Na Bertha Lumala, Dar esSalaam
Kocha mkuu wa SC Villa, Sam Ssimbwa aliitosa ofa ya Azam FC ya kuwa msaidizi wa George Nsimbe katika kukinoa kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imefahamika.
Nsimbe ameteuliwa kocha kocha mkuu wa muda wa Azam FC akirithi mikoba ya Mcameroon Joseph Omog, aliyetimuliwa. Nsimbe alitaka Mganda mwenzake Ssimbwa awe msaidizi.
“Ofa imekuja pesa nzuri. $5,000 ni pesa nyingi, lakini inakuwaje niwe msaidizi wa Nsimbe? Ni kujishushia heshima mimi mwenyewe," amekaririwa kocha huyo na moja ya mitandao ya michezo ya Uganda akiponda mawazo ya Nsimbe kuwashawishi Azam wamchukue.
Ssimbwa (48), amefundisha timu 16 ikiwamo timu ya taifa ya Somalia, klabu zote tatu za makabila ya Uganda, ATRACO ya Rwanda, Police FC na Sofapaka (Kenya), huku akidai kuwa kwa sasa ni tajiri mno, hivyo hawezi kukimbilia kazi ya ukocha kwa kukurupuka.
Imeripotiwa nchini Uganda kwamba kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uganda ya U-23, Frank Video Anyau, ndiye aliyekuwa anaunganisha dili la Ssimbwa kutua Azam FC.
Aidha, Ssimbwa ameripotiwa akitaka kurejea kuwanoa mabingwa wa Uganda KCCA FC kwa mara ya tatu baada ya kuwa nao 2002 na 2009.
Villa ilimnasa Ssimbwa Oktoba akipewa jukumu la kuwarudisha wachezaji wa timu hiyo iliyomkuza Emmanuel Okwi wa Simba, katika uchezaji mzuri na wenye weledi.
Hata hivyo, Azam FC imemwajiri Dennis Kitambi kuwa kocha msaidizi baada ya kutimuliwa Ndanda FC ya Masasi, Mtwara.
0 comments:
Post a Comment