wa kina japo upande mmoja unaonekana kulaumu zaidi na kuona kama
Uongozi wa Ligi kupitia kwa Kaimu afisa
Mtendaji mkuu wake Bi Fatma Abdallah ulikengeuka.
Sarakasi hizi zilianzia kunako
maamuzi ya Uongozi wa Simba kumtumia mshambuliaji wao Ibrahim Hajib Migomba
ambaye alikuwa mhanga wa kadi tatu za njano kabla ya kukutana na Tanzania
Prisons katika mchezo wa wikiendi iliyopita.
Kuhusu sakata hilo tayari yamekwishazungumzwa
mengi sana na baadhi ya wadau wa kandanda hapa nchini lakini mwisho wa siku
Bodi ya Ligi ambayo ndiyo muamuzi wa mwisho pale inapotokea sintofahamu za
namna hii imekwishaliweka wazi suala hilo.
Kwa mantiki hii ni kama kusema Klabu ya Simba ilikuwa sahihi kumtumia mchezaji
huyo, ambapo kwa mujibu wa TPLB Hajib hatacheza katika mechi dhidi ya Mtibwa
lakini aliruhusiwa kucheza katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons lakini pia
atacheza dhidi ya Yanga Jumapili hii.
Si nia yangu kuendelea
kuyazungumzia hayo kwa siku ya leo. Lengo la makala yangu haya ni kutaka
kuuzungumzia mchezo wa Jumapili baina ya vilabu vikubwa katika historia ya soka
la Tanzania, vilabu Kurwa na Doto, yaani Yanga (1935) na Simba (1936).
Ni mchezo ambao mara zote
huongoza kwa kujaza mashabiki pale Taifa, ni mchezo ambao ndio kila kitu katika
mawanda ya soka la Tanzania. Wakubwa, watoto, Wazee, na hata vijana huonekana
kushikwa na shauku kubwa ya kuushuhudia mchezo huu, ni mchezo unaosubiriwa na
watu wa rika na jinsia zote.
Siku zote matumaini ya wapenzi
wengi wa kandanda hutegemea makubwa sana pale ambapo timu hizi hukutana. Wengi
hutegemea soka ya ushindani kuonekana ndani ya dimba. Wengi hutegemea kiwango
cha hali yajuu kuoneshwa na wachezaji wa timu husika. Kwa kifupi wengi
hutegemea mambo yasiyo haba kutokelezea ndani ya dimba wakati wanaume hawa
wanapopambana.
Wengi wetu hatutegemei kuuona
mpira wa butua butua siku hiyo, ni wazi kuwa hatutategemea kuona ubabe na visa
visivyomithilika ndani ya uwanja. Hapana shaka mimi na wewe tutapenda kuona
kaulimbiu ya FIFA ya ‘FAIR PLAY’ ikipewa nafasi zaidi kuliko sintofahamu
nyinginezo.
Tuna amini kila timu ina kikosi
chenye wachezaji watakaokuwa chachu ya ushindi Jumapili. Achana na historia ya
klabu hizo katika siku za usoni, ni wazi kuwa maandalizi yenye tija kwa kila
timu lakini pia nidhamu ya wachezaji wa timu husika ni moja ya siri ya
mafanikio ambayo timu fulani itaweza kupata matokeo.
Mpira si ugomvi, mpira si visa
lakini pia mpira si lelemama. Wakati wenyeji wa mchezo huo, Timu ya soka ya
Simba wakiwa visiwani Zanzibar kujiandaa na mtanange huo, watani wao wenyewe
wapo Bagamoyo tayari kwa kujiweka sawa kunako mchezo huo.
Pamoja na kauli za mbwembwe za
viongozi wa timu hizo, Bwana Jerry Muro kwa Yanga lakini pia Bwana Iddi Kajuna kwa Simba, ni dakika 90 pekee
ndizo zitakazotoa jawabu stahiki la nani ni nani katika mchezo huo.
Ikumbukwe kuwa Yanga wataingia
katika mchezo huo wakiwa kileleni mwa VPL msimu huu 2014/2015 wakiwa na jumla
ya pointi 31 baada ya kushuka dimbani mara 15 huku Simba wenyewe wakiendelea
kubaki katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 23 baada ya kucheza michezo 16.
Ni mchezo ambao ni wazi kuwa timu
ya Yanga itahitaji ushindi zaidi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa
ubingwa wa VPL kwa msimu huu baada ya kuukosa msimu uliopita 2013/2014.
Lakini pia ni mchezo ambao timu
ya Simba itataka kuongeza idadi ya pointi ili angalau kuwapa morali mashabiki
wake, mashabiki ambao kwa kiasi kikubwa wanaonekana kutokuwa na imani na timu
yao japo katika mchezo wa mahasimu hawa lolote huweza kutokea.
Kiufundi, kila timu ina kikosi
bora katika maana ya mchezaji mmoja mmoja, lakini pia kila timu ina walimu
ambao kwa kiasi kikubwa wanaonekana kuwa na weledi wa kutosha katika mawanda ya
mchezo wa mpira wa miguu. Ni wazi kuwa tutashuhudia mchezo utakaotawaliwa na
ufundi wa hali ya juu zaidi tofauti na michezo mingineyo baina ya timu hizo
siku za nyuma.
Ni matumaini yangu sheria 17 za
FIFA zitafuatwa na kutekelezwa kinaganaga na marefarii watakaohudumu kunako
mchezo huo ili kila timu iweze kukubaliana na kile kitakachopatikana baada ya
mchezo kumalizika, yaani kuridhika na matokeo.
KUELEKEA
MCHEZO WA SIMBA vs YANGA: WACHEZAJI WAWAPE RAHA MASHABIKI WAO KWA KUONESHA
KANDANDA SAFI UWANJANI
Wasalaaaaam
(0767 57 32 87)
0 comments:
Post a Comment