Azam fc wakifanya mazoezi jana jioni uwanja wa Mkwakwani. Picha kwa hisani ya Salehjembe
COASTAL Union inaikaribisha Azam FC katika mechi ya ligi kuu itayopigwa uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga kesho majira ya saa 10:00 jioni.
Azam fc tayari walishaweka mawindo yao Tanga na jana jioni walifanya mazoezi uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Yanga nao walifanya mazoezi katika uwanja huo jana asubuhi kujiandaa na mechi ya leo jioni dhidi ya Mgambo JKT.
Kuelekea mechi ya kesho, afisa habari wa Coastal Union, Oscar Assenga amesema kikosi chao kina ari kubwa ya ushindi.
"Azam ni timu nzuri, lakini nia yetu ni kuibuka na ushindi ili tuweze kuchukua ubingwa au kushika nafasi tatu za juu".
"Tutapambana kwa nguvu zote na kimsingi maandalizi yote yamekamilika". Amesema Assenga.
Kwa upande wa Azam fc, Meneja wa klabu hiyo, Jemedari Said Kazumari amesema wapo Tanga kwa lengo moja tu la kuvuna pointi tatu.
"Tupo nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi moja na vinara Yanga, kwa muda huu ushindi ni kila kitu tukihitaji kutetea ubingwa wetu. Mechi ya kesho tuko tayari kushindana na tunatarajia kuvuna pointi tatu". Amesema Jemedari.
Yanga wanaongoza ligi kwa kujikusanyia pointi 34 wakifuatiwa na Azam fc pointi 33.
0 comments:
Post a Comment