Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio
vya mchezo wa siku ya jumapili kati ya Simba SC na Young African utakaofanyika
kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 kamili za jioni.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro,
akisaidiwa na Soud Lila (DSM) mshika kibendera wa kwanza, Florentina
Zabron (Dodoma) mshika kibendera wa pili, Mwamuzi wa akiba Israel Mjuni (DSM),
na kamisaa wa mchezo ni Ame Santimeya (DSM).
Viingilio vya mchezo huo, VIP A sh. 40,000, VIP B sh.
30,000, VIP C sh. 20,000, Rangi ya Machungwa (Orange) sh. 10,000, huku Rangi ya
Bluu na Kijani ikiwa ni sh. 7,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa keso (jumamosi) saa 2 kamili asubuhi katika
vituo vya, Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom
(Buguruni), BigBon (Kariakoo), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala),
Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya
uwanja siku ya jumapili kwa kupitia barabara ya Mandela na Uwanja wa Uhuru,
barabara ya Chang'ombe itafungwa kuanzia saa 12 kamili asubuhi.
TFF inawaomba, wapenzi, washabiki na wadau wa mchezo kununua
tiketi katika vituo vilivyotajwa ili kuepuka kuuziwa tiketi bandia, ili
kuimarisha ulinzi na usalama wa mchezo, mashabiki wenye mabegi, silaha, vilevi
na chupa za maji hawataruhusiwa kuingia navyo uwanjani.
Aidha katika mchezo huo TFF itatoa ujumbe maalum kupitia kwa
wachezaji kuhamasisha juhudi za Taifa za kuzuia mauaji dhidi ya watu wenye
ulemavu wa ngozi (Albino).
0 comments:
Post a Comment