Na Shaffih Dauda
MWISHONI mwa juma hili wawakilishi wa Tanzania
bara katika michuano ya kimataifa barani Afrika, Azam fc na Yanga wanacheza
mechi za marudiano ugenini.
Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara,
Azam fc watachuana na Al Merreick ya Sudan katika mechi ya marudiano ligi ya
mabingwa Afrika itayopigwa mjini Khartoum, Sudan.
Mechi ya kwanza iliyochezwa uwanja wa Azam
Complex, Chamazi, Mbande, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, februari 15
mwaka huu, Azam fc waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mabao hayo yalifungwa na Mrundi, Didier Fortune
Kavumbagu na nahodha mwandamizi, John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
Katika mechi ya marudiano Azam wanahitaji ushindi
wowote ule au suluhu, sare ya 1-1 au kutofungwa zaidi ya goli 1-0 ili kusonga
hatua inayofuata.
Wakati Azam fc wakiwa Khartoum, mabingwa mara 24
wa ligi kuu Tanzania bara, Dar Young Africans watakuwa mjini Gaborone, Botswana
kuchuana na maafande wa Jeshi, BDF XI.
Mchezo wa kwanza uliopigwa februari 14 mwaka huu uwanja
wa Taifa, Dar es salaam, Yanga walishinda mabao 2-0.
Mabao yote mawili yalifungwa na mfungaji bora wa
ligi kuu msimu uliopita, Amissi Joselyn Tambwe.
Yanga wanahitaji suluhu, sare ya 1-1 au kutofungwa
zaidi ya goli 1-0 ili kusonga mbele.
Kuelekea katika mechi hizo mbili kubwa, tayari
kumezuka mambo ya mizengwe na fitina, hususani kwa waarabu wa Sudan.
Miaka yote waarabu wamekuwa bora kwenye michezo ya
fitina na wamekuwa wakifanikiwa kutimiza malengo yao. Kumbuka kinachozikumba
timu za Tanzania, Simba, Yanga zinapoenda kucheza nchi kama Misri.
Nakumbuka Zamalek waliofungwa goli 1-0 na Simba
uwanja wa Taifa mwaka 2003, walifanya fitina nyingi ndani na nje ya uwanja nchini
Misri ili kuwatupa Simba nje ya mashindano, lakini Simba walijipanga na
kujikita katika maandalizi na kuchukulia ‘poa’ mizengwe yote.
Simba walifungwa goli 1-0 kama ambavyo waliwafunga
Zamalek Dar es salaam, ngoma ikaisha kwa wastani wa bao 1-1 na Simba wakashinda
kwa penalti na kuwavua ubingwa Zamalek.
Penalti ya ushindi ilifungwa ma Christopher Alex
Massawe aliyefariki dunia jumapili iliyopita Hospitali ya Milembe, Dodoma
kutokana na maradhi ya kifua kikuu yaliyomsumbua kwa muda mrefu. Mungu ailaze
mahala pema peponi roho ya marehemu. Amina.
Waarabu walichukia sana kutolewa na Simba , walihamanika
kwasababu mipango yao haikutimia.
Nimetumia mfano huo ambao sijaeleza kiundani zaidi
Simba walikwepaje fitina kwasababu sio lengo la makali hii, kikubwa nataka
kuwapa mbinu wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.
Azam na Yanga wasipambane na zile timu (Al
Merreick, BDF XI) kutokana na fitina au mizengwe,
inabidi wakubali kisaikolojia kujiandaa vizuri.
Kwa uzoefu wangu, mara nyingi huwa tunaingia
kwenye mtego wa wale jamaa kwasababu ya sisi kuhamanika (ku-paniki). Kwa mfano
Azam walivyopewa basi bovu vile nchini Sudan, wao hawatakiwi ku-paniki,
wakubali, waendelee na mipango yao.
Wasiwape nafasi Waarabu ya kuonekana wamekasirika.
Viongozi waliombanata na timu wakikasirika, muda wa kufanya maandalizi unapungua
na umakini wa kufanya maandalizi ya mchezo unapungua pia, kwasababu akili
nyingi inahamia kutegua au kupambana na fitina.
Hata Mashabiki wenyewe kisaikolojia watakuwa
wamejiandaa kuwaondoa mchezoni Azam, hizo ndio mbinu zao.
Wachezaji wakiamini wanaonewa, wanapoteza
malengo,wanapunguza umakini, wakiingia kwenye mechi unakuta akili yao tayari
inaamini kuwa jamaa wamewafanyia vurugu,
mwisho wanakula 4-0, dakika 90’ zinakwisha, wamepigwa na wao wanasonga mbele.
Kwa kutumia uzoefu huo, mbinu pekee ni kutojali kabisa kwa kila
wanachofanyiwa, wakubali, wachukulie
kama changamoto, wasihamishe malengo ya maandalizi ya mchezo kwenda kupambana
na fitina.
Wao wamsikilize mwalimu, watengeneze mipango ya
mchezo, waende wakacheze mechi tu. Wasiingie uwanjani wakiwa na wasiwasi.
Kwa mfano wale Waarabu wanaweza kujiangusha, hata
marefa wengine walishapangwa ili wachezaji wa Azam wafanye makosa ya kijinga ili
penalti itolewe. Kwa mazingira hayo wachezaji watakasirika na kuamini wanaonewa.
Azam na Yanga wayajue yote hayo kuanzia nje hadi ndani ya uwanja kwenye mechi.
Wachezaji wawe makini kutofanya makosa au ‘faulo’
zozote zile, waepuke kuwashika ili kutotengeneza mazingira ya kuwapa faida
yoyote ile.
Kwa mfano wakishafanikiwa kutowapatia ‘faulo’ dakika 15’ za kipindi cha
kwanza, mipango yao itakuwa haijafanikiwa na wao ‘wana-paniki’. Azam watatulia
na watakuwa wameshawazoea na hapo ndipo
mpira utachezwa vizuri.
Wanachotakiwa kufanya Azam na Yanga ni kujikita
katika maandalizi yao na kuepuka kuingia kwenye mtego wowote wa kutaka
kushindana na fitina. Mimi nawapa mbinu hiyo, wakifanya hivyo tu, matokeo
mengine yatakuwa ya kimchezo tu na ya kawaida.
Kwa mfano lile Basi walilopewa lisiwaondoe katika
misingi ya kuiandaa timu kiufundi na kimbinu, wasiingie kwenye fitina.
Wao wangewaambia Al Merreick kuwa “Tunashukuru kwa
basi lenu, ni zuri, lakini kuna wenzetu
wametupatia usafiri mwingine, tunashukuru kwa usafiri huu mliotupatia”
Msikasirike kwa kupewa basi bovu, nyie mnakuwa
watulivu mkiamini uwezo wao umeishia pale, mkifanya hivyo wao ndio ‘wana-paniki’.
Mkipaniki nyie wao wanakuwa wamefanikiwa, kwahiyo ni kufanya kinyume tu.
Kila la kheria Azam, Yanga katika mechi zenu za
marudiano, Watanzia wengi wapo nyuma yenu!!
0 comments:
Post a Comment