Na
Oswald Ngonyani
SIKU zote Historia ya
mwanadamu inajengwa na mwanadamu mwenyewe hususan katika kile ambacho anakifanya katika
mwenendo mzima wa maisha yake ya kila siku, maisha ambayo yanaendana na makuzi
yake pia.
Kitu chochote kile kiwe
kizuri au kibaya kinaweza kikamfanya mtu akumbukwe tena na tena na walimwengu
hasa kutokana na upekee wa kitu hicho, leo hii dunia haiachi kumkumbuka shabiki
mkubwa wa klabu ya Arsenal ya nchini Uingereza, Osama bin Laden aliyekwisha
tangulia mbele ya haki kwa sasa.
Kwanini anakumbukwa
sana? Jawabu la mdawaka huu lipo wazi, “Septemba 11” ndilo jibu stahiki la
swali hili, mwanamume huyu aliongoza shambulio la kigaidi katika moja ya
majengo makubwa na muhimu ya Serikali ya nchi ya Marekani maarufu kwa jina la
‘Pentagon’ zilikuwa nyakati za Urais wake Bwana George W. Bush.
Marekani haikuwa tayari
kumsamehe Osama, ilijikuta ikihatarisha hata maisha ya raia wake kwa lengo la
kumsaka gaidi huyu. Harakati hizo zilitamatika baada ya kifo chake ambacho
kilichagizwa na majeshi ya Marekani katika enzi za rais wa sasa Barrack Obama.
Katika soka, mpaka leo
hii mchezaji bora wa dunia katika miaka ya 1998, 2000 na 2003 mfaransa Zinedine
Yazid Zidane maarufu kama ‘Zizzou’ amegoma kabisa kumuomba msamaha Mlinzi Marco
Materrazi wa Italia.
Kwanini? Hapana shaka
Fainali ya kombe la dunia ya mwaka 2006 iliyofanyika Juni 13 nchini Ujerumani
inakumbukwa vizuri na wanafamilia wengi wa mchezo wa soka. Fainali hiyo
ilihusisha nchi za Italia dhidi ya Ufaransa.
Katika fainali hiyo
iliyotamatika kwa changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya dakika 120
kumalizika kwa sare ya 1-1, Zidane hakuweza kumaliza dakika hizo baada ya
kutolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kosa la kumpiga kichwa mlinzi huyo wa Italia.
Zinedine Zidane mwanasoka
mahiri aliyekuwa ameuteka ulimwengu wa
soka kwa wakati huo alilazimika kuiaga familia ya wapenda soka kwa namna ambayo
dunia ya soka ilibaki midomo wazi.
Ulikuwa ni mwisho
wenye huzuni, mwisho wenye kusononesha kwa mpambanaji huyu. Haukuwa mwisho
wenye heri, ilikuwa tamati yenye kufadhaisha sana inayozungumzwa mpaka leo hii
katika vinywa vya walimwengu wapenda soka.
Mara baada ya tukio
lile mashabiki wa soka nchini Ufaransa walitangaza kumsamehe Zidane,
shujaa wao wa siku nyingi aliyelipa heshima kubwa Taifa hilo hususan kutoa
mchango mkubwa katika fainali ya mwaka 1998 dhidi ya Brazili na kuiwezesha
Ufaransa kutwaa taji hilo tena kwa ushindi mnono wa goli 3-0.
Waliamua
kuonyesha wazi mapenzi yao kwa Zidane. Lakini, ulimwengu wa soka haujakoma
kujiuliza maswali tofauti tofauti yanayolenga kujua sababu ya Nguli huyu
kufanya tukio lililomharibia sifa kiasi kile. Naam tukio la kumtwanga ‘ndoo’ ya
kifua Materrazi.
“Bora nife kuliko kumuomba radhi Materrazi” Aliwahi
kutamka Zidane mbele ya halaiki ya waandishi wa habari kuonesha msimamo wake
kwa kile alichokuwa amekifanya uwanjani.
Inasemekana kuwa kabla
ya kupigwa kichwa hicho kilichompeleka chini, Materrazzi alikuwa amemtusi
‘Fundi’ huyo wa chenga, tusi ambalo lilishindwa kuvumilika ndani ya nafsi ya
Zidane na kuamua kufanya maamuzi yaliyowashangaza wengi.
Ni kama kusema imebaki
historia kwa sasa, historia isiyofutika katika viriba vya ubongo wa mashabiki
wengi wa soka duniani kote, wakati wengi wao wakitaka kujua matusi aliyotukanwa
mfaransa huyo, yeye mwenyewe ameweka bayana kuwa kamwe hatakuja kuyajutia
maamuzi yake hayo.
Maisha yangali yakienda
kasi sana huku enzi zikizidi kujenga historia za kila namna. Mpaka leo hii
mashabiki wa soka ulimwenguni kote wangali wakikikumbuka kichwa cha Zidane huku
kila shabiki akionekana kufikiri tofauti.
Nakumbuka muda mfupi
tangu kustaafu kwake Zidane alitoa kitabu kilichoeleza ukweli kuhusu maisha
yake tangu utotoni mpaka ukubwani. Kwa waliokisoma kitabu hicho huenda wakawa
wamepata majibu ya kwanini Zidane alimpiga kichwa Materazzi.
Historia ya maisha
yake inaeleza kuwa alifika Ufaransa na wazazi wake akiwa mtoto mdogo sana.
Wazazi wake walikuwa wakimbizi kutoka katika nchi ya Algeria. Zidane huyu
alijikuta akiishi maisha ya umasikini kwenye moja ya vitongoji vya mji
wa Marseille kutokana na ukata wa wazazi wake.
Kitabu hicho kinazidi
kudadavua kuwa kuwa tangu utotoni Zidane amekuwa akigombana sana na watoto
wenzake na hata waliomzidi umri. Amekuwa akipigania haki yake tangu
utotoni, alichukia sana kubaguliwa kutokana na rangi ya ngozi na nywele
zake.
Pamoja na FIFA kuwa na
kampeni maalum ya kupinga ubaguzi wa rangi katika soka la sasa,
inasemekana kuwa moja ya sababu zilizomfanya Zidane ashindwe kuvumilia na
kufikia uamuzi wa kumpiga kichwa Materrazi ni kitendo cha beki
huyo kumuudhi Zidane kwa maneno ya kibaguzi na kudhalilisha wakati wa
mchezo huo wa fainali.
Lilikuwa ni tukio
lililowasikitisha wapenzi wengi wa soka hususan mashabiki wa Ufaransa, tukio
ambalo lilimfanya mwanaume huyu aamue kustaafu soka akiwa katika ubora wa hali
ya juu wa kuuchezea mpira, maamuzi ambayo mashabiki wengi wa soka walionekana
kutoyakubali kutokana na ukweli kuwa kiwango chake bado kilikuwa juu.
Mpaka leo hii
anakumbukwa kwa heshima aliyojijengea katika soka ambapo pamoja na kutenda kosa
hilo tuzo ya mchezaji bora wa Fainali hizo za mwaka 2006 zilienda kwake huku
jamii ya wanasoka duniani kote ikionekana kuridhia.
Naomba kuwasilisha………
(0767 57 32 87) au [email protected]
0 comments:
Post a Comment