YANGA SC imeondoka alfajiri ya leo kwenda Botswana kuwafuata wapinzani wao, BDF XI watakaochuana nao katika mechi ya marudiano ya kombe la Shirikisho itayopigwa mwishoni mwa wiki hii, mjini Gaborone.
Mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa Dar es salaam (Februari 14 mwaka huu), Yanga walishinda mabao 2-0.
Mabao yote yalitiwa kambani na mfungaji bora wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu uliopita, Amissi Tambwe.
Kabla ya mechi hiyo, Yanga wamefanya maandalizi wakitumia mechi mbili za ligi kuu dhidi ya Prisons na Mbeya City fc.
Waliwafunga Prisons 3-0 alhamisi ya februari 19 na wakashinda 3-1 dhidi ya Mbeya City jumapili ya februari 22 mwaka huu.
Dida, Msuva, Sherman na Tegete wakiwa uwanja wa Ndege leo alfajiri tayari kwa safari ya kwenda Gaborone.
Katika mechi hizo mbili zilizopigwa uwanja wa Sokoine, Mbeya, Yanga waliweka rekodi ya kukaa siku sita Mbeya, wakafunga magoli sita katika mechi mbili, wakavuna pointi sita na kufungwa goli moja. Ulikuwa mwendo wa sita-sita.
Licha ya ushindi huo, Yanga walicheza soka zuri na walifanya mashambulizi mazuri na kujilinda vizuri kuanzia safu ya ulinzi mpaka kiungo.
Salum Telela, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Amissi Tambwe, Andrey Coutinho, Mrisho Ngassa walikuwa katika ubora huko Mbeya.
Safu ya ulinzi ikiongozwa na Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Juma Abdul na Oscar Joshua walilinda lango lao na kuruhusu goli moja katika mechi mbili.
Ugumu wa Prisons na Mbeya City umewafanya Yanga wapate kipimo kizuri zaidi.
Kumbuka wanakwenda Botswana wakiwa na mtaji wa magoli 2-0, hivyo wanahitaji kufungwa si zaidi ya goli 1-0 au sare ya aina yoyote.
Kwa kiwango walichokuwa nacho Yanga wanaweza kushinda hata Botswana. Kocha Hans van der Pluijm si muumini wa soka la kujihami.
Anapenda kumiliki mpira, kugongeana pasi za uhakika na kushambulia kwa kasi.
Hata alipotolewa na Al Ahly ya Misri mwaka jana ligi ya mabingwa Afrika kule Misri alicheza soka la kujiamini na la wazi.
Kocha huyo wa Kidachi anaenda Botswana bila shaka kwa staili ileile ya kushambulia na kujilinda vizuri.
Kinachotakiwa kufanyika ni kuwa makini na mfumo atakaotumia. BDF XI si timu ya kubeza, inatakiwa wachezaji wa Yanga waamini kuwa wamefungwa hata kama walishinda.
Wacheze kwa kujituma na kutofikiria ushindi wa Dar es salaam. Zamani mcheza kwako alikuwa anatunzwa kwa kiwango kikubwa, sahizi mpira umekuwa wa kisayansi, hata ugenini unaweza kushinda.
Yanga wanaweza kuichapa BDF tena, kikubwa waongeze umakini safu ya ulinzi na kiungo, halafu washambuliaji wasiwe wachoyo kwa kila mtu kukata kufunga.
Yeyote atayefunga ni faida kwa klabu, unaweza kung'ang'ania kufunga hata kona isiyowezekana kwa lengo la kuonekana umefunga, kumbe kuna mwenzako alikuwa sehemu nzuri zaidi, hivyo ni muhimu kupeana nafasi.
Kucheza ugenini kuna presha, wenyeji wanatawala kwa kila kitu nje ya uwanja, ardhi yao, mashabiki wao, hivyo wanaweza kufanya mambo mengi kuwatoa mchezoni, lakini Yanga wana uzoefu mkubwa na wala haiwezi kuwa tatizo.
Vijana wa Pluijm tulieni, msiwe na papara, mnaweza kuwataoa nishai BDF hata huko kwako.
Kila la kheri Yanga! Watanzania tuko nyuma yenu.
0 comments:
Post a Comment