Na Oswald Ngonyani
SIKU zote shabiki wa mpira miguu huenda uwanjani
kufanya kazi mbili kubwa, Kushangilia na kuzomea. Huishangilia timu yake lakini
pia huizomea timu pinzani inapocheza na timu yake, huo ndio ukweli.
Nadharia hii ya shabiki kushangilia timu yake
wakati mwingine huweza kuyeyuka kama barafu iwapo wachezaji wa timu husika
wataonekana kufanya tofauti na vile inavyotegemewa na mashabiki hao.
Hapo mashabiki wenye hasira na wenye mioyo
isiyoweza kuvumilia huweza kufanya mambo kinyume na ilivyozoeleka, kuizomea
timu yao hiyo na hata kuishangilia timu pinzani.
Mara nyingi hali hii huchagizwa na msukumo wa
hasira ndani ya mioyo yao lakini pia hufanywa na mashabiki wachache sana
waliokosa ari ya uzalendo ndani ya nafsi zao.
Mashabiki ambao kiufundi ni wachezaji namba 12 wa
timu husika ni watu wanaopenda kupendezwa na kufurahishwa muda wote. Hawapendi
kukosa amani mioyoni mwao kwa timu yao kuvurunda.
Hii ndivyo ilivyo kwa klabu ya Simba kwa sasa
ambapo kuna kila dalili ya mashabiki wake kukosa fanaka mioyoni mwao kutokana
na mwenendo usio hila wa timu yao kwa sasa japo inacheza kandanda safi la
kuonana.
Pengine kuna kitu chenye nguvu ya ziada zaidi nyuma
ya matokeo haya mabovu ambayo imekuwa ni kawaida sasa kwa timu ya Simba
kukumbana nayo ndani ya uwanja wa Taifa lakini pia nje ya Uwanja wa Taifa.
Kipigo cha ugenini dhidi ya Stand United mjini
Shinyanga kimeonekana kuwaghadhibisha mashabiki wengi sana wa Mnyama. Wengi
walitegemea Simba kuvuna pointi tatu za muhimu kunako mchezo ule lakini mambo
yakawageuka.
Ni wazi kuwa kipigo hicho kimeifanya Simba iendelee kubakia na pointi zake 20 katika
nafasi ile ile ya nne nyuma ya vinara Yanga, Azam, na Kagera Sugar.
Pengine ni jambo linaloweza kuleta hasira zaidi
kwa mashabiki wake hasa kwa utofauti wa pointi uliopo baina ya timu zote zilizo
juu yake, huku Pointi za mpinzani wake Yanga zikionekana kuwa tishio zaidi.
Wakati Yanga ikiwa na pointi 31 Simba yenyewe ipo
nyuma kwa tofauti ya pointi 11, si jambo la heri, ni wazi kuwa jitihada za
dhati zinahitajika ili kuirejesha shauku ya kuufukuzia ubingwa wa VPL
vinginevyo msimu huu wa 2014/2015 unaweza ukawa ni msimu wa tatu mfululizo kwa
Vijana hawa kuwa na ukame wa Kikombe hicho cha Ligi Kuu.
Tangu timu hiyo ianze kuchechemea kunako VPL
tayari kuna mambo mengi makubwa yamekwishafanyika klabuni hapo ili kuweza
kuirudisha hadhi ya timu hiyo.
Kuboresha posho za wachezaji lakini pia kuboresha benchi la ufundi ni miongoni
mwa mambo machache kati ya mengi ambayo yamefanywa na Uongozi wa juu wa timu
hiyo.
Pamoja na jitihada zote hizo bado mwenendo wa klabu
ya Simba umeendelea kuwa wa kinyonga na hata kuwafanya watu waanze kuhoji
sababu zilizo nyuma ya matokeo hayo.
Alikuwepo Zdravco Logarussic lakini akatimuliwa
mapema kabisa kwa lengo la kuifanya Simba iendelee kuwa Simba. Akaja kocha
mpole na mzoefu wa soka la bongo, Mzambia Patrick Phiri lakini yalimkuta yale
yale ya Loga.
Mwishoni mwa Mwezi Januari mwaka huu 2015 KOCHA wa
sasa wa Simba Mserbia, Goran Kopunovic alimkabidhi rasmi beki chipukizi, Hassan
Isihaka Unahodha wa klabu ya Simba SC, huku kiungo Jonas akiwa msaidizi wake.
Kopunovic alifanya uteuzi huo baada ya mazoezi ya
muda mfupi Uwanja wa Boko Veterani, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam lengo
likiwa kuwapa ari ya kujiamini wachezaji wa kikosi hicho ambapo wengi wao ni
vijana wadogo.
Nakumbuka alifanya uteuzi huo, kuelekea mchezo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mabingwa watetezi, Azam FC ambao
ulimalizika kwa sare ya goli 1-1 kufuatia magoli yaliyofungwa na Emmanuel Okwi
(Simba) na Kipre Tchetche (Azam).
Pamoja na kuteua Manahodha hao wote walioibuliwa
katika mfumo wa soka ya vijana ya klabu, Kopunovic pia aliteua jopo maalum la wachezaji
‘watu wazima’ kama viongozi wa wachezaji wenzao lengo likiwa kukiimarisha
kikosi hicho kinachochagizwa na kauli mbiu ya ‘Nguvu Moja’.
Hao ni kipa Ivo Mapunda, beki Nassor Masoud
‘Chollo’ na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi ambao jukumu lao lilikuwa
kuwaongoza wachezaji wenzao, ambao wengi wao ni vijana wadogo.
Mambo yote hayo yameendelea kufanyika kwa lengo la kuirudisha
hadhi ya Simba, hadhi ambayo kwa kiasi kikubwa imeshuka kutokana na vile kikosi
hicho kilivyo kwa sasa lakini bado haijasaidia kitu.
Kikosi cha Simba wala hakitishi, kila timu katika VPL
inaonekana kuitamani Simba. Akina Stand United, Mbeya City na hata Kagera Sugar
wamekwishajipigia tayari.
Ni wazi kuwa akina Prisons, Mgambo na wengineo wengi pamoja
na ukibonde wao watakuwa na hamu kubwa ya kukutana na Simba hii ambayo
inaonekana kukosa dira.
Kwa siku za usoni kikundi fulani
cha wanachama walioenguliwa na Uongozi wa Rais Evans Aveva kimeonekana kupewa
sana lawama na huku mashabiki wengi wa klabu hiyo wakimtaka Rais wao kukaa meza
moja na Kikundi hicho.
Imani ya mashabiki wengi wa Simba inawatuma
katika kuamini kuwa Kikundi hicho ndiyo sababu ya timu yao kukosa matokeo.
Wengi wanaamini sababu ya timu yao kusuasua ni
jitihada za Kikundi hicho maarufu kama ‘Simba Ukawa’ kuzorotesha ustahimilivu
wa kikosi hicho kwa lengo la kuukomoa Uongozi wa timu hiyo uliowafuta uanachama
japo mara kwa mara Bw. Aveva ameonekana kulikanusha hilo.
Binafsi silipi sana nafasi suala hilo la ‘Simba
Ukawa’, pengine wanasimba wenyewe wanaujua ukweli uliopo nyuma ya mwenendo huu
wenye kukatisha tamaa kwa timu yao.
Ni wazi kuwa Uongozi husika chini ya Bwana Aveva
unajua cha kufanya ili kuhakikisha kuwa mashabiki wa ‘Mnyama’ wanapata kile
ambacho wanakihitaji tofauti na ilivyo sasa.
Wahenga walisema ‘Usiku wa deni haukawii kucha’Ni
jambo jema sana kama akina Aveva watachukua hatua mapema kabla Ligi haijafikia
ukingoni ili kuirudisha ari ya kuwania ubingwa wa VPL kwa msimu huu 2014/2015,
kinyume na hapo watakuwa wamewaweka njia panda Mashabiki wao.,
Tamati rasilimali
0767 57 32 87
0 comments:
Post a Comment