Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Baada ya kukaa siku 129 bila ushindi, Mtibwa Sugar FC wameona mwezi leo baada ya kuwachapa majirani zao Polisi Moro FC mabao 2-1 huku Ruvu Shooting Stars wakikiona cha moto kwa kupewa kipigo kama hicho dhidi ya Ndanda FC katika mechi tatu za leo za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mabao ya Mtibwa Sugar FC ambayo kabla ya mechi ya leo ilikuwa imekaa kwa siku 129 ambazo ni sawa na dakika 3,096 sawa na sekunde 185, 760 tangu ilipoifumua Mbeya City FC 2-0 jijini Mbeya Oktoba 26, mwaka jana, yamefungwa na mshambuliaji Mzanzibar, Ali Shomari dakika ya 53 na beki wa pembeni Said Mkopi dakika ya 79 akimalizia kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na beki wa pembeni, David Luhende.
Mshambuliaji aliyekuwa akisotea namba katika kikosi cha Yanga SC, Said Bahanunzi amefunga boa pekee la Polisi Moro FC dakika ya 40 kwa penalti iliyotolewa na refa Richard Kayombo baada ya beki wa kati wa Mtibwa Sugar FC, Salim Mbonde kuunawa mpira ndani ya boksi.
Kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, wenyeji Ruvu Shooting Stars waliokuwa wanahitaji ushindi ili kuishusha Simba SC katika nafasi ya nne baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC.
Mabao ya kikosi cha Meja Mstaafu Abdul Mingange cha Ndanda FC, yamefungwa dakika ya 40 na Jacob Masawe, mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2011/12 akiwa na Toto Africans ya Mwanza, na Omega Seme katika dakika ya 84 wakati wenyeji wamefutwa machozi na Yahya Tumbo dakika ya 41.
Kwa ushindi wa leo, Mtibwa Sugar FC imepanda kutoka nafasi ya nane hadi ya tano katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 22 sawa na Coastal Union FC katika nafasi ya sita wakati Ndanda FC imekwea kutoka nafasi ya 11 hadi nafasi ya 7 ikiwa na pointi 22 pia.
Katika mechi nyingine leo, Tanzania Prisons FC iliyoachana na kocha mkuu, David Mwamaja, licha ya kucheza pungufu tangu dakika ya 25 baada ya Godfrey Mageta kutolewa kwa kadi nyekundu, walifanikiwa kuweka rekodi ya kutopteza mechi kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam baada ya kuilazimisha suluhu JKT Ruvu iliyopanda hadi nafasi ya nnae ikiwa na pointi 20.
Hiyo ni kadi ya pili nyekundu kwa wajelajela hao baada ya beki wao tegemeo Nurdin China kutolewa pia katika mechi yao ya kipigo kikubwa zaidi msimu huu cha 5-0 dhidi ya Simba SC Uwanja wa Taifa jijini hapa Jumamosi.
Prisons FC inayokamata mkia licha ya kufikisha pointi 13 jana, iliilazimisha suluhu Azam FC Uwanja wa Azam katika mechi yao iliyopita.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Prisons umesema umemkabidhi timu Mbwana Makata kurithi mikoba ya Mwamaja kumalizia msimu huu na akifanya vizuri, hususan kuinusuru timu hiyo kushuka daraja, watampa mkataba mnono.
0 comments:
Post a Comment