Mlinzi wa kutumainiwa wa City Juma Nyosso anatarajia kurejea uwanjani kutumikia timu yake kwenye mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Azam Fc uliopangwa kuchezwa Chamanzi Complex mapema mwezi ujao.
Nyosso aliyekuwa akitumikia adhabu ya kufungiwa michezo 8 atakamilisha kifungo hicho jumamosi ya tarehe 4.4 2015 wakati City itakapokuwa uwanjani kucheza na Ndanda Fc kwenye mchezo mwingine wa ligi hiyo utakaochezwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoni Mtwara.
Akizungumza mapema leo Katibu Mkuu City Emmanuel Kimbe amesema kurejea kundini kwa Nyosso kutaongeza nguvu kubwa kikosini hasa kwenye wakati huu ambao timu inafanya jitihada za dhati kupata matokeo ili kusaka nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.
“Kila mmoja hapa anayo kumbukumbu ya kazi nzuri aliyoifanya Nyosso kwenye mechi alizocheza kabla ya kupata adhabu, niseme wazi kuwa ni mchezaji muhimu ambaye uwepo wake unaongeza kitu, kila mmoja anaweza kuitafsiri adhabu ile kwa namna yake, lakini uwanjani kuna mambo mengi, kuna wakati unaweza kufanya jambo usijue ulilifanya vipi, kizuri kwetu ni kuwa anamaliza adhabu hiyo na kurudi kuitumikia timu” alisema.
Wakati huo huo nyota wanaunda safu ya ushambuliaji Paul Nonga, Mwegane Yeya na Themi Felix wamesema wako tayari kuwasha moto ndani ya uwanja wa Nangwanda sijaona kwa lengo moja tu la kuipatia City ushindi kwenye mchezo dhidi ya ndanda fc.
wakizungumza kwa nyakati tofauti nyota hao waliweka wazi kuwa hivi sasa city iko kwenye kiwango kizuri tofauti na ilivyokuwa kwenye michezo kadhaa iliyopita jambo ambalo kwa anamna moja ama nyingine lilikuwa linachangia kukosekana kwa matokeo.
“Takribani michezo mitano tuliyolicheza awali tulikuwa na matatizo kwenye kikosi wachezaji wengi walikuwa majeruhi hiyo ilitufanya kushindwa kucheza kwenye ubora, sasa tuko sawa na kila mmoja ana ari kubwa ya kutetea na kurudisha kile kilichopotea, nia yetu ni kuiona city inarudi pale juu alisema Themi Felix.
Kwa upande wao Paul Nonga na Mwegane Yeya walisema kuwa wana uhakika City itafanya vizuri kwenye mchezo huo wa Mtwara hasa ukizingatia matokeo mazuri yaliyopatikana uwanja wa Sokoine dhidi ya Stand United juma lililopita.
Katika mchezo huo wa juma lililopita City iliibuka ushindi wa mabao 2-0 yalifungwa na Yufuph Abdalah Sisalo kwa mkwaju wa penalti na Paul Nonga aliyefunga akiunganisha krosi ya Hamad Kibopile.
0 comments:
Post a Comment