Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Mahakama Kuu ya Zanzibar imeipiga kalenda kesi inayoukabili uongozi wa Chama cha Soka visiwani humo (ZFA) kutokana na kujitoa kwa mmoja wa walalamikaji katika kesi hiyo.
Kesi ya madai Na. 62 ya mwaka 2014 iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Zanzibar, ilianza kusikilizwa na Jaji Isack Sepetu Januari 20, mwaka huu ikifunguliwa na Haji Ameir Haji, Makamu Mwenyekiti wa ZFA - Unguja na Mwenyekiti wa ZFA - Chakechake, Pemba, Ali Bakar Ali dhidi ya ZFA, Rais wa ZFA, Makamu wa Rais wa ZFA - Pemba, Katibu Mkuu wa ZFA na wajumbe watatu wa kamati ua utendaji ya chama hicho.
Katika kesi hiyo walalamikaji wanadai kuwa watuhumiwa walichota kinyume cha sheria Sh. milioni 108.2 za ZFA kwa nyakati tofauti kati ya Oktoba 2013 na Desemba 2014 kutoka akaunti ya PBZ Na. 021108000540 na fedha nyingine ya ZFA Sh. milioni 363.9 inayodaiwa kuchotwa kinyume cha sheria kutoka akaunti KCB Na. 3300721695 kati ya Oktoba 2013 na Desemba 2014.
Hata hivyo, kesi hiyo haikutolewa uamuzi leo kutokana na mlalamikaji wa pili, Mwenyekiti wa ZFA - Chakechake, Pemba Ali Bakar Ali kujitoa, hivyo kuhitaji uandaaji mpya wa malalamiko ya kesi hiyo.
Katika kesi hiyo iliyochukua dakika 35 jana kwenye Mahakama Kuu ya Zanzibar iliyopo eneo la Vuga, Mji Mkongwe visiwani Zanzibar, mahakama imetoa siku 21 (kuanzia leo Machi 4, 2015) kwa mlalamikaji wa kwanza, Haji Ameir Haji kufanya marekebisho katika idadi ya walalamikaji kutokana na mlalamikaji wa kwanza kujitoa.
Ali Bakar Ali alijitoa Januari 28, mwaka huu wakati kesi hiyo iliposikilizwa kwa mara ya pili na mahakama hiyo na kupangwa kutolewa uamuzi Februari 19, mwaka huu, lakini Jaji alisema uamuzi ungetolewa Machi 4, mwaka huu (leo) kwa vile hakuwa ameandika hukumu katika tarehe iliyokuwa imepangwa awali kwa ajili ya hukumu.
Tayari pande mbili zinazovutana katika kesi hiyo zimeripotiwa zikitamba kuchukuliana hatua zaidi kwa kufungua kesi nyingine za madai kutokana na kashfa za uhujumu wa mali za ZFA.
0 comments:
Post a Comment