Na Oswald Ngonyani
Pengine siwezi kuongopa kama
nitaeleza kuhusu maisha ya Ronaldinho katika enzi zile akiwa na ubora wa hali
ya juu na kuzikonga nyoyo za wapenda soka wengi duniani kote, ni kama kusema
kilikuwa kipindi cha Ufalme wake, naam! Kipindi cha Mfalme Ronaldinho.
Uwezo wake wa kuufanyia chochote
mpira uliwakuna wengi na hata kuzidi kukumbukwa mpaka leo hii katika nyakati za
akina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, ama kwa hakika miaka ile ya 2000 na
ushee ilipendezeshwa sana na umaridadi wa Mbrazili huyu.
Ronaldinho ni nani?
Ni nyota wa nchini Brazili ambaye amekuwa
akicheza soka kama kiungo mshambuliaji na ni mtundu sana wa kuuchezea
mpira akiwakuna wengi awapo ndani ya dimba hasa kutokana na madoido anuai
ayafanyayo awapo dimbani.
Jina lake halisi ni Ronaldo de Assis Moreira, alipewa
jina la Ronaldinho kwa kufuata matamshi ya lugha ya Kireno lakini pia
kujitofautisha na akina Ronaldo wengine ambao ni wengi sana huko Brazil, kama
walivyo akina Mapunda, Tembo, Komba, Ngonyani huko Songea ama akina Mwandosya, Mwambulukutu,
Mwakasege, Mwakasoke jijini Mbeya.
Gaucho ni jina lake la kimichezo ambalo
linamtofautisha zaidi na wanasoka wengineo kama akina Rivaldo, Ronaldo, na wengineo wengi. Ni miongoni mwa wanasoka
wachache waliowahi kuiteka dunia nyakati hizo ambao wanaendelea kuhusudiwa
mpaka sasa.
Aliwahi kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia
mara mbili mfululizo katika miaka ya 2004 na 2005. Alipata mafanikio makubwa zaidi
katika uchezaji soka alipokuwa katika timu ya FC Barcelona ya Uhispania lakini
hata baada ya kuhamia katika kikosi cha AC Milan cha nchini Italia.
Aliwahi
kuvichezea vilabu gani?
Achana na klabu ya Flamengo ya nchini kwao,
Ronaldinho amewahi kuvichezea pia vilabu vya FC Barcelona lakini pia AC Milan na
kuweza kuvifanyia mambo makubwa timu hizo.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni, hakuna atakayenipinga
kama nitatamka wazi kuwa mtalamu huyu wa chenga amepungua kiwango, pengine hali
hii imesababishwa na kuongezeka uzito, lakini pia kutokana na starehe nyingi
anazozifanya baada ya kuwa na fedha za kutosha.
Je, ni
kweli ana fedha za kutosha?
Ronaldinho ni mmoja kati ya wanasoka matajiri
duniani ambaye amepata utajiri huo kupitia uwezo wake wa usakataji wa kandanda
kwenye klabu kubwa duniani na hata kuingia katika mikataba minono na makampuni
makubwa yaliyokuwa yakimlipa kwa matangazo, miongoni mwa makampuni hayo ni
pamoja na Nike na Pepsi. Utajiri wake unakadiriwa kufikia zaidi ya dola Milioni
90.
Amekuwa akipata kiasi cha dola milioni 24 kwa
mwaka. Tazama, alikuwa akipata kiasi cha Euro milioni 25 kwa mkataba wake wa
miaka mitatu katika timu ya AC Milan ya Italia. Lakini pia inasemekana kuwa
alikuwa akilipwa kiasi cha dola milioni 10 kwa mwaka kutokana na mshahara wake
wakati akiwa pale Nou Camp.
Vipi
kuhusu mipangilio yake ya kifedha?
Kama walivyo watu wengine wengi walio na fedha, Ronaldinho
naye hayupo nyuma katika hili, ni mahiri katika matumizi ya pesa hususan katika
kuishi maisha ya kifahari kutokana na faida aliyoipata baada ya kukitendea haki
kipaji chake dimbani.
Anamiliki nyumba kadhaa nchini kwao Brazil lakini
pia barani Ulaya katika nchi ya Hispania. Anamiliki na kuendesha magari ya bei
mbaya na ya kifahari sana kama Mercedes-Benz Eclass na Mercedes-Benz CLS.
Ana gari lenye gharama ya juu zaidi aina ya
Bugatti Veyron ambalo linasifika kwa kuwa na kasi ya ajabu. Gari hilo la
mashindano limekuwa likiteka nyoyo za watu wengi akiwemo Ronaldinho mwenyewe.
Limekuwa na mvumo kama wa nyuki likiwa na uwezo
wa kusafiri kwa kasi ya kilometa 253 kwa saa. Alilinunua gari hilo kwa
dola milioni 1.8. Mara kwa mara aendapo mazoezini hupendelea sana kulitumia.
Ana Hummer H2, ambayo ni imara na yenye
nguvu. Ni gari ya ajabu wakati inapoendeshwa ambayo humvutia kila mtu. Ni moja
kati ya magari yanayopendwa na mastaa wengi wa majuu mmoja wapo akiwa ni mcheza
sinema za kibabe Arnold Alois Schwarzenegger.
Si mtu anayependa kujinyima, amekuwa mfuasi mzuri
wa anasa kama walivyo akina Ronaldo wa Brazili lakini pia akina Ronaldo wa
Ureno. Mara zote anaposafiri safari ya mbali lakini pia hata safari ya karibu amekuwa
akisafiri kwa kutumia ndege ya kukodi na hata kulipa kiasi kikubwa cha pesa.
Ameifanyia
nini Jamii?
Achana na habari za Desemba 8 mwaka
juzi (2013) zilizowahi kutikisa anga la Tanzania kuhusu mwanasoka huyu kutaka
kutoa msaada wa fedha zitakazo tumika kwa
ajili ya ujenzi wa hospitali katika
mkoa wa Singida.
Kutokana
na kufahamika zaidi kwa watu wengi na hata kulifanya jina lake kuwa kubwa,
Ronaldinho amekuwa mwenye ushawishi mkubwa katika jamii na hata kuweza kumiliki
mfuko wa hisani kwa ajili ya kusaidia watu wengine. Wakati fulani aliwahi kugombana
na kaka yake kwa matumizi mabaya ya fedha.
Ametokea
katika familia ya namna gani?
Alizaliwa katika familia ya tabaka la kati nchini
Brazil. Baba yake alikuwa akifanya kazi getini na alipatwa na mkosi wa kufiwa
na baba yake wakati akiwa na umri wa miaka nane tu.
Katika familia yao amezaliwa pamoja na kaka yake
na dada yake.Amekuwa na mahusiano na wanawake wengi wa kariba tofauti na
anajulikana zaidi kwa kuwa na mahusiano na mwanamke wa Kifaransa wakati
alipokuwa Barcelona.
Ana mtoto wa kiume aliyepata kutokana na kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na dansa wa Kibrazil, Janaina Mendes. Ili kujenga
kumbukumbu isiyofutika, aliamua kumpatia mwanaye jina la marehemu baba yake.
Kwa sasa anadaiwa kuoa, awali aliwahi kuoana na Milene Domingues lakini baada
ya muda mfupi walipeana talaka.
Hakika RONALDINHO
GAUCHO: DUNIA HAITAMSAHAU KWA UFUNDI WAKE WA KUUCHEZEA MPIRA UWANJANI.
Wakatabahu wakaa.
(0767 57 32 87)
0 comments:
Post a Comment