Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Simba imesubiri kwa zaidi ya miezi
16 ili kupata ushindi mfululizo walau katika michezo mitatu ya ligi kuu
Tanzania Bara. Baada yaushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Tanzania Prisons wiki
mbili zilizopita, ' Wekundu wa Msimbazi' waliishinda Yanga SC kwa goli 1-0 wiki
iliyopita kabla ya kikosi hicho cha mkufunzi, Goran Kopunovic kuonesha '
ukomavu' na kuishinda ' timu inayowasumbua sana' Mtibwa Sugar kwa goli 1-0 siku
ya jana Jumamosi.
Kitendo cha timu hiyo kushinda
michezo mitatu mfululizo ' imejivuta ' hadi katika nafasi ya tatu ikiwa na
alama 29 baada ya kucheza michezo 18. Mfungaji bora wa klabu hadi sasa, Mganda,
Emmanuel Okwi alifunga ' goli la stahili yaje' katika dakika ya mwisho ya
mchezo. Akipokea pasi ya ' mtaalamu wa pasi ndefu' kiungo Abdi Banda, Okwi
alimchungulia golikipa 'aliyekuwa akipoteza muda' Said Mohamed katika dakika za
nyongeza na kuifanya timu yake kutoa presha kwa vinara Yanga walio na alama 31
na Azam FC walio nafasi ya pili na alama 30.
Mara baada ya mchezo huo, Okwi
alisema; " Kufunga magoli mazuri ni kawaida yangu, nachofurahi ni timu
kupata pointi tatu" ni maneno mazuri ambayo mashabiki wa Simba watapenda
kuyasikia mara kwa mara kutoka kwa mchezaji ambaye huisumbua klabu yao katika
wakati muhimu. Okwi amefunga mabao nane hadi sasa katika ligi kuu, bila shaka
mchango wake katika ufungaji umekuwa ukiimarisha timu hiyo katika siku za
karibuni.
Kama mchezaji huyo mwenye miaka 24
ataendelea kufanya kazi yake bila shaka atarudisha hamasa ya mashabiki ambao
walijitokeza kwa uchache katika mchezo dhidi ya Mtibwa. Mashabiki wachache
waliojitokeza katika mchezo huo wa ' ushindi uliochelewa zaidi msimu huu'
waliimba kwa ' kupaza' sauti; Okwiii, Okwiii, Okwiii...ni ishara kwamba
mashabiki wana imani kubwa na mchezaji huyo, huku mchezaji mwenyewe akionesha
kupiga hatua nyingi katika uwajibikaji.
Baada ya kupoteza mchezo wa ugenini
dhidi ya Stand United mwishoni mwa Februari, Okwi amefunga katika michezo
mitatu mfululizo huku mabao yake ya ' video' katika gemu dhidi ya Yanga na
Mtibwa yakisimama kama 'magoli muhimu zaidi hadi sasa'. Sasa huyu ndiye kinara
na mchezaji wa hatari zaidi katika safu ya mashambulizi ya Simba.
Katika michezo mitatu iliyopita Simba imefunga
jumla ya magoli saba huku wachezaji wawili ( Okwi & Ibrahimu Ajibu)
wakifunga magoli matatu matatu kila mmoja, kiungo mshambulizi, Ramadhani
Singano pia ni miongoni mwa wafungaji wa mabao hayo. Sasa Simba SC inashinda
kwa kutumia magoli ya washambuliaji. Licha ya ulinzi ikiendelea kuimarika baada
ya kucheza dakila 270 pasipo kuruhusu nyavu zao kuguswa.
Mechi nane za mbele ni muhimu zaidi kwa Simba,
jitihada kubwa waliyoifanya hadi sasa inatakiwa kuongezwa mara mbili zaidi huku
suala la umakini likipaswa kupewa kipaumbele kikubwa. Kufunga magoli mazuri ni
kawaida kwa Okwi, lakini anahitaji pointi tatu katika kila gemu huku akisema
mwendo huu wa Simba bado si wa kujivunia kwa kuwa timu inakwenda katika kipindi
kigumu zaidi msimu huu.
0713 08 43 08
0 comments:
Post a Comment