Meya wa jiji la Mbeya Mh. Athanas Kapunga amewataka wachezaji wa Mccfc kutulia na kujipanga vizuri ili kutafuta pointi tatu muhimu kwenye mchezo ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting unatarajiwa kupigwa jumamosi hii kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa.
Mh Kapunga aliyasema hayo jana jioni wakati wa hafla maalum aliyoindaa kwa wachezaji hao kuwapongeza kwa namna walicheza kwa kiwango bora kwenye mchezo dhidi ya Yanga juma lililopita licha ya kupoteza mchezo huo.
“Najua mlipambana sana, dunia nzima iliona mpira mkubwa mliocheza siku hiyo licha ya kupoteza kwa sababu hata walioshinda walikiri kuwa ninyi mlikuwa bora uwanjani na hakika cha moto walikiona alisema” Mh Kapunga.
Akiendelea zaidi Mh. Kapunga alisema kuwa baada ya kuona jinsi timu ilivyocheza siku hiyo aliamua kuandaa hafla fupi ili kuwapongeza na kuwahakikishia kuwa licha ya kupoteza dhidi ya Yanga lakini uongozi wa jiji bado uko pamoja nao na imani yake kubwa ni City itaibuka na ushindi jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting.
“Tuko pamoja, uongozi wote wa jiji uko pamoja nanyi ndiyo maana jioni hii tumekutana hapa, imani yangu kubwa jumamosi tutapata pointi tatu muhimu, naomba nikuhakikishie Mwalimu Mwambusi wewe pamoja na benchi lote la ufundi kuwa tunatambua kile mnachokifanya kwa ajili ya wanambeya na wapenzi wote wa timu yetu duniani kote tutaendelea kuwaunga mkono mpaka kieleweke” alisema Mh Kapunga na kuwafanya wageni waliohudhuria kumpigia makofi mengi.
Katika hatua nyingine Kocha Mkuu Juma Mwambusi alisema anashukuru kwa Mh Kapunga kuandaa hafla hiyo jambo ambalo limewafanya kuongeza morari kuelekea mchezo wa jumamosi huku akiwataka wachezaji wake kutambua kile kinachofanywa na uongozi wa jiji kwa ajili yao hivyo wahakikishe wanajituma uwanjani ili kutafuta matokeo.
“Tunashukuru kwa hiki ulichokindaa jioni hii kwa ajili yetu na wadau wengine wa City, binafsi naona njinsi ambavyo msukumo wa sisi kufanya vizuri jumamosi unaanzia hapa, kazi inabaki wa vijana wangu kuhakikisha wanajituma uwanjani ili kupata matokeo kitu ambacho ndiyo zawadi pekee kwa uongozi, mashabiki na wadau wa timu yetu” alisema Mwambusi.
Hafla hiyo ilifanyika GR City Hotel na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa Mccfc ikiwa ni pamoja na viongozi na madiwani kutoka jiji la Mbeya.
0 comments:
Post a Comment