Na Oswald Ngonyani
Kwa siku za karibuni
kumekuwa na hali ya ukinzani mkubwa wa kimtazamo miongoni mwa mashabiki wengi
wa mchezo wa soka hususan wanazi wakubwa wa wachezaji fulani wawili kutoka
katika klabu mbili tofauti zinazocheza ligi moja barani Ulaya.
Wanazi hao wamekuwa
hawaridhiki pale mchezaji mmoja anapozungumzwa kwa mazuri. Mioyo yao huingiwa
na gubu na hata kujikuta wakionesha chuki ya wazi kwa mchezaji anayesifiwa,
lengo hasa ni kutaka kuzipambanua sifa fulani za mchezaji wanayemkubali.
Hivi ndivyo mchezo wa soka
ulivyo, mchezo ambao mbali na kuwa na mashabiki wengi ulimwenguni kote lakini
bado umetawaliwa na vibweka lukuki, vibweka ambavyo kila kunapokucha vinazidi
kushika kasi.
Mpaka leo hii bado kuna
mvutano mkali kuhusu umaridadi wa wachezaji hawa ‘Cristiano Ronaldo wa Real
Madrid na Lionel Messi wa Barcelona’.
Kiuwezo wa ndani ya uwanja
kila mmoja ana upekee wake unaompambanua na hata kuonekana kuwa bora zaidi ya
mwingine. Nakumbuka wakati fulani niliwahi kuandika makala ya uchambuzi kuhusu
wanandinga hawa.
Ni katika makala yale ndipo
nikagundua kitu fulani kuhusu wachezaji hawa. Si watu wa mataifa mengine pekee,
hata watanzania wengi wamegawanywa katika pande mbili za uhusuda wao kwa hawa
jamaa.
Maoni ya watu kutoka pande
zote za nchi kuhusiana na unazi wao kwa wachezaji hawa ni vitu vilivyonifanya
nielewe kuwa kweli akina Messi na Ronaldo ni wachezaji bora wa dunia kwa sasa.
Utamu wa mchezo wa soka
kama unavyonakshiwa na uwepo wa historia na rekodi nyingi zenye kutia hamasa
huzidi zaidi pale rekodi fulani zinapovunjwa na hata kuzua gumzo kwa
wanaozifuatilia rekodi hizo. Hivi ndivyo mchezo wa soka ulivyo, karibu kila
siku mambo mapya yanaibuka na hata kujenga historia kamambe yenye kutia hamasa.
Achana na sifa tukufu wanazopewa
akina Pele na Maradona, nadhani hao jamaa wana upekee wao unaowafanya wawe
maarufu mpaka leo hii kutokana na kile ambacho waliwahi kukifanya enzi za ujana
wao.
Nyuma ya watu hawa kuna mtu
fulani wa umri wa makamo ambaye hazungumzwi sana, anaitwa Raul Gonzalez kipenzi
cha mashabiki wengi wa soka nchini Hispania ambaye alipewa sifa iliyotukuka
sana pale Santiago Bernabeu na hata kujikuta akiwa mchezaji wa miaka mingi
zaidi wa Klabu ya Real Madrid.
Mpaka tunaanza siku ya
kwanza ya wiki hii, Mwanamume huyu alikuwa anashikilia rekodi fulani, rekodi
ambayo alidumu nayo kwa muda mrefu sana kutokana na wachezaji wengi wa sasa
kuonekana kutokuwa na ‘mzuka’ wa kuivunja rekodi hiyo.
Mashabiki wengi wa Real
Madrid walikuwa na hamu kubwa ya kumuona mchezaji wao kipenzi akiivunja rekodi
hiyo. Nadhani kuna hali fulani ya chuki ilikuwa imewatawala ndani ya mioyo yao,
hawakuwa tayari rekodi ya kipenzi chao Gonzalez ivunjwe na mtu wanayemchukia
sana, Lionel Messi.
Mashabiki wengi wa Madrid
wanamchukia Messi kwa sababu ya maneno yanayozungumzwa mara kwa mara na baadhi
ya watu wa familia ya mchezo wa soka kuwa Messi ni zaidi ya Ronaldo. Kwao kauli
hizo ni kama dhihaka, hawazitaki kuzisikia hata kidogo.
Wanaamini Ronaldo wao ndiye
fundi pekee wa mpira kwa sasa kuliko wengine wote, hii ndiyo imani yao na kamwe
hawawezi kubadilika. Hawakutaka Messi atangulie kuvunja rekodi ile, walitaka kipenzi
chao Ronaldo afanye vile lakini haikuwezekana.
Raul alikuwa akishikilia
rekodi ya kufunga mabao 71 na kuwa mfungaji mwenye mabao mengi zaidi kwenye
Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu kuanzishwa kwake miaka 60 iliyopita.
Kabla yake Messi alikuwa
hapewi nafasi, lakini mabao mawili aliyofunga Messi wakati Barcelona ikiitwanga
Ajax kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, yamesitisha ndoto za
Ronaldo aliyekuwa kipewa nafasi kubwa.
Muargentina huyu aliyekuzwa
pale Lamasia amefikisha mabao 71 huku Ronaldo akibaki na mabao 70 na
anachotakiwa sasa ni kufunga zaidi ili kumfikia Messi na Raul na ikiwezekana
kuwapita wote vinginevyo ataendelea kusubiri kwa muda.
Takwimu
za sasa za ufumaniaji wa magoli mengi katika UEFA zinamweka Messi wa Barcelona
katika nafasi ya kwanza akiwa amelingana na Gonzalez kwa kuwa na magoli
71 huku Ronaldo akiwa na magoli 70.
Nyuma
ya wachezaji hawa watatu kuna wengine wawili ambao wanafuatia. Nyota wa zamani
wa Manchester Uniter Ruud Van Nistelrooy mwenye magoli 56 na Thiery Henry,
mfaransa aliyewahi kuvuma pale Emirates akiwa na hazina ya magoli 50 kwa sasa.
Kimsingi, rekodi ya Raul
Gonzalez ambayo kwa miaka mingi sasa imekuwa ikisakwa kwa udi na uvumba
imekwishavunjwa tayari. Ninaamini tunakwenda kushuhudia rekodi mpya kabisa
ambayo mmoja kati ya wachezaji hawa wanaochuana kwa sasa ataiweka na hata
kulifanya jina lake kutamkwa mara kwa mara katika vinywa vya mashabiki wengi wa
mchezo wa soka duniani kote.
Ni wazi kuwa, wote wawili
wanaweza wakaweka historia ya pekee zaidi katika ufumaniaji wa nyavu katika
michuano ya UEFA lakini pia wachezaji wengine wana nafasi pia ya kuifikia
rekodi hii na hata kuanza ukurasa mpya wa rekodi mpya zenye kuongeza chachu
katika mawanda ya soka la sasa.
Naomba kutamatika.
(Maoni/Ushauri tuma kwenda
namba 0767 57 32 87. Kitabu changu ‘MAGWIJI WA SOKA WALIOWAHI KUITIKISA DUNIA…..’
kipo jikoni kikiendelea kupikwa, Mola akipenda Mwezi Desemba kitakuwa sokoni,
NITAWAHABARISHA)
0 comments:
Post a Comment