Wakati Ligi Kuu ya England (EPL) ikiwa inazidi kushika kasi,
hapana shaka nitakuwa sijakosea iwapo nitawazungumzia wachezaji wachache katika
Ligi hiyo ambao kwa kiasi kikubwa usajili wao ulionekana kutia fora zaidi kabla
ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi 2014/2015.
1.
Angel Di Maria
Mwanandinga huyu raia wa Argentina ni
kama ‘Lulu’ kwa sasa katika kikosi cha Mholanzi Louis Van Gaal ambapo mashabiki
wengi wa Man U wanaamini kuwa uwepo wake utachagiza ari ya ushindi katika
kikosi chao hicho ambacho msimu uliopita hakikuwa na jipya.
Mabosi wa ‘Man U’ wala hawakuwa na
hiyana, walijikuta wakiweka mezani mzigo wa pauni Milioni 59.7 kumng’oa katika
klabu yake ya Real Madrid na hata kuanza maisha mapya pale Old Trafford. Usajili
wake umeonekana kutia fora zaidi.
2. Alexis Sanchez
Siku zote imezoeleka kuona klabu ya
Barcelona ikiinyima raha klabu ya Arsenal kwa kuwapoka wachezaji wake tegemezi,
safari hii mambo yameonekana kwenda kinyume kwani Alexis Sanchez alijikuta
akiihama klabu yake ya Barcelona na hata kutua kunako mitaa ya Fly Emirates.
Pengine uwepo wa mafundi wengi pale
Nou Camp ulimfanya nyota huyu kutoka Chile kuridhia kuihama klabu hiyo lakini
pia mabosi wake kutokuwa na kinyongo katika hilo.
Ni kama kusema amekwenda kuongeza
nguvu zaidi katika kikosi cha Profesa Wenger huku mashabiki wengi wa ‘Washika
bunduki’ hao wakionekana kusubirishia makubwa.
Amesajiliwa kwa Pauni Milioni 35.
3. Diego Costa
Mashine ya Chelsea inayoonekana kuwa
mhimili katika kikosi cha Jose Mourinho. Umakini wake katika kucheka na nyavu
umemfanya awe na jina kubwa na hata kuzidi kuwanyima raha wapinzani katika EPL.
Mabosi wa Cheslea hawakuwa na hiyana,
walimsajili kutoka katika klabu ya Atletico Madrid kwa dau nono la Pauni
Milioni 32. Tangu ajiunge na Chelsea tayari amekwisha ifanyia makubwa timu hiyo
katika EPL na hata kuiweka timu hiyo katika Uongozi wa Ligi kwa sasa.
4. Eliaquim Mangala
Pamoja na kuwa na shehena la
wachezaji wenye vipaji, Matajiri hawa wa England (Man City) wala hawakubweteka
kufanya usajili.
Mazungumzo yao dhidi ya klabu ya FC
Porto ya nchini Ureno yalikuwa na tija kubwa na hata kufanikisha kuinasa saini
ya mwanasoka huyu aliyetua Etihad kwa ada ya Pauni Milioni 32.
5. Cesc Fabregas
Klabu ya Barcelona bado imeonekana
kuwashangaza wengi msimu huu hasa kwa kujikuta ikiwatoa kirahisi sana wachezaji
wake tofauti na misimu iliyopita.
Kitendo cha kuondoka kwa wachezaji
Alexis Sanchez kwenda Arsenal lakini pia Cesc Fabregas kwenda Chelsea
kimewashangaza wengi lakini huo ndio ukweli.
Katika hili Mourinho wala hakupuuzia,
Pauni Milioni 30 zilitosha kabisa kumhamisha makazi Fabregas kutoka Nou Camp
kwenda Stamford Bridge na kwa kiasi kikubwa amekuwa bingwa wa kutoa pasi za
mwisho ‘assists’ zenye tija kwa The Blues.
6. Ander Herrera
Hii ni mashine
nyingine ya ‘Man U’ iliyosajiliwa kutoka katika klabu ya Atletic Bilbao na hata
kuongeza nguvu katika kikosi kilichokuwa ‘mdebwedo’ msimu uliopita. Uhamisho
wake umegharimu kitita cha Pauni Milioni 29 na tayari amekwishaanza kuonekana
kuwa msaada katika maskani yake mapya ya Old Trafford.
7. Romeru Lukaku
Aliungana na
Samuel Etoo’ kusema kwaheri kunako klabu ya Chelsea na hata kuanza maisha mapya
katika maskani ya klabu yake mpya ya Everton huku mashabiki wa timu hiyo
wakitegemea makubwa kutoka kwake.
Dau la Pauni
Milioni 28 lilitolewa pasipo kuwa na kinyongo na mabosi wa klabu ya
Everton huku usajili huo ukionekana
kukipa nguvu zaidi kikosi hicho kilicho katika nafasi ya 12 kwa sasa baada ya
kucheza michezo 26 huku ikijikusanyia pointi 28 mpaka sasa.
8. Adam Lallana
Jina lake si
ngeni katika masikio ya mashabiki wengi wa soka hususan mashabiki wa EPL. Kwa
kipindi chote alichoitumikia Southampton, mwanandinga huyo amekuwa kila kitu
ndani ya kikosi hicho na hata kuwa sehemu ya kufanya vema kwa timu hiyo katika
mechi za msimu uliopita.
Majoogoo wa
Jiji, klabu ya Liverpool wala hawakufanya masihara katika zoezi zima la kuinasa
saini ya mpambanaji huyu. Kitita cha pauni Milioni 25 kimempeleka pale Anfield
na kutengeneza kikosi chenye mafundi wengi kama akina Gerald, Balloteli,
Henderson, na wengineo.
9. Dejan Lovren
Ni kama kusema
Liverpool wameamua kukibomoa kikosi cha Southmpton baada ya kuwachukua
wachezaji wengi kutoka klabuni hapo.
Dejan Lovren
si maarufu hivi kwa mtu ambaye hafuatilia mchezo wa soka lakini kwa wale
wenzangu na mimi ambao ulevi wetu mkubwa ni soka ni lazima wataniungana mkono
kuwa Liverpool imepata Jembe ndio maana haikusita kutenga Pauni Milioni 20 na
kumjumuisha kundini mwanandinga huyu asiye na jina katika EPL.
10. Lazar Markovic
Orodha ya
wachezaji waliotikisa katika usajili wa Msimu Mpya wa Ligi ya EPL inatamatika
kwa mtalaamu huyu. Pengine ninaweza nikapata maswali mengi ya kwanini
sijamjumuisha katika orodha hii mchezaji kama Mario Ballotelli wa Liverpool au
Danny Welbeck wa Arsenal.
Unajua
kwanini? Tazama thamani ya usajili wao lakini pia linganisha usajili huo na
wanasoka hawa niliowaainisha katika makala yangu haya.
Klabu ya
Liverpool imemsajili Lazar Markovic kutoka Benfica kwa dau nono la Pauni
Milioni 20 na hata kuzidi kuongeza nguvu katika kikosi hicho cha Anfield. Hapana
shaka atakuwa msaada mkubwa kwa Majogoo hao wa Jiji ambao Msimu uliopita
almanusura watwae ubingwa wa EPL.
Tamati natamatika…….
(0767 57 32 87 au [email protected].
0 comments:
Post a Comment