MICHUANO ya soka ya kuwania kombe la Utalii ‘Utalii Cup 2015’ inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Februari 23, kwenye viwanja mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Msemaji wa mashindano hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya michezo ya Bos Promotions, Samuel Peter, alisema maandalizi yanakwenda vizuri na bingwa atazawadiwa Ng’ombe.
Peter alisema mbali ya zawadi hiyo, washindi wa kwanza pia watapata nafasi ya kutembelea moja ya mbuga za wanyama zilizopo nchini.
Alisema lengo la michuano hiyo ni kuibua vipaji vya wanasoka chipukizi jijini Dar es Salaam na kutangaza utalii wa ndani kupitia mchezo wa soka.
Msemaji huyo alisema timu 12 zinatarajia kushiriki na zitapangwa katika makundi mawili ambapo nne za juu kutoka kila kundi zitafuzu kwa hatua ya robo fainali.
Peter alisema milango ipo wazi kwa timu ya daraja lolote inayotaka kushiriki mashindano hayo yatakayokuwa yakifanyika kila mwaka.
“Maandalizi yanakwenda vizuri na tayari tumeshaanza kutoa fomu kwa timu zinazotaka kushiriki na namba ya mawasiliano ni 0714 743276”, alisema.
0 comments:
Post a Comment