MABINGWA mara 24 wa ligi kuu Tanzania bara, Dar Young Africans wamefurahi kuvunja mwiko katika uwanja wa Sokoine, Mbeya baada ya kuvuna pointi sita katika mechi mbili dhidi ya Prisons na Mbeya City fc.
Mkuu wa Idara ya habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amewaambia waandishi wa habari leo makao makuu ya klabu hiyo, Mitaa ya Jangwani, Dar es salaam kuwa kwa miaka mitano iliyopita, Yanga haijawahi kupata matokeo ya kuridhisha, lakini safari hii wameibuka na ushindi wa kishindo.
"Tunashukuru kambi yetu ya siku sita Mbeya imetupa pointi sita na magoli sita. Tumevunja mwiko uwanja wa Sokoine, kwa miaka mitano iliyopita Yanga imesumbuka sana kupata ushindi". Amesema Muro.
Yanga wanaongoza ligi kwa kujikusanyia pointi 31, pointi 4 mbele ya mabingwa watetezi Azam fc wanaoshika nafasi ya pili.
Alhamisi ya wiki iliyopita, Prisons iliwatandika Prisons 3-0 katika mechi ya ligi kuu iliyopigwa uwanja wa Sokoine na jumapili ya wiki iliyopita ikiwafumua 3-1 Mbeya City fc.
Kipigo hicho kimewavuruga City na wamemuondoka kikosini Mlinda mlango chaguo la kwanza la Juma Mwambusi, David Buruhani.
Wakati huo huo, Yanga inaondoka kesho kwenda Botswana kuwafuata BDF XI kucheza mechi ya marudiano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.
Februari 14 mwaka huu, Yanga ilishinda mabao 2-0 dhidi ya BDF kwenye uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Kwasasa Yanga inahitaji ushindi au suluhu au kipigo kisichozidi bao 1-0 ili kuwatupa nje ya michuano wanajeshi hao wa Botswana.
0 comments:
Post a Comment