Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars itacheza na Malawi
mwishoni mwa wiki hii katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ikiwa ni sehemu ya
michezo ya kirafiki ya Kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, Shirikisho la
soka duniani. Stars inacheza na Mawali ‘ The Flames’ kwa mara ya Tatu ndani ya
miezi 12. Mapema mwaka uliopita ( 2014),
timu hizo zilikutana mara mbili katika michezo ya kirafiki na kutoka sare
katika michezo yote.
Tanzania imepanda kwa nafasi kumi katika viwango vya FIFA
vilivyotolewa mapema mwezi huu hadi kufikia nafasi ya 100, na endapo itaishinda
Malawi inaweza kusogea kwa nafasi walau saba hadi kuwa miongoni mwa timu 100
bora ulimwengu.
Ikiwa na wachezaji kadhaa wanacheza nje ya nchi, Stars ni timu yenye vipaji vingi hivi sasa huku
wachezaji wengi wakiwa chini ya miaka 25. Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ni
miongoni mwa washambuliaji mahiri kwa sasa barani Afrika, wawili hao wanakipiga
katika klabu ya TP Mazembe ya DR Congo, Mwinyi Kazimoto anakipiga katika klabu
ya Qatar ni moja ya wachezaji waandamizi wa Stars ambao tangu mwaka 2009 wamekuwa
katika timu hiyo.
Juma Luizio ni kijana mpya katika timu, mshambulizi huyo wa
zamani wa Mtibwa Sugar kwa sasa anatesa katika ligi kuu ya Zambia akiwa na
Zesco United, hawa ni wachezaji wanne wa uhakika ambao mkufunzi, Martin Nooij
anawategemea katika kikosi chake. Ukichanganya na vipaji vingi vilivyopo katika
ligi ya Tanzania Bara bila shaka umefika wakati ambao Shirikisho la Soka nchini
kutafuta mechi kubwa zaidi hasa na timu za Kaskazini na Magharibi mwa bara la
Afrika ambazo huisumbua mno Stars katika michuano ya kimataifa.
Ndiyo, wakati mwingine ni vizuri kucheza na timu za
kawaida ( mfano, Malawi) kwa kuwa
humsaidia mwalimu kupima uwezo wa wachezaji wake na mifumo yake ya uchezaji,
lakini ni vizuri pia kucheza na timu ambazo huisumbua Stars katika
michuano ( kufuzu AFCON % Kombe la
dunia). Kucheza na nchi kama Misri, Ghana , Brazil, Ivory Coast wakati wa
utawala wa Marcio Maximo ilisaidia sana kuwajenga wachezaji kama Nadir Haroub,
Kelvin Yondan n.k kutokana na viwango vya juu katika ufundi, mbinu na maarifa
ya nchini hizo.
Kucheza na Malawi mara tatu ndani ya miezi 12, ni sawa na
kuendelea kubaki na mbinu zilezile zisizo na mabadiliko licha ya kuwa na vipaji
vingi katika nchi. Samatta, Ulimwengu, Kazimoto, Nadir, Kelvin, ni wachezaji
wanaotakiwa kucheza mechi kubwa zaidi za kimataifa na si kucheza dhidi ya
Malawi mara tatu ndani ya mwaka. Stars inahitaji kucheza na timu kubwa zaidi
katika michezo ya kirafiki ili kuzoea mazingira ya uchezaji ya timu hizo kubwa
barani Afrika ambazo mara nyingi hutufunga na kutuondoa wakati wa mashindano
kutokana na uwezo wetu mdogo kiufundi na kimbinu.
0714 08 43 08
0 comments:
Post a Comment