Na Oswald Ngonyani.
Msimu wa Ligi Kuu ya England umefikia patamu kwa
sasa, hapana shaka mashabiki wengi wa Ligi hiyo wamekaa mkao wa kula tayari kwa
kushuhudia nyakati za mwisho za msimu huu, nyakati zitakazoweka bayana nafasi
ya kila timu katika msimamo wa EPL 2014/2015.
Tumekwishajionea mengi lakini pia kusikia habari
lukuki kuhusu mikakati ya kila timu shiriki katika Ligi ya msimu huu, huku
Klabu ya Chelsea ikionekana kudhamiria vilivyo kuitwaa ndoo ya ‘EPL’ msimu huu
kwa kuendelea kujikita kileleni kwa pointi 63 baada ya kucheza mechi 27.
Tazama, Mashetani wekundu baada ya kuboronga sana
katika ligi iliyopita 2013/2014 chini ya David Moyes wameonekana kujidhatiti
kwa hali na mali ili kuhakikisha kuwa wanairudisha heshima ya klabu yao
iliyokuwa imeyeyuka ghafla, wapo chini ya Van Gaal kwa sasa na ama kwa hakika
wanaonekana kudhamiria kufanya kitu fulani cha muhimu kwa mashabiki wao.
Wakati Mashetani hao wekundu wakionekana kujidhatiti
kunako mbio za ubingwa wa EPL kwa msimu huu, Washika bunduki wa London wao wameonekana
kufanya vema zaidi katika siku za usoni wakichagizwa na uwepo wa mchezaji
tegemeo wa timu ya Taifa ya Chile Alexis Sanchez.
Nakumbuka usajili wa mchezaji huyu aliyekuwa akikipiga
katika klabu ya Barcelona uliwafanya mashabiki wengi wa timu hiyo kuamini kuwa
katika msimu huu wa sasa wa EPL timu yao hiyo huenda ikafanya makubwa zaidi
pengine kuliko ilivyokuwa katika misimu iliyopita.
Ni wazi kuwa uwepo wa Sanchez umeifanya Arsenal iwe
mahali ilipo sasa. Washika bunduki hawa wanashika nafasi ya tatu katika msimamo
wa EPL nyuma ya vinara Chelsea na Man City, wakiwa na hazina ya pointi 58 baada
ya kushuka dimbani mara 28.
Tayari mchezaji wao tegemeo, Alexis Sanchez
amekwishafunga magoli 13 akishika nafasi ya tano katika orodha ya wafumania
nyavu wa EPL msimu huu nyuma ya Sergio Aguero(Man City), Diego Costa
(Chelsea), Charlie Austin (QPR) na Harry
Kane (Sunderland).
AKIWA NA BARCELONA ALIFANYA NINI?
Akiwa
na Barcelona, alifanikiwa kucheza michezo 88 na hata kuitendea vema nafasi yake
ya ushambuliaji kwa kuifungia timu hiyo magoli 39 katika mechi zake zote
alizocheza. Mbali na Barcelona, Sanchez amewahi pia kuchezea vilabu vya
Cobreloa (2005-2006), ambapo alifanikiwa kupangwa katika mechi 47 huku akifunga
magoli 9.
Hakudumu
sana katika klabu hiyo, badala yake alisajiliwa katika klabu ya Udinese ya
nchini Hispania na kufanikiwa kuichezea katika misimu mitano yaani msimu wa 2006-2011 ambapo aliichezea klabu hiyo mechi
95 na kuifungia magoli 20.
MAISHA YAKE YAKE NDANI YA UDINESE YALIKUWAJE?
Akiwa
ndani ya mkataba wa klabu ya Udinese kwa
nyakati tofauti aliwahi kutolewa kwa mkopo na kupelekwa katika vilabu vya Colo- Colo (2006-2007) ambapo akiwa na timu
hiyo alicheza michezo 32 na kufunga magoli 5.
Kama
hiyo haitoshi, katika msimu wa 2007-2008 klabu hiyo ilimtoa kwa mkopo na
kumpeleka katika timu ya River Plate ambapo kocha wa timu hiyo alimpanga
Sanchez katika mechi 23 tofauti huku akifunga magoli 4 ambapo baadaye aliuzwa
na kwenda kukipiga katika klabu ya Barcelona katika msimu wa 2011 alikokipiga
mpaka anahamia Arsenal.
UHAMISHO WAKE KWENDA BARCELONA ULIKUWA NA THAMANI?
Alisajiliwa
na Barcelona kwa mkataba wa dau la Euro 25 milioni, na kuwa mchezaji ghali
zaidi katika historia ya wacheza kandanda wa nchini Chile kwani kabla yake
hakuna mchezaji kutoka Chile aliyewahi kusajiliwa kwa kiasi hicho cha Pesa.
Jicho
la kocha wa klabu ya Arsenal lilimuona, namzungumzia mfaransa aliye muumini mkubwa wa Uchumi
Profesa Arsene Wenger na hata kuamua kutenga kitita cha zaidi ya Euro 30 kwa
ajili ya kuinasa saini yake.
JE WENGER ALIFANIKIWA?
Ndivyo
ilivyokuwa kwani mpaka kufikia Mwezi
Julai mwaka jana 2014 dili hilo liliwekwa hadharani huku kila kitu
kuhusu uhamisho wa mwanandinga huyo kikionekana kukamilika na hata kujikuta
akiweka rekodi ya aina yake kwa Washika bunduki hao akiwa mchezaji wa pili
kusajiliwa kwa dau nono zaidi klabuni hapo.
Sanchez
ameweka rekodi ya kuwa nyuma ya Mjerumani Mesut Özil,
lakini pia ameendelea kuweka rekodi ya kuwa mchezaji kutoka nchini Chile
aliyesajiliwa kwa kitita kikubwa zaidi katika mawanda ya soka ya nchini humo.
VIPI KUHUSU TIMU YAKE YA TAIFA?
Amekuwa
mchezaji tegemezi wa timu ya Taifa ya Chile tangu mwaka 2006 akicheza nafasi ya
kudumu ya ushambuliaji. Akiwa na kikosi hicho cha Taifa ameweza kupangwa katika
michezo 70 lakini pia amefanikiwa
kulichezea Taifa hilo katika fainali mbili za Kombe la dunia yaani mwaka 2010
na 2014. Kwa upande mwingine Sanchez amewahi kulitumikia Taifa hilo katika
michuano ya Copa Amerika mwaka 2011.
Ana jina la utani
analolitumia zaidi anapokuwa nchini kwao lakini pia alikuwa analitumia sana
akiwa na Barcelona, ambapo wachezaji wengi walipenda kumuita Niño Maravilla. Ana
urefu wa Sentimita 168 na uzito wa Kilo 69.
Mwaka 2007 alianza kukichezea kikosi cha timu ya
Taifa ya Vijana cha Chile (U20) ambapo aliweza kukichezea kikosi hicho michezo
12 huku akifunga magoli mawili.
Baada ya hapo akaitwa katika kikosi cha
timu ya wakubwa ambapo amedumu mpaka sasa akiwa amecheza michezo 71 na hata
kufanikiwa kukifungia kikosi hicho magoli 24 (Takwimu hizi ni kabla ya Fainali
za Kombe la dunia za mwaka jana 2014)
Ni wazi kuwa mashabiki wa Arsenal
walikuwa na haki ya kuisubiri EPL 2014/2015 kwa shauku kubwa. Pengini tamati ya
EPL kwa msimu huu 2014/2015 itatoa majibu stahiki ya kinachosubirishiwa.
NGOJA TUSUBIRI
TUONE…….
(Maoni/Ushauri
tuma kwenda 0767 57 32 87 au [email protected])
0 comments:
Post a Comment