Na Oswald Ngonyani
Hapana shaka Msimu wa 2003-2004 utaendelea kukumbukwa
na mashabiki wengi wa Arsenal duniani kote kutokana na mambo makubwa yaliyokuwa
yamefanywa na wapiganaji wa kikosi hicho, wapiganaji ambao waliongozwa na
Thiery Henry na Patrick Vierra.
Kumbukumbu zinaeleza kuwa ulikuwa ni msimu wa
12 wa Arsenal katika Ligi Kuu nchini England (EPL) lakini pia msimu wa 74
mfululizo katika ligi ngazi ya juu katika soka la England.
Binafsi nitauadadavua Msimu huu kwa mapana
yake ili kuweza kuuelezea upekee wa Washika bunduki hawa nyakati hizo, enzi
ambazo kila mchezaji alionekana kuwa na mchango mkubwa ndani ya dimba tofauti
na ilivyo sasa.
Ni kweli, Msimu wa 2003/2004 unabaki kuwa wa
historia katika katika klabu ya Arsenal lakini pia kwa upande fulani katika
historia ya mchezo wa soka nchini England. Arsenal ilifanya kitu fulani ambacho
kimeifanya iheshimike mpaka sasa.
Timu hii kutoka London ya Kaskazini iliweza
kumaliza msimu mzima wa ligi pasipo kupoteza mchezo wowote na kuifanya kuwa
timu ya pili kuingia katika historia ya soka kwa kumaliza msimu mzima bila
kufungwa. Timu ya kwanza ikiwa ni Preston North End mwaka 1889, timu zote hizo
zimepewa majina ya utani "The Invincible" (Yaani timu zisizofungika)
Wakati fulani, Meneja wa Arsenal Mfaransa aliye muumini mkubwa
wa uchumi, Arsene Wenger alitabiri mwaka 2002 kwamba ana kikosi bora
kinachoweza kumaliza msimu mzima bila kufungwa.
Alikuwa hatanii, Ni kweli mafanikio hayo
yalifikiwa japokuwa hali haikua hivyo katika michuano mingine ambayo kikosi
hicho kilishiriki mwaka huo kwani waliweza kutolewa na Chelsea katika hatua ya
Robo fainali ya Ligi ya mabingwa ulaya (UEFA) na kufika hatua ya nusu
fainali katika Kombe la FA na lile kombe la Ligi ( Carling Cup zamani hivi sasa
ni Capital one)
AKINA NANI WALIMPA KIBURI WENGER?
Nakumbuka baada ya kikosi cha Wenger kukubali kufungwa 2-1
na Liverpool msimu uliotangulia katika fainali ya kombe la FA wakati
wakitangulia kwa goli 1-0.
Msimu mpya ulipoanza Wenger alimsajili mlinda
mlango Jens Lehmann kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa paundi milioni
1.5 huku akiwapa mikataba mipya wachezaji wake nahodha Patrick Viera na winga
Robert Pires.
Giovanni van Bronckhorst alisajiliwa
kutoka Rangers kwa paundi milion 8.5 wakati Sol Campbell alijiunga na Arsenal
akitokea kwa wapinzani wa jadi Spurs.
Kinda Francis Jeffers alijiunga akitokea Everton kwa
ada ya uhamisho paundi milion 8. Janichi Inamoto na Richard Wright, Johan
Djourou, Gael Clichy,Cesc Fabrigas pia waliongezwa kikosini wakati msimu
mpya ulipokaribia.
Wapambanaji hawa waliungana
na wachezaji wengine waliokuwepo kikosini katika kuweka historia. Hapa
alikuwepo Mfungaji bora wa msimu huo Thiery Henry aliyekuwa amefunga magoli 30
katika ligi na magoli 39 katika michuano yote.
Walikuwemo pia akina Ashley Cole,Patrick
Viera,Martin Keown,Fredrick Ljungberg, Dennis Bergkamp,Sylvain Wiltord, Lauren,
Edu,Gilberto Silva,Reyes, Nwankwo Kanu, Kolo Toure na wengineo.
UKWELI KUHUSU MATOKEO
YA THE GUNNERS KWA MSIMU MZIMA WA LIGI
Ni kweli umaridadi wa kikosi cha Wenger
katika msimu wa 2003/2004 ulikifanya kikosi hicho kiwe gumzo katika mawanda ya
soka la ndani na nje ya England. Siyo Ulaya tu hata nje ya bara hilo bado ukulu
wa Arsenal ulizidi kuzungumzwa.
Arsenal ya wakati huo ilifanikiwa kuzifunga
timu zote zilizokuwa zinashiriki EPL katika msimu huo isipokuwa vilabu viwili
pekee Man United na Portsmouth, vilabu ambavyo viliambulia sare katika mechi zote mbili dhidi ya Arsenal.
Msimu ulimalizika na Arsenal kuweka historia mpya katika Ligi
kuu England kwa kushika nafasi ya kwanza ikitawazwa mabingwa wapya wa
England.
Wanaume hawa walicheza jumla ya mechi 38, na
kushinda mechi 26, sare 12 pasipo kupoteza mchezo wowote.
Walifunga magoli 73 na kufungwa magoli 26 na
kupata jumla ya pointi 90 kati ya magoli hayo, 30 yalifungwa na Thierry Henry
ambaye aliibuka kinara wa kufumania nyavu katika EPL msimu huo.
WAPAMBANAJI HAWA WAPO WAPI KWA SASA?
Wengi wao wamestaafu soka kwa sasa huku mfungaji wao kwa miaka yote tangu
kuanzishwa kwa klabu hiyo, Thiery Heinry akiwa amestaafu soka na kujikita
katika mawanda ya uchambuzi wa kandanda katika kituo maarufu cha televisheni
cha Sky sport.
Akina Jens Lehmann, Lauren, na Sol Campbell, wote hawa
wamekwishastaafu soka kwa sasa na kufanya mambo mengine lakini akina Kolo Toure
na Gilberto Silva wangali wakisakata ‘Gozi la ng’ombe’
Patrick Viera aliajiriwa na mabosi wa timu hiyo kama Afisa wa
Maendeleo ya Soka wa klabu ya Manchester City huku Dennis Bergkamp akihudumu
katika klabu ya Ajax akama kocha msaidizi.
Ama kwa hakika kilikuwa ni kipindi ambacho Mashabiki wengi wa
Arsenal wangependa sana kijirudie, lakini
mambo yameendelea kwenda ndivyo sivyo kwa Washika bunduki hao na hata
kujikuta wakiwa wasindikizaji wa kila mwaka katika mbio za ubingwa katika EPL.
Hapana shaka Profesa Wenger ana kazi ya ziada, kazi ya
kuirudisha Arsenal ile iliyokuwa imemaliza Ligi pasipo kupoteza mchezo na hata
kutwaa ubingwa wa EPL mapema. Si kazi rahisi, akili ya ziada inatakiwa kutumika
zaidi vinginevyo mambo yataendelea kuwa yale yale.
Nawasilisha hoja……….
(0767
57 32 87)
0 comments:
Post a Comment