Kwa mwanadamu yeyote yule aliye mdau mkubwa wa mchezo wa soka sidhani
kama atakuwa mgeni wa jina hili ‘Zinedine Zidane’ maarufu kama “Zizzou”. Fundi
huyu aliifanyia makubwa sana nchi yake ya Ufaransa.
Nakumbuka wakati akiutangazia umma kuhusu uamuzi wake wa kustaafu soka
mashabiki na wadau wengi wa kandanda walionekana kumshangaa mwanandinga huyu.
Hapana shaka sababu ya wengi kumshangaa ilikuwa ni uwezo wake wa
kusakata ‘Gozi la ng’ombe’ ndani ya dimba, uwezo wa hali ya juu uliowafanya
wengi kuusikitikia uamuzi wake huo wa kutundika daruga mapema.
Alistaafu soka mwaka 2006 baada ya fainali za kombe la dunia ambapo timu
yake ya ufaransa ilitolewa kwa mikwaju ya penalti na Italia, wakati huo alikuwa
na miaka 34 kwani alizaliwa mwaka 1972, kwake miaka hiyo ilikuwa inamtosha
kustaafu, alistaafu na heshima yake iliyotukuka.
Wakati nyakati na enzi zake zikiwa zinapita, mwanandinga huyu mwenye
asili ya kiafrika kutoka katika nchi ya Algeria ameendelea kuwa kivutio cha
wengi huku heshima yake katika mawanda ya soka ikizidi kuimarika.
Alistaafu akiwa amefanya makubwa katika soka, ambapo miaka minne tangu
kustaafu kwake yaani Novemba 2010 mabosi wa Real Madrid walimteua kuwa mshauri
mkuu wa klabu hiyo, hii ilikuwa baada ya maombi ya muda mrefu ya Kocha wa timu
hiyo kwa kipindi hicho Jose Mourinho ambaye anainoa Chelsea kwa sasa.
Baada ya kuridhika na utendaji wake,Baadaye Mwezi Julai mwaka 2011
Uongozi huo uliamua kuketi chini na kumteua kuwa mkurugenzi wa Michezo wa klabu
hiyo, cheo ambacho amedumu nacho kwa muda mrefu mpaka sasa anapoongeza ujuzi
zaidi katika masuala ya ukufunzi wa soka.
Akiwa klabuni hapo Zidane ameendelea kupewa vyeo kadha wa kadha kwani
Mwaka jana 2013 aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo yenye jina kubwa
ulimwenguni kote akimsaida Carlo Ancelloti.
Ni kama kusema Zidane anaitumikia timu ambayo aliichezea kwa mahaba
makubwa, alihamia Real Madrid akitokea nchini Italia katika klabu ya
Juventus.Akiwa klabuni hapo aliiwezesha timu hiyo kufika fainali ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya mwaka 2002 na kufanikiwa
kutimiza ndoto zake.
Kwenye fainali hiyo, Zidane alifunga bao ambalo linaweza kuwa bora kwa
miaka yote ya michuano hiyo.
Mwaka 2003 alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia, ikiwa ni mara yake ya tatu
kupewa tuzo hiyo. Kabla ya hapo aliwahi kutwaa tuzo hiyo kwenye miaka ya 1998
na 2000.
Anasifika kwa uwezo wake wa kubadili matokeo uwanjani, upekee huu unamfanya
azidi kuheshimika ulimwenguni kote.
Ikumbukwe kuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia ya mwaka1998, Zidane alilazimika kungoja hadi
mchezo wa fainali kisha kufunga mabao yake ya kwanza ya michuano hiyo, Ufaransa
ikiirarua Brazili magoli 3-0.
Mabao hayo ndiyo yaliyoipa Ufaransa ubingwa wa Dunia kwa mara ya kwanza,
na hapa hakukuwa na ubishi kuwa, Zidane alikuwa roho ya timu hiyo na pasipo
yeye wala isingekuwa rahisi kwa wafaransa hao kutwaa ubingwa huo mkubwa wa
dunia.
Miaka miwili baadaye, Ufaransa ilitwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya
Ulaya licha ya Zidane kutofunga bao hata moja. Ni wazi kuwa alikuwa ametoa
mchango mkubwa katika mafanikio hayo ya Ufaransa kwa mwaka huo.
Wakati fulani (mwaka 2002) aliandamwa na majeraha, Majeraha ambayo
yalishuhudia timu yake ya Taifa ikipoteza ubingwa wa Dunia kwenye hatua ya
makundi.
Ufaransa ilishindwa kupata hata bao moja katika kinyang’anyiro hicho
ambapo katika mechi yake ya kwanza iliadhibiwa na lililowahi kuwa koloni lake
yaani timu ya Taifa ya Senegal.
Mwaka 2006 ulikuwa wa aina yake kwenye historia ya mchezo wa soka. Mpambanaji
huyu aliweza kuifikisha Ufaransa hadi fainali ya Kombe la Dunia 2006.
Mechi ambayo itakumbukwa na wengi ilikuwa katika hatua ya robo fainali dhidi ya Brazil, ambapo ilikuwa
vita yake na Ronaldinho Gaucho.
Hakuna upekee ulioonekana kwa Gaucho, kwani Zidane alionekana
kumzidi vilivyo Mbrazili huyo na kamwe Ronaldinho hakuweza kufua dafu kwa Zidane,
baada ya dakika 90 kumalizika Brazili ililala kwa goli 1-0 lililokuwa
limefungwa na Thiery Daniel Henry.
Kwa mara nyingine tena aliiwezesha Ufaransa kucheza fainali ya Kombe la
Dunia mwaka 2006, Fainali hiyo ilikuwa ya aina yake kwani ililazimika kuamuliwa
kwa muda wa nyongeza baada ya dakika 90 za awali kumalizika kwa sare ya 1-1.
Pasipo kutegemea mashabiki wa Ufaransa walijikuta wakishika vichwa vyao, baada
ya shujaa wao wa muda mrefu Zinedine Zidane kuonyeshwa kadi nyekundu
zikiwa zimebaki dakika kumi fainali hiyo ifikie hatua ya matuta.
Kadi hiyo ilitolewa baada ya
Zidane kumpiga kichwa beki wa Italia, Marco Materazzi kwa kile kilichodaiwa
kuwa Muitaliano huyo alimtusi.
Ufaransa iliishia kufungwa kwa mikwaju ya penalti na wengi walifikiri kuwa
endapo Zidane asingetolewa, Ufaransa ingekuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa wao
wa pili.
Miaka 34 ni mingi kwa wanasoka wengi lakini uwezo wake ndio uliowafanya
wengi washtushwe na uamuzi wake huo, alistaafu huku akitunukiwa tuzo ya
mchezaji bora wa mashindano hayo ya kombe la dunia ya mwaka huo 2006.
Ilikuwa ni fainali ya kukumbukwa sana katika zama za soka kwani ‘fundi huyo’
Zinedine Zidane alikuwa anamaliza nyakati zake za utawala wa soka huku
akiwaacha mashabiki wake wakimlilia.
(0767 57 32 87)
0 comments:
Post a Comment