Na Frank M Mgunga
Mshambuliaji
wa zamani wa klabu ya Simba Zamoyoni Mogella, amelizungumzia pambano la
Jumapili la watani wa jadi Simba na Yanga na kuipa Yanga nafasi kubwa ya
kushinda mchezo huo kutokana na uimara pamoja na matokeo yao katika
mechi za siku za karibuni.
Mogella aliyetamba na kikosi cha Simba miaka ya 80 ameiambia Mpenja Blog,
haipi nafasi kubwa ya timu yake ya zamani kushinda mchezo huo kutokana
na timu waliyokuwa nayo pamoja na ubovu wa viongozi wanayoiongoza timu
hiyo kwa sasa.
“Yanga wananafasi kubwa ya kushinda mchezo wa Jumapili labda wenyewe
wafanye uzembe lakini kwa uimara wa timu yao Simba hawawezi kuzuia
wasipate kipigo kwanza timu yao haina mwendelezo kila siku naona
inamabadiliko lakini kitu kingine migogoro imezidi viongozi wenye kwa
wenyewe hawaelewani,’amesema Mogella.
Mogella anasema anayakumbuka mambo mengi wakati timu yake inapokutana
na Yanga miaka hiyo na namna ushindani unavyokuwepo kwa pande zote
mbili japo baada yamchezo huo wachezaji huwa marafiki
Mogella aliyepewa jina la ‘Golden Boy’ na mashabiki wa Simba kutokana
na kumtesa beki wa Yanga Athuma Juma Chama anasema wakati huo alikuwa
nahakikisha anapambana na kuifungia bao timu yake ili kuonyesha uwezo
wake anapokuwa uwanjani.
“Nakumbuka mwaka 1983 tulicheza na Yanga na kutoka sare ya 1-1 wakati
huo nilikuwa rafiki sana na kipa wa Yanga Steven Nemes lakini
tulipokutana katika mchezo huo tulikuwa kama hatujuani na
niliisawazishia timu yangu bao baada ya Abed Mziba kuifungia Yanga bao
la kuongoza,’amesema Mogella
Mkongwe huyo amesema ili Simba iweze kuifunga Yanga inatakiwa kuanza
kuimarisha kikosi chao kwa kufanya usajili wa wachezaji wenye uzoefu
mkubwa ambao unalingana na wale wa Yanga lakini wanakuwa na wachezaji
wenye uchungu na timu yao kama wakati wanacheza wao.
“Wakati wetu sisi tunacheza ilikuwa tunaweka pembeni mambo ya
migogoro ya uongozi na kila mmoja alikuwa anapambana kwa ajili ya
kuipigania timu yake kitu kama hicho kwa wachezaji wa sasa imekuwa nadra
siyo ajabu ukasikia mchezaji wa Simba kabla ya mechi alikutwa na
kiongozi wa Yanga,”anasema Mogella.
Ingawa Mogella aliwahi kuchezea Yanga miaka ya mwishoni kabla ya
kuachana na mpira lakini anasema yeye ni shabiki mkubwa wa Simba lakini
hafuraishwi na mwenendo wa timu hiyo katika siku za karibuni.
0 comments:
Post a Comment