Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars chini ya kocha mholanzi Mart Noij, leo hii imelazimisha sare ya kufungana bao moja kwa moja dhidi ya timu ya taifa ya Malawi "The Flames" katika mchezo wa kirafiki uliopo katika kalenda ya shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA iliopigwa katika dimba la uwanja wa CCM kirumba Mwanza.
Ilikuwa ni timu ya Taifa ya Malawi iliyoanza kupata bao katika mchezo huo dakika ya 4 ya mchezo kwa kupitia Mchezaji Essau Kanyenda baada ya mabeki wa stars kujichanganya na kujikuta wakiruhusu bao la mapema kabisa.
Bao hilo la timu ya Taifa ya Malawi lilidumu mpaka mapunziko na kuifanya timu hiyo kwenda mapunziko ikiwa kifua mbele.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kushambuliana kwa zamu na kuwa makini katika safu ya ulinzi, lakini kocha Mart Noij alifanya mabadiliko ya kumtoa mchezaji Amri Kiemba na kumuingiza Mrisho Ngassa.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda katika dakika ya 76, Mrisho Ngassa alitoa pasi safi kwa Mbwana Samatta ambaye bila kuzembea alikwamisha mpira wavuni na kuisawazishia taifa stars na mchezo kumalizika kwa bao moja kwa moja.
0 comments:
Post a Comment