Jina lake linaonekana kuzungumzwa tena na tena kwa
sasa, hii inatokana na mwenendo usiotia matumaini kwa kikosi anachokinoa, mwenendo
ambao tayari umekwisha wagawa mashabiki wengi wa ‘The Gunners’.
Kitendo cha kuendelea kuwa mdebwedo kwa Man United
ni miongoni mwa sababu ambazo zimewafanya mashabiki wengi wa Arsenal kumuona
Arsene Wenger kama sababu ya timu yao kuasua sua.
Wengi wanaamini kuwa Wenger ana kikosi kizuri, tena
kizuri sana tatizo linakuja katika namna ya kuwatumia wachezaji aliokuwa nao
yaani mfumo wa kiuchezeshwaji ndani ya dimba lakini pia uteuzi anaoufanya kwa
kikosi chake cha kwanza, wengi huamini kuwa anakosea.
Tangu ajiunge na Arsenal, Wenger amepitia katika
nyakati tofauti tofauti, nyakati ambazo kwa kiasi fulani zimempa heshima kubwa
sana lakini pia kwa upande mwingine zimemweka katika masononeko makubwa baada
ya kukinzana na matakwa ya mashabiki wa timu husika.
NYAKATI TAMU ZA
WENGER KWA ARSENAL
Nakumbuka Msimu
kamili wa kwanza wa Arsene Wenger 1997/98 katika uwanja wa Highbury,
ulishuhudia Arsenal kwa mara ya pili katika historia yake ikifanikiwa kunyakua
vikombe vyote viwili; cha Ligi Kuu na FA na kumwezesha mfaransa huyo kuchukua
tuzo ya Carling ya meneja bora wa mwaka, ni nyakati ambazo alionekana kuwa
tumaini jipya na jema kwa wakereketwa wengi wa ‘The Gunners’.
Ni katika nyakati hizo Dennis Bergkamp akawa
mwanasoka bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Soka (FWA) na
mwanasoka bora wa mwaka wa Chama Cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA).
Msimu huo huo uling’ara zaidi kwa wanasoka wa
Arsenal kutoka nchini Ufaransa Emmanuel Petit na Patrick Vieira baada ya kutoka
kutoa mchango wao mkubwa katika ushindi wa timu yao ya taifa katika fainali za
kombe la Dunia 1998.
Arsenal kwa miaka mitatu mfululizo ikakamata nafasi
ya pili na mwaka 2001, Arsenal ikafika kunako robo fainali ya Kombe la Mabingwa
wa Ulaya kabla ya kutolewa na Valencia ya nchini Hipania.
NYAKATI TAMU
ZAIDI ZA WENGER PALE HIGHBURY
Kipindi cha 2001/02 mambo yakawa mazuri zaidi kwa
Wenger na Arsenal yake pale walipoweza tena kuchukua vikombe vyote viwili kwa
kuichapa Chelsea katika fainali ya FA na kubeba kombe la ligi kwa kuilaza
Manchester 1-0 katika mechi kali ya kukumbukwa katika uwanja wa Old Trafford na
kufikisha rekodi ya michezo 13 bila ya kufungwa.
Nakumbuka katika msimu huo mzima hawakuwahi kufungwa nyumbani. Hivyo Arsene Wenger akatajwa kuwa meneja bora wa mwaka wa
Barclays huku Robert Pires akitajwa kuwa mwanasoka bora wa Chama cha Waandishi
wa habari za michezo (FWA).
Msimu uliofuata Arsenal wakashindwa kwa ufinyu
kubakisha kombe lakini wakaweza kuwa klabu ya kwanza kwa zaidi ya miaka 20 kuweza
kubakisha kombe la FA baada ya kuilaza Southampton 1-0.
Ni katika kipindi hicho mchezaji wa Kihistoria wa
timu hiyo, Thierry Henry akachaguliwa na PFA na FWA kuwa mchezaji bora wa
mwaka. Henry akawa ameweza kujiunga na Bergkamp katika orodha ya wachezaji
walioweza kuifungia Arsenal magoli 100.
WENGER
NA REKODI YA KUTOPOTEZA MCHEZO HATA MMOJA KATIKA EPL
Msimu wa 2003/04 Arsenal ya Wenger ikamaliza michezo
yote bila ya kufungwa na kuchukua taji la ubingwa wa ligi (EPL). Pia walimaliza
michezo yote wakiwa pointi 11 mbele ya mshindi wa pili Chelsea na kubeba taji
kwa mara ya 13.
Wakati huo huo Cesc Fabregas ambaye aliwasili
Arsenal mwezi wa kwanza, akaweza kuweka rekodi ya aina yake ya kuwa mchezaji
mdogo kabisa kuchezea Arsenal akiwa na umri wa miaka 16 na siku 177 wakati
msimu unamalizika.
Vipigo vya nusu fainali ya FA walivyovipata kutoka
kwa Manchester United na robo fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya toka kwa
Chelsea vikaondoa matumaini yote ya kunyakua vikombe vitatu. Rekodi ya
kutofungwa ikaendelea msimu uliofuata na mwezi wa nane Arsenal ikaipiku rekodi
ya Nottingham Forest ya kucheza muda mrefu bila ya kufungwa katika EPL.
KUTOKA HIGHBURY
MPAKA EMIRATES
Kampeni ya 2005/06 ilikuwa ya mwisho katika uwanja
wa Highbury ambao ulikuwa ni makazi ya Arsenal kwa miaka 93. Timu ikaweza
kukamata nafasi ya nne mwisho wa msimu na kuweza kupata nafasi ya kushiriki
Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa wakati wote ilipokuwa Highbury, rekodi ya
Arsenal ni kama ifuatavyo: Michezo 2,010; kushinda 1,196; sare 475; kufungwa
339; magoli 4, 038; magoli ya kufungwa 1,955.
REKODI TAMU ZAIDI
YA KUCHEZA FAINALI YA UEFA
Msimu wa 2005/06 Arsenal iliweza kufanya kazi kubwa na
nzuri iliyoonekana kuwapendeza wanazi wengi wa klabu hiyo. Washika bunduki hao waliweza
kufika fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya maarufu kama UEFA.
Mbali na kufika fainali ya UEFA, pia waliweka rekodi
ya kucheza Michezo 12 bila ya kufungwa ikijumuisha rekodi mpya ya mashindano,
kutofungwa katika mechi 10 mfululizo. Mwenendo huo wa aina yake ukawawezesha Washika
bunduki hao kumenyana na Barcelona katika fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya
tarehe 17 mwezi Mei katika dimba la Stade de France.
Licha ya Jens Lehman kupewa kadi nyekundu baada tu
ya dakika 18 za mchezo, washika bunduki walikuwa wa kwanza kufunga bao kupitia kwa
mlinzi Sol Campbell. Hata hivyo mwishoni mwa kipindi cha pili, Barcelona
wakapachika mabao mawili na kuumiza mioyo ya mashabiki wa Arsenal waliofunga
safari kuishangilia timu yao huku wakiamini kuwa wangeutwaa ubingwa huo kwa
mara ya kwanza ndoto ambayo iliyeyushwa na akina Samuel Etoo pale Stade de
France.
MAISHA
NDANI YA UWANJA MPYA WA EMIRATES
Wakati klabu ikijiandaa kuhamia Emirates, nahodha
wao na mfungaji bora kabisa katika historia ya klabu, Thierry Henry akaweka
dhamira ya kubaki Arsenal kwa siku zijazo. Baadaye akiwa Ujerumani katika kombe
la Dunia akaweza kuisaidia nchi yake kufika fainali. Mwezi wa saba 2006 klabu ikahama
rasmi Highbury ambako ilidumu kwa miaka 93.
Dennis Bergkamp akacheza mechi yake ya mwisho kwa
Arsenal na ya kwanza kabisa ndani ya uwanja mpya wa Emirates wakati Ajax
Amsterdam inapambana na Arsenal katika mechi maalumu ya kumuaga mwanasoka huyo
nguli.
UHAMISHO WA
THIERY HENRY NA KUSTAAFU KWA MKONGWE BERGKAMP
Baadaye tangu kustaafu kwa Dennis Bergkamp lakini
pia tangu kuondoka kwa akina Thiery Henry na Patrick Viera kwa kiasi kikubwa
klabu ya Arsenal ikaanza kupoteza umaarufu wake wa kuwa klabu tishio nchini
England.
Pamoja na kudumu na Wenger kwa kipindi chote hiki
bado mashabiki wake hawataki kuridhika na mwenendo wa kikosi hicho kwa siku za
karibuni huku wengi wakionekana kushinikiza Arsene Wenger kuondoka Emirates kwa
lengo la kuirudisha hadhi ya timu yao.
Mara kwa mara mashabiki wamekuwa wakionekana
kulalamika sana lakini tofauti na mategemeo ya wengi, mabosi wa The Gunners
wanaonekana kumkumbatia sana Wenger, nadhani kuna tija wanayoipata kutoka kwa
Mfaransa huyu, tija ambayo haipo wazi kwa mashabiki.
Rekodi yake kwa kiasi kikubwa inaonekana kuvutia
sana, hapana shaka mashabiki wanataka ayafanye mambo aliyokwishawahi kuyafanya
siku za nyuma hususan katika msimu wa 2003/2004 ili kuiweka Arsenal katika
ubora wake, tofauti na ilivyo sasa.
Kabla yake, klabu ya Arsenal wala haikuwa na uteja
wa kudumu kwa vilabu vya Man U na Chelsea. Lakini kwa siku za karibuni washika
bunduki hao wameonekana kuwa mteremko sana kwa vilabu hivyo na hata kuwafanya
mashabiki wake wakose amani mioyoni mwao.
Wanaitaka Arsenal yao, Arsenal ile iliyowahi
kumaliza Ligi pasipo kupoteza mchezo, Arsenal ile iliyowahi kucheza fainali ya
UEFA, Arsenal ya ukweli iliyowafanya mashabiki wake watembee kifua wazi huku
wakijidai.
0 comments:
Post a Comment