Alex enzi za uhai wake
Na Oswald Ngonyani
Nyakati na enzi zingali zikitiririka huku maisha yakizidi
kusonga mbele na historia ikizidi kuwekwa kila jua linapochomoza. Siku zote
kila tunapoianza siku mpya, jana huonekana kuwa na afadhali zaidi kuliko leo.
Hivi ndivyo maisha ya binadamu yalivyo, yanatofautiana
siku hadi siku na mara nyingi siku iliyopita huonekana kuwa na unafuu zaidi
kuliko siku mpya, ni hali ambayo ipo tu wala hauwezi kuikwepa.
Majonzi na masononeko ameumbiwa binadamu. Pengine hata
wanyama wana hulka hiyo lakini kwa sababu hawana utashi inakuwa ni ngumu kwao
kuwalinganisha na binadamu.
“Pumzika kwa amani Christopher Alex
Massawe,mpambanaji mahiri dimbani uliyelala usingizi wa fofofo” nakumbuka sana mchango
wako katika ushindi wa ugenini dhidi ya ZAMALEK ya Misri, Kocha wa enzi hizo JAMES AGGREY SIANG'A alikuwa
anakukubali kuliko kawaida naamini taarifa hizi atazipokea kwa masikitiko
makubwa huko aliko.
Unakikumbuka kikosi cha Simba cha mwaka 2003? Kile kikosi
ambacho kiliwatoa jasho waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano ya klabu bingwa
barani Afrika nyumbani kwao katika dimba la Stade International du Caire?
Naizungumzia klabu ya Zamaleki FC ya nchini Misri ambapo
ubingwa wao ulivuliwa na Jeshi la Msimbazi kutoka Tanzania, timu ya Simba.
Nyuma ya mafanikio hayo makubwa ambayo Simba iliyapata
kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa ameweka historia kubwa sana katika soka la
bongo na Afrika kwa ujumla, Christopher Alex Massawe.
Mpambanaji huyu alifunga penalti ya ufundi na ya ushindi
iliyowapeleka Simba mpaka katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa
kwa ngazi ya Vilabu.
Waarabu wengi wala hawakuamini, walibaki na fadhaiko
mioyoni mwao. Christopher Alex alikuwa ameyeyusha ndoto zao za kuutetea ubingwa
wao waliokuwa wameutwaa katika msimu uliotangulia.
Ilikuwa ni mechi ya marudiano baada ya ile ya awali
kuisha kwa Simba kuibuka na ushindi wa goli 1-0 jijini Dar es Salaam kabla ya
kufungwa 1-0 nchini Misri na baadaye changamoto ya mikwaju ya penalti kuchukua
nafasi yake.
Lilikuwa ni jeshi lililokuwa na mafundi wengi
kama akina Juma kaseja, Said Swedi Ramadhan
Waso Ramadhan, Victor Costa, Boniface Pawasa, 6.Christopher Alex (+), Athuman Machupa,
Suleiman Matola, Emanuel Gabriel, Yusuph Macho Ulimboka mwakingwe na wengine wengi.
Katika Jeshi hilo kuna askari mmoja ambaye kwa bahati
mbaya sana hatunaye duniani kwa sasa, Christopher Alex Massawe kama
nilivyokwishamwelezea katika aya za awali, ameianza safari ambayo kila aendaye
huwa harudi.
Amefariki dunia baada ya kulala kitandani kwa muda mrefu
pasipo kupata nafuu. Mwisho wa siku Mwenyezi Mungu ameamua kumchukua, naam
amelala usingizi wa moja kwa moja, usingizi wa fofofo.
Ni
kama kusema Tanzania imempoteza mmoja kati ya viungo bora kabisa waliowahi
kutamba katika soka la bongo. Umaridadi wake wa kuichezesha timu lakini pia
kufanya maamuzi ya ushindi kwa timu yake ni vitu ambavyo havitakuja
kusahaulika katika vichwa vya wapenda
soka wengi nchini Tanzania.
Ni pigo kwa timu ya soka ya Simba SC kwa
sababu aliifanyia mambo makubwa mno na hata kuchagiza ukulu wake katika
kuuchezea mpira, ni pigo kwa vilabu vya CDA ya Dodoma na reli ya Morogoro kwa
sababu aliwahi kuwa sehemu ya mafanikio yenye tija kwa vilabu hivyo.
Jumapili iliyopita (22/02/2015) saa tatu
za asubuhi ‘askari’ huyu aliianza safari ambayo kila mwanadamu ataipitia, ni
kama kusema ametangulia na sisi tutamfuata.
Amefariki dunia katika hospitali ya
Milembe mkoani Dodoma alikokuwa akitibiwa baada ya kuugua kwa muda mrefu
ugonjwa wa Kifua Kikuu.
Taarifa sahihi kutoka kwa Mama yake mzazi Bi Martha
Matonya aliyekuwa akimuuguza amesema walimfikisha hospitalini hapo Ijumaa ya
wiki iliyopita baada ya kuona hali yake inazidi kuteteleka.
Alisema ilipofika Jumamosi hali yake
ilibadilika, akashindwa kuongea hadi alipofariki siku iliyofuata.
Kwa simanzi na uchungu mkubwa Mwanamama huyu
aliweka bayana mateso aliyokuwa ameyapata mtoto wake kabla ya kufikwa na umauti;
“Mwanangu hali yake ilibadilika akawa
hana uwezo hata wa kuongea ila ameteseka sana afadhali akapumzike’’Ndivyo
alivyonukuliwa akisema Bi Matonya baada ya kumuuguza mtoto wake mpendwa kwa
muda mrefu pasi mafanikio.
Marehemu Christopher
Alex, alizaliwa Septemba 12 mwaka 1975,na kupata elimu yake ya msingi katika
shule ya msingi Uhuru na kumaliza katika shule ya Chamwino huko Dodoma mwaka
1993,na alianza kucheza mpira kwenye timu ya Daraja la nne Chamwino UTD na
baadaye daraja la tatu akiwa na kikosi cha Aston Villa nayo ya Dodoma.
Mwaka 1999-2001 aliitumikia klabu ya CDA ya Dodoma,kabla ya kutimkia klabu ya
Reli mwaka 2002 na baadaye kujiunga na wekundu wa msimbazi Simba,Marehemu
ameacha mtoto mmoja aitwaye Alex.
“A Lion Never Die, He Just Lays There Sleeping” Kwa maana Simba huwa hafi,
analala tu chini kupumzika. Mungu aiweke Roho ya marehemu Christopher Alex
mahala panapo Stahili, Ameen.
‘Kwa maana huyu alionekana anampendeza Mungu, akachukuliwa’
Yeyey mbele yetu, sisi nyuma yake.
(0767 57 32 87) au
[email protected]
0 comments:
Post a Comment